Uamuzi wa Jaji Siyani kesi ya kina Mbowe hatua kwa kwa hatua-2

Jana katika toleo la kwanza la mapitio ya uamuzi wa kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na watu wengine watatu waliowahi kuwa askari wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ), tuliona jinsi mawakili wa utetezi walivyopinga maelezo ya onyo ya mshtakiwa wa pili, Adam Kasekwa yasipokelewe mahakamani kama kielelezo.

Mawakili wa utetezi waliweka mapingamizi mawili ya kuitaka mahakama isipokee maelezo hayo kama kielelezo, kwa madai kuwa hayakutolewa kwa hiari kwani mshtakiwa aliteswa kabla na wakati akichukuliwa maelezo.

Walitaka pia mahakama isipokee maelezo hayo kama kielelezo, wakidai yalichukuliwa nje ya muda, yaani saa nne tangu mshitakiwa alipokamatwa.Tuliona pia jinsi upande wa Jamhuri ulivyoanza kupangua hoja hizo kufuatia kuibuka kwa kesi ndogo ndani ya kesi ya msingi inayowakabili kina Mbowe. Endelea…

Upande wa Jamhuri waliendelea kudai kuwa wakati Kasekwa akidai kupitia mapingamizi yaliyowekwa na mawakili wake kuwa maelezo yake hayakutolewa kwa hiari, mshtakiwia huyo, mbali na kueleza kuwa alitishwa na kulazimishwa kusaini baadhi ya nyaraka, lakini wakati wa ushahidi wake alikana kutoa maelezo au kuteswa wakati akiwa Dar es Salaam.

Soma hapa: Mwanzo, mwisho uamuzi wa Jaji Siyani

Kwa maoni ya Wakili wa Serikali mwandamizi, Robert Kidando tofauti ya maelezo ya Kasekwa hayakuwa na ukweli.

Akirejea uamuzi wa Mahakama ya Rufani katika kesi ya James Rugemalira dhidi ya Jamhuri, Kidando alidai kuwa ni sharti kuwa kesi lazima ziamuliwe kutokana na masuala yaliyorekodiwa na mahakama na kama kuna upande unataka kuongeza masuala ya kuamuliwa, lazime yaingizwe kwanza kwenye rekodi ya mahakama .

Alisema yanayotakiwa kuamuliwa katika kesi iliyokuwa mbele yao ni yale tu yaliyorekodiwa na mahakama Septemba 15, 2021 pale upande wa utetezi ulipoleta mapingamizi dhidi ya kupokelewa kwa maelezo ya Kasekwa.

Kidando aliendelea kutoa hoja kuhusu kushindwa kwa upande wa utetezi kuhoji mashahidi wa Jamhuri kwenye masuala muhimu ya kesi hiyo. Alidai kuwa Kamishna Msaidizi wa Polisi (ACP) Ramadhani Kingai hakuhojiwa kuhusu madai ya kuteswa kwa Kasekwa wakati akiwa Moshi, kutishwa wakati akichukuliwa maelezo na kushikiliwa kwake katika vituo mbalimbali vya polisi.

Kwa mujibu wa Kidando, kushindwa huko kuhoji mambo ya msingi yaliyoibuliwa na ushahidi wa Kingai, kumemnyima Kasekwa nafasi ya kuifanya mahakama isiuamini ushahidi wa Jamhuri.

Kidando alidai kwamba ushahidi wa Kasekwa ulikuwa ukijichanganya na kutofautiana, lakini ushahidi huo ulikuwa na mambo yasiyoweza kuthibitishwa.

Alisema, kwa mfano, wakati Kasekwa alidai kuwa aliteswa wakati akisafirishwa kutoka Moshi alikokamatiwa kuja Dar es Salaam, mshitakiwa mwenzake waliokuwa wakisafirishwa pamoja, Mohamed Ling’wenya hakutaja suala kama hilo.

Baada ya hoja hizo za Jamhuri, upande wa utetezi nao ulitoa hoja zao za mwisho za maandishi zilizotayarishwa na wakili John Mallya.

Hoja ya Mallya kuhusu pingamizi la kwanza ni kuwa, kurekodiwa kwa maelezo ya onyo ya Kasekwa Agosti 7, 2020 baada ya kukamatwa Agosti 5, 2020 kulifanyika nje ya muda wa kisheria na kinyume na kifungu cha 50 (1) (a) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai inayotaka maelezo hayo yachukuliwe ndani ya saa nne baada ya kukamatwa kwa mshukiwa.

Kuhusu mwanya unaotolewa na kufungu cha 50 (2) cha Sheria hiyo kuruhusu mpelelezi kuomba kuongeza muda wa kuchukua maelezo endapo kuna sababu za msingi, Mallya alidai kuwa mwaya huo lazima utumike katika mazingira yanayoruhusu.

Alidai kuwa mmoja wa mashahidi wa Jamhuri alikiri kuwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi, kilikuwa na nyenzo zote za kuwezesha Kasekwa kuchukuliwa maelezo, lakini hakuna maelezo yaliyotolewa kwa nini maelezo ya Kasekwa hayakuweza kurekodiwa huko.

Kuhusu mateso aliyodaiwa kupewa Kasekwa ili akiri kosa, Mallya alidai kuwa kuteswa si lazima kuwe kwa kimwili, lakini inaweza kuwa kiakili, ukatili au udhalilishaji huku akirejea Ibara ya 66 (6) (d) na (e) ya Katiba.

Alisema licha ya kutokuwapo kwa ushahidi wa kitabibu kuthibisha mateso dhidi ya Kasekwa, kwa maoni yake kulikuwa na ushahidi unaoungwa mkono na mashahidi watatu wa Jamhuri.

Hivyo aliiomba mahakama kuona kuwa kulikuwa na ushahidi wa kimazingira wa kuteswa kwa Kasekwa kutokana na ucheleweshaji usioelezeka wa kuchukua maelezo yake, kuchelewa kumleta Dar es Salaam, kuficha ukweli kuwa Kasekwka alishikiliwa katika Kituo cha Polisi Tazara, ucheleweshaji usioelezeka wa kumshitaki mahakamani hadi tarehe 19 Agosti, 2020 and kushindwa kwa Lilian Kibona kumpata mume wake (Kasekwa) licha ya juhudi kubwa aliyofanya.

Kwa maoni ya Mallya, mlolongo huo wa ucheleweshaji wa mambo ulimaaanisha kuwa upande wa mashtaka ulishindwa kuthibitisha bila kuacha shaka kuwa maelezo ya onyo ya Kasekwa yalirekodiwa kwa mujibu wa sheria, huku akitaka mahakama iyakatae.

Washtakiwa wengine katika kesi hiyo ni Halfan Bwire Hassan na Mohamed Ling’wenya ambao wanakabiliwa na mashtaka sita, mawili kati yake yakiwa ya kula njama ili kutenda vitendo vya kigaidi yanayowakabili washtakiwia wote wanne.

Mengine ni kufadhili vitendo vya kigaidi (Mbowe peke yake) na la kukutwa na silaha ya kutekeleza vitendo vya kigaidi (Ling’wenya peke yake na lile la kukutwa na sare na vifaa vingine vya JWTZ, kwa Halfani.

Washtakiwa hao wanadaiwa kupanga kutekeleza vitendo vya kigaidi kwa kulipua vituo vya mafuta na sehemu mbalimbali nchini, kwa lengo la kuvuruga amani.

Washtakiwa hao wanadaiwa pia walipanga kumuua aliyekuwa Mkuu wa Wilaya ya Hai, Lengai Ole Sabaya ambaye sasa anatumikia kifungo cha miaka 30 jela kwa kosa la unyang’anyi wa kutumia silaha.

Kesho katika sehemu ya tatu na ya mwisho tutaona jinsi Jaji Mustapha Siyani, alivyochambua hoja za pande zote mbili na kutoa uamuzi

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments