CHONGOLO AELEZA MKAKATI WA KUTATUA CHANGAMOTO YA MBOLEA NCHINI, ASISITIZA KIDATO CHA KWANZA KUJIUNGA KWA PAMOJA

 Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amesisitiza kuwa elimu  bila malipo itaendelea na kwamba wale wote watakaofaulu  kwenda shule za sekondari watajiunga wote kwa pamoja na hakutakuwepo na chaguo la kwanza wala la pili.

Katibu Mkuu huyo amesema kuwa wanafunzi hao wote watajiunga kwa pamoja kwa sababu madarasa yote yanayopaswa kupokea wanfunzi tayari  Mhe. Rais Samia Suluhu Hasaani ameshatoa fedha hizo.

Ndg. Chongolo amesema hayo leo tarehe 20 Novemba, 2021 wakati akihutubia wananchi, viongozi wa chama na serikali ngazi za wilaya na mkoa, katika mkutano wa mapokezi kata ya Pongwe wilaya ya Tanganyika mkoa wa Katavi ambapo Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa imeingia leo katika Mkoani huo kwa ziara ya siku mbili kukagua utekelezaji wa ilani ya CCM na kuhimiza uhai wa chama ngazi ya mashina.

Aidha Katibu Mkuu amefafanua, sababu za mbolea kupanda ikiwa ni kilio cha wakulima hasa katika mikoa inayozalisha mazao ya kilimo kwa wingi  ambapo ameeleza sababu ya korona kuwa ndio chanzo kikuu cha gharama hiyo kupanda.

"Wote mnajua kuna kitu kinaitwa korona, ugonjwa huu umetokea huko kwa wenzetu China na mataifa mengine makubwa, ambapo ulipoanzia ndipo walipo wazalishaji wakubwa wa mbolea na ililazimisha watu hao wajifungie ndani, ingawa huku kwetu tuliendelea na shughuli wakati wenzetu walikuwa wamejifungia na hakukuwa na mtu aliyekuwa anazalisha. Matokea yake tukatumia mbolea yote iliyokuwa kwenye akiba, na mashamba yao walipofungua wakaitumia yote na kusababisha uhaba mkubwa na bei kupanda." Katibu Mkuu amefafanua

Hata hivyo katika jitihada za kuhakikisha changamoto hiyo haijirudii tena serikali ya Chama Cha Mapinduzi imeweka mkakati wa kujenga kiwanda cha ndani cha kuzalisha mbolea.

"Serikali imeweka mpango kwa kuingia makubaliano wa ujenzi wa kiwanda kikubwa cha mbolea kinajengwa Dodoma ili changamoto hii isijirudie tena na inawezekana mbolea ya kukuzia tukaipata hapa hapa kwetu." Katibu Mkuu Ndg. Chongolo amefafanua

"Hili tatizo halijaletwa na mwanadamu ama kiongozi yeyote, ni changamoto iliyoletwa kutokana na majanga ya Dunia na sasa tumeshajifunza," amesisitiza Katibu Mkuu.

Katibu Mkuu wa CCM Ndugu Daniel Chongolo akihutubia wakazi wa Luhafwe, Kata ya Tongwe Wiayani Tanganyika mkoa wa Katavi ikiwa sehemu ya ziara yake ya siku 2 pamoja na Wajumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Taifa. (Picha na CCM Makao Makuu)  



TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments