Recent-Post

Wakimbiza Mwenge wa Uhuru wawaondoa hofu vijana

Jumuiya ya Wakimbiza Mwenge wa Uhuru Tanzania (TAUTA) imeitaka jamii kuachana na imani potofu zinazoenezwa na baadhi ya watu wasiolitakia mema Taifa kuwa wakimbiza mwenge kitaifa hupoteza maisha muda mfupi baada ya kuhitimisha mbio hizo.

Wito huo umetolewa leo Oktoba 11 na mzee Chum Abdalla aliyekimbiza mwenge mwaka 1988 wakati akizungumza kwenye maonesho ya wiki ya vijana yanayoendelea katika uwanja wa Mazaina wilayani Chato, mkoani hapa kuelekea kilele cha kuhitimisha mbio za mwenge wa uhuru kitaifa Oktoba 14 mwaka huu.

Amesema vijana wanapaswa kutambua kuwa kitendo cha kukimbiza Mwenge ni cha kizalendo kinachohamasisha maendeleo na kuwaunganisha Watanzania na kusema dhana potofu kuwa wakimbiza mwenge wanakufa muda mfupi baada ya kukabidhi mwenge sio ya kweli.

Mimi nimekimbiza mwenge wa uhuru toka mwaka 1988 nipo na nina afya njema mkimbiza mwenge akifariki amefariki kwa maradhi kama watu wengine na sio sababu ya kukimbiza Mwenge wa uhuru,” amesema Abdalla.

Awali akikagua mabanda kwenye maonyesho hayo, Waziri ofisi ya Waziri Mkuu, Sera na Uratibu wa Bunge, Jenista Mhagama amesema jamii haina budi kuwapuuza wale wanaoeza uvumi huo na kuachana na dhana hiyo.

Amesema matunda ya Mwenge wa Uhuru ni pamoja na kusaidia  kuwabaini Viongozi  wanaojihusisha na rushwa, ufisadi na  kuimarisha maadili na uzalendo katika Taifa.

Akizungumzia wiki ya vijana iliyoanza Oktoba 8, Waziri Mhagama amesema maonesho hayo yamewakutanisha vijana kutoka mikoa mbalimbali nchini lengo likiwa kuwakumbusha wajibu wao katika Taifa na yanatarajiwa kuzinduliwa Oktoba 12 na Waziri Mkuu Kassim Majaliwa.

Post a Comment

0 Comments