Wizara ya Kilimo: Serikali haijazuia uuzaji mazao nje ya nchi

 SERIKALI imesema haijazuia mfanyabiashara yeyote kuuza mazao yake nje ya nchi, na kwamba mkulima wa nchi hii wajibu wake ni kulima , kuvuna ,kuhifadhi na kuuza kwa kuwa hiyo ndio biashara yake.


Akizungumza katika ziara ya kikazi wilayani Mpanda mkoani Katavi baada ya kukagua ,kituo cha kununulia mahindi cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA), Naibu Waziri wa Kilimo Hussein Bashe amesema Serikali haijazuia uuzaji wa mazao  nje ya nchi.

"Hivyo kama yupo ambaye amazuiwa kuuza mazao yake nje ya nchi  Wizara hiyo inamkaribisha na watampa ushirikiano kwani vibali vyote vya kusafirisha mazao nje ya nchi wanatoa vibali bure  ili mradi awe leseni ya kufanya biashara hiyo.

"Serikali imeanza utaratibu wa kujenga na kukodi maghala katika nchi ambazo zina masoko ya mazao kama vile Sudan Kusini, DRC Congo, Kenya, tunaenda kuweka maghala katika nchi hizo ili Bodi yetu ya  Mazao Mchanganyiko (CPB) na Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA)  waweke mazao hayo kwenye maghala hayo na kuyauza,"amesema.

Ameongeza wataruhusu wafanyabiashara wa Tanzania waweze  kuuza mahindi yao kupitia maghala hayo ili kurahisisha biashara yao.
Kuhusu maombi ya  Mkuu wa Mkoa wa Katavi Mwanamvua Mrindoko aliyeomba kituo cha Mpanda kuongezwa tani zingine 10,000 kwa ajili ya wakulima kuuza mahindi yao amesema kwa sasa Wizara inapitia vituo vyote ili kujiridhisha na kujua mahitaji kamili ya vituo hivyo.

Amefafanua  kwa sababu unaweza kuruhusu wanunue tani hizo kumbe mahindi yenyewe hayapo.“Napita katika kila kituo kujiridhisha na tutafanya ukaguzi huo mpaka Oktoba 15,  2021 ili tukifanya maamuzi tujue kila mkoa utapata mgao wa kiasi gani tutakapowaruhusu kununua mahindi hayo kulingana na kiasi tutakachowaongezea."

Bashe ameongeza Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Samia Suluhu Hassan  amejipambanua kuwalinda wakulima wa Tanzania na wanafahamu bei ya pembejeo imepanda katika soko la dunia hivyo  njia pekee ya  kumlinda mkulima ni kumpa ruzuku ya mbolea au kununua mahindi yake na hiyo ndiyo sababu Serikali inanunua mahindi ili kulinda wakulima wetu.

Ameongeza mazao mengi ya wakulima  yanaathiriwa na uhifadhi hii ni sehemu muhimu sana ndiyo maana serikali inajenga maghala  mengi mpaka vijijini ili kuwasaidia wakulima namna ya kuhifadhi mazao kwa ubora lakini pia imekuwa ikitoa elimu sana kwa wakulima namna ya kuhifadhi mazao yao.

“Lakini Serikali inagawa mbegu za kisasa kupitia Taasisi ya Uzalishaji wa mbegu bora ya (ASA) kwa wakulima na imepunguza gharama za mifuko ya kuhifadhia mahindi inayozalishwa na A to Z na kupunguza hasara zinazotokana baada ya kuvuna mazao ambapo mkulima akiingiza mahindi katika mchakato wa kusafisha anapunguza kilo moja kwa kila kilo 100 kwa sababu mahindi yanakuwa na mchanga, mabunzi pamoja na vumbi.

 Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akiangalia ubora wa mahindi katika moja ya maghala ya kuhifadhia mahindi katika kituo cha Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Mpanda mkoani Katavi wakati alipokagua zoezi la ununuzi wa mahindi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo kulia ni Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bw. Milton Lupa  na Katikati ni Marwa Range Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Sumbawanga.




Naibu Waziri wa Kilimo Mhe. Hussein Bashe akijadiliana jambo na Afisa Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Taifa wa Hifadhi ya Chakula (NFRA) Bw. Milton Lupa  wakati alipotembelea katika kituo (NFRA) Mpanda mkoani Katavi na kukagua zoezi la ununuzi wa mahindi akiwa katika ziara ya kikazi mkoani humo kulia ni na Katikati ni Marwa Range Kaimu Meneja wa NFRA Kanda ya Sumbawanga na kulia ni Beatus Malema Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Maendeleo ya Mazao Wizara ya Kilimo.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments