Rais Samia Azindua Mpango Wa Maendeleo Kwa Ustawi Wa Taifa Na Mapambano Dhidi Ya UVIKO 19.

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Samia Suluhu Hassan, leo tarehe 10 Oktoba, 2021 amezindua Mpango wa Serikali wa Kuinua Uchumi na kukabiliana na janga la Korona, UVIKO -19 wenye thamani ya shilingi trilioni 3.62  katika hafla iliyofanyika katika ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dododma.

Akizungumza wakati wa uzinduzi wa Mpango huo, Mhe. Rais Samia ameitaka Wizara ya Fedha na Mipango pamoja na Taasisi nyingine zitakazonufaika na fedha za mkopo wa Shilingi trilioni 1.3 kutoka Shirika la Fedha Duniani (International Monetaruy Fund-IMF) kuhakikisha zinatumika katika malengo yaliyokusudiwa.

Mhe. Rais Samia amebainisha kuwa fedha hizo  za mkopo wa masharti nafuu kutoka IMF zitatumika katika kutekeleza Miradi ya Maendeleo ikiwemo kuboresha huduma za jamii katika sekta ya Afya, Elimu, Utalii na Maji.

Aidha, Mhe. Rais ameitaka sekta binafsi kutumia fursa hiyo kwa kuzalisha bidhaa zitakazotumika katika utekelezaji wa miradi hiyo mfano uzalishaji wa saruji, mabati na nondo ili tusiwe na sababu ya kuchelewa kutumia fedha hizo.

Mhe. Rais Samia ameagiza miradi hiyo itekelezwe na wakandarasi wazawa ili fedha hizo ziendelee kubaki na kuzunguka katika uchumi wetu.

Aidha, amewataka Wakandarasi hao wazawa kuwajibika kwa kufanya kazi kwa ubora, umakini na ufanisi.

Katika Mpango huo ambao unatakiwa kutekelezwa ndani ya miezi 9, Mhe. Rais Samia ametaka kutumika kwa utaratibu wa manunuzi wa single source ili kupunguza urasimu katika ununuzi wa vifaa vya ujenzi wa miradi hiyo.

Aidha, Mhe. Rais Samia amemuagiza Waziri wa Fedha na Mipango Dkt. Mwigulu Nchemba kusimamia na kuondoa urasimu wa misamaha ya kodi katika vifaa na bidhaa zitakazotoka nje ya nchi ambazo zitatumika katika Mpango huo.

Vilevile Mhe. Rais Samia amemuagiza Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) pamoja na Mkaguzi wa Hesabu za ndani kufatilia kwa karibu matumizi ya fedha hizo ili malengo na thamani halisi iweze kuonekana.

Mhe. Rais Samia amezitaka Kamati za Bunge kuisimamia kikamilifu miradi hiyo wakati wa kuitembelea. Pia amewataka Wakurugenzi wa Halmashauri zote nchini pamoja na timu zao kuhakikisha wanasimamia vizuri fedha hizo ili ziweze kuleta tija katika miradi hiyo.

Aidha, Mhe. Rais Samia ameishukuru IMF kwa mkopo huo wa masharti nafuu utakaosaidia katika utekelezaji wa Mpango huo. Pia Mhe. Rais Samia amewashukuru wadau wengine wa maendeleo wakiwemo Serikali ya China, Benki ya Dunia na Umoja wa Ulaya kwa kuonesha nia ya kuunga mkono katika utekelezaji wa mradi huo.

Katika hafla hiyo, Mhe. Rais Samia pia amezungumzia mafanikio ya Serikali ya Awamu ya Sita katika kipindi cha miezi sita na kusema kuwa   Miradi yote mikubwa ya kimkakati iliyoasisiwa katika Awamu ya Tano ikiwemo ujenzi wa Reli ya Kisasa (SGR), Ujenzi wa Bwawa la kufua umeme wa Mwalimu Nyerere (Rufiji), madaraja pamoja na barabara, inaendelea vizuri na inatarajiwa kukamilika katika muda uliokusudiwa.

Aidha, Mhe. Rais Samia amewapongeza wasanii pamoja na wanamichezo mbalimbali walioiwakilisha Tanzania katika mashindano ya kimataifa hususan Timu ya Taifa ya Wanawake Twiga Stars kwa kutwaa ubingwa wa mashindano ya COSAFA wanawake 2021.


Jaffar Haniu

Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu.

 


 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akihutubia Taifa kwenye uzinduzi wa kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma leo tarehe 10 Oktoba 2021.



Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan, akizungumza na Makamu wa Rais Dkt. Philip Isdor Mpango na Rais wa Zanzibar Dkt. Hussein Mwinyi nje ya Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma mara baada ya kuzindua rasmi kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 leo tarehe 10 Oktoba 2021.

  

Baadhi ya viongozi mbalimbali waliohudhuria wakifatilia hotuba ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan,(hayupo pichani) wakati wa uzinduzi wa kampeni ya Maendeleo kwa Ustawi wa Taifa na Mapambano dhidi ya Uviko-19 katika Ukumbi wa Jakaya Kikwete Jijini Dodoma leo tarehe 10 Oktoba 2021.

PICHA NA IKULU

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments