SIMBA SC YAPEPERUSHA BENDERA YA TAIFA BOTSWANA

 WAWAKILISHI pekee wa Michuano ya Ligi ya Mabingwa Afrika kutoka Tanzania, Simba SC wamepeperusha vyema Bendera ya taifa baada ya kupata ushindi wa bao 2-0 ugenini nchini Botswana dhidi ya wenyeji Jwaneng Galaxy FC kwenye mchezo wa mkondo wa kwanza wa Michuano hiyo uliopigwa katika dimba la uwanja wa taifa la nchi hiyo mjini Gaborone

Simba SC walianza vyema kipute hicho kipindi cha kwanza kwa kupata mabao yote mawili katika dakika ya 2 na 6 kupitia kwa Mshambuliaji wake mkongwe, John Raphael Bocco aliyeunganisha safi krosi za Bernard Morrison na Rally Bwalya na kuifanya Simba SC kwenda  mapumziko kwa kuongoza mchezo huo kwa mabao hayo 2-0.

Kipindi cha pili kilianza kasi kwa Simba SC ambao walilazimika kulinda mabao hayo huku Jwaneng Galaxy wakitaka kusawazisha. Simba SC walifanya mabadiliko kuwatoa Bernard Morrison na kuwaingia Duncan Nyoni, pia walimtoa Sadio Kanoute akaingia Erasto Nyoni huku akitoka Rally Bwalya na kumpisha Mzamiru Yassin, na John Bocco alimpisha Meddie Kagere.

Mchezo wa mkondo wa pili unatarajiwa kuchezwa Oktoba 24, 2021 katika dimba la Benjamin Mkapa Dar es Salaam huku Jwaneng Galaxy FC wakitakiwa kuwafunga Simba SC mabao 3-0 ili kusonga mbele hatua ya Makundi ya Michuano hiyo mikubwa barani Afrika katika ngazi ya vilabu.

Benchi la Ufundi la Simba SC liliongozwa na Kocha Thierry Hitimana wakati Kocha Mkuu Didier Gomes Da Rosa akishuhudia mtanange huo jukwaa kutokana na kukosa vigezo vilivyowekwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) msimu huu wa Mashindano hayo

Kikosi cha Simba SC kilichoanza kwenye mchezo huo ni:- Kipa, Aishi Salum Manula, Mabeki, Shomari Kapombe, Mohammed Hussein, Henock Inonga Baka, Pascal Wawa, Viungo, Taddeo Lwanga, Sadio Kanoute Rally Bwalya, Washambuliaji ni Bernard Morrison, Hassan Dilunga na John Bocco.

Upande wa Jwaneng Galaxy FC walianza na Ezekiel Morake, Mphayamodimo Keiponye, Thabo Leinanyane, Lesego Keredilwe, Gape Mohutsiwa, Gilbert Baruti, Moagi Sechele, Thabang Sesinyi, Resaobaka Thatanyane.

Wachezaji wa Simba SC, Nahodha John Bocco, Henock Inonga Baka, Taddeo Lwanga na Sadio Kanoute wakishangilia moja ya bao la timu hiyo katika mchezo wa Ligi ya Mabingwa Afrika dhidi ya Jwaneng Galaxy FC, Simba SC wameondoka na ushindi wa bao 2-0.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments