Recent-Post

WANAWAKE CHACHU YA MAENDELEO - MAMA ZAINAB

 Mke wa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar,  Mama Zainab Kombo Shaib, ametoa wito kwa wanawake nchini kushikamana ili kuweza kujikomboa kutokana na ukubwa wa wimbi la changamoto zinazowakabili


Mama Zainab ametoa wito huo leo, Konde Mkoa wa Kaskazini Pemba, akiongea na akinamama wa ACT-Wazalendo wa Mikoa miwili kichama, ya Wete na Micheweni kisiwani humo.

Amesema ukombozi wa mwanamke ni sawa na ukombozi wa jamii yote na njia ya matumaini kuelekea maendeleo ya Taifa zima

Amefahamisha kuwa matumaini na mafanikio ya ukombozi wa kweli wa mwanamke hayawezi kufikiwa pindipo akinamama wenyewe watashindwa kujitambua, kushikamana na kusaidiana.

"Wanawake ni wengi, na  nguvu yetu ni kubwa sana, tukiungana,tukishirikiana pamoja tukaacha makundi na kuchukiana tutafika mbali na tutalisaidia taifa katika kufikia ukombozi" alieleza Mama Zainab.

Mama Zainab amewataka wanachama hao kuendeleza uwajibikaji katika shughuli za chama ili kuisimamisha dhamira ya Uzalendo.

Aidha Mama Zainab amesema amejitolea kwa kushirikiana na wadau mbali mbali kuwasaidia watoto yatima na wenye mahitaji maalum, kwani kufanya hivyo ni wajibu wa kila mwanajamii sambamba na kuwataka wazazi kutokuwaficha watoto wenye ulemavu kwani nao wanahaki ya kuishi nakupata huduma za kijamii kama wengine.

Katika kikao hicho wanawake 50 wamechukua kadi kwa niaba ya wenzao 350 na kujiunga rasmi na chama hicho, sambamba na kurejesha kadi 20 za Chama cha CUF.

Mama Zainab amewasihi wanawake hao kuendelea kuiunga mkono serikali ya umoja wa kitaifa na kuwaahidi kwamba Makamu wa kwanza wa Rais, kwa kushirikiana na serikali wapo katika mipango madhubuti ya kuitafuta haki ya wahanga wa uchaguzi mkuu wa mwaka 2020.

Bi. Awena Sinani Masoud, mke wa aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais, Marehemu Maalim Seif  Sharif Hamad, amesema binafsi anamuunga mkono Mhe.Othman Masoud, Makamu wa Kwanza wa Rais Zanzibar, na kusema anamatumaini makubwa kwamba ataifikisha Zanzibar katika hadhi yake.

"Uwezo mkubwa  alionao Mhe. Othman unanipa faraja sana kwamba anaweza kuendeleza hatua alipofika Maalim Seif" alieleza

Aidha amewaasa wanachama wa ACT jimbo la Konde kuingia katika uchaguzi wa marudio unatarajiwa kufanyika tarehe 9Oktoba, kwa njia za amani na ustaarabu, sambamba na kuwaonesha umuhimu wa kushinda uchaguzi huo.

Akitoa salamu za Wanawake wa chama hicho wa kisiwani Pemba mratibu wa wanawake Bi.Mkunga Hamad Sadala amesema, wanawake wa kisiwa cha Pemba wataendelea kumpa ushirikiano Makamu wa Kwanza wa Rais ambayepia ni Mjumbe wa kamati kuu ya Chama hicho.

Baada ya kikao hicho Mama zainab alipata fursa ya kukutana na watoto yatima na wenye mahitaji maalum wa Shehia ya Kinyasini na Mtemani za Wilaya wa Wete mkoa wa Kaskazini Pemba.

Post a Comment

0 Comments