Tuongee kiume: Nini maana ya ndoa

Wakati Serikali, dini na karibu kila taasisi ikiwa na maana yake ya ndoa, wanaume pia tunazo tafsiri zetu tena nyingi na zenye kufurahisha. Na leo tunaonyeshana baadhi ya tafsiri hizo.

Ndoa ni kumuita mwanamke aje atumie pesa zako, kisha aone haitoshi, azae marafiki zake ili washirikiane kula pesa zako zaidi.

Kisha baadaye ukianza kufulia marafiki zake waseme tumelelewa na kuhudumiwa na mama, mzee alikuwa anazingua tu, hajatusaidia kwa lolote, alikuwa mtu wa mitungi, wanawake na starehe.

Na mzee mmoja aliulizwa na mwanaye, baba ni gharama kiasi gani kuoa? Mzee akajibu, sijui mwanangu, bado naendelea kulipia.

Pia wapo wanaosema ndoa ni mapenzi, na mapenzi ni upofu, kwa hiyo ndoa ni upofu. Na kuna wanaosema maisha ni ndoto nzuri za usiku na ndoa ni ‘alarm’.

Kanisani watu wanapooana mfungisha ndoa huita ndoa pingu za maisha; na nikukumbushe, mara yako ya mwisho kuziona pingu ilikuwa ni kwenye matatizo, au mtu alikuwa anakamatwa na polisi au ametekwa na magaidi, au uliziona zikining’inia kiuoni mwa askari anayekwenda kukamata muhalifu. Pia nikukumbushe soksi zinauzwa elfu moja, pingu zinaweza kufikia elfu thelathini, lakini ukiuliza mtu mwenye birthday wiki ijayo umletee zawadi gani? Soksi za elfu moja au pingu za elfu thelathini atachagua soksi.

Pia nina uhakika methali ya ndoa ndoano sio ngeni masikioni mwako.

Wengine wanaielezea ndoa kwa soga, wanasema mtu akikupigia simu, akasema amemteka mke wako wa ndoa kitu bora zaidi unachoweza kufanya ni kumuacha abaki na mkeo.

Na wengine wanaielezea ndoa kwa nahau, wanasema mwanaume bila kuoa hajatimia, na mwanaume bila kuoa hajateketea. Patamu hapo. Pia ukiona mwanaume anamfungulia mke wake mlango wa gari ujue kuna mawili, gari ni jipya au ndoa mpya.

Bado sijakwambia kuhusu wanaosema kuwa ndoa ni kama karata mchezo wa ‘last card’, isipokuwa karata zote ni majokeri,zamu ya kucheza ni ya mwenza wako.

Kuna mwingine alisema ndoa ni kutafuta mtu ambaye atakukera maisha yako yote.

Wakati kuna wahenga wanasema kinyume na kila tulichoongea hapo juu, wanasema hivi ‘aliyebarikiwa ni yule aliyepata rafiki wa kweli, lakini mwenye baraka ni yule aliyepata rafiki wa kweli ambaye ni mke wake. Ninachokisema ni tunaweza kuongea maana za ndoa kwa mujibu wa wanaume mpaka asubuhi.

Nyingi zitatuelezea upande wa ubaya kwa sababu wengi wanapitia upande huo ilihali kuna baadhi wanaziona ndoa kama pepo. Kwa hiyo yote kwa yote ukipata nafasi jitahidi uoe.

Ukibahatika kupata ndoa njema utaishi kwa furaha miaka yote ya uhai wako na ukipata ndoa mbaya pia hakijaharibika kitu, utakuwa mwanafilosofia.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments