DC IRAMBA AFANIKISHA ASKARI 85 WA JESHI LA AKIBA KUPATA AJIRA SUMA JKT

MKUU wa wilaya ya Iramba mkoani Singida, Mheshimiwa Suleiman Yusuph Mwenda amefanikisha askari 85 wa Jeshi la akiba waliohitimu mafunzo yao kupata ajira SUMA JKT.


Mheshimiwa Mwenda ameeleza hayo wakati akifunga mafunzo ya askari wa Jeshi la Akiba katika viwanja vya Shule ya Msingi Kata ya Ulemo wilayani hapa.
“Vijana hawa ni jeshi kamili, leo hii tukipata uvamizi wa aina yoyote katika wilaya yetu ya Iramba ninajivunia kwamba ninacho kikosi kamili cha kukituma kwenda kumsambaratisha adui na adui akasambaratika

“Vijana hawa ni hazina kwa Taifa kwa sababu wamejaa uzalendo, ukomavu , ujasiri, uhodari na utaifa katika mioyo yao ya kulilinda na kulitetea Taifa lao,”amesema.

Hakika vijana hawa ni rasilimali na mtaji mkubwa kwa nchi ya Tanzania. Niwaambie ndugu zangu kwa kutambua umuhimu wa vijana hawa sikutaka wapotee tena kurudi mitaani, nimeshirikiana na msimamizi wa Jeshi la Akiba kuhakikisha vijana hawa wanapata ajira, hivi ninavyoongea vijana hawa 85 wamepata ajira katika Shirika la SUMAJKT,"amesema Mkuu huyo.
Amesema, kupata ajira kwa askari hao kumetoa fundisho kwa vijana na wazazi kuhimiza vijana wao kujiunga na mafunzo ya Jeshi la akiba pale mafunzo yanapokuwa
yameitishwa kwa sababu mafunzo hayo ni sehemu ya kuwaandaa vijana kupata ajira na kuwa raia bora wa Taifa la Tanzania.

Katika hatua nyingine DC Mwenda amempongeza Diwani wa Kata ya Ulemo wilayani hapo, Mheshimiwa John Peter ambaye ameshiriki na kuhitimu mafunzo hayo.

“Kwa kweli ni vijana wachache ambao ni viongozi wanatambua umuhimu wa mafunzo haya ambayo yanamfanya mtu anakuwa kiongozi mahiri, mwenye nidhamu na alioshiba utaifa,"aliongeza na kufafanua kuwa, kufuatia Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan kuipatia Wilaya ya Iramba takribani 1.3 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa madarasa 47 na mengine ya shule shikizi.

“Vijana hawa wameshiriki ujenzi wa kuchimba msingi ya madarasa 15 na kufanikwa kuokoa takribani 900,000,"amesema hivyo kutoa wito kwa wananchi kujifunza kwa vijana hao kujitolea kuchimba misingi, kupeleka mchanga na kupeleka mawe ili kuhakikisha madarasa yanajengwa kwa kiwango bora na yanakamilika kwa wakati.
Akitoa taarifa fupi ya askari hao mbele ya Mkuu huyo wa wilaya, Kapteni Eusebius Mtesigwa amesema kuwa vijana hao wako tayari wakati wote kulilinda na kulitumikia Taifa.

Kapteni Mtesigwa alifafanua kuwa askari (wanafunzi) hao wanaohitimu wako 132 ambapo askari wa kike 14, askari wa kiume 118 huku askari wawili hawajahitimu baada ya kukosa vigezo.

Askari hao wamefundishwa mafunzo ya kijeshi, mafunzo ya TAKUKURU, mafunzo ya Zimamoto,mafunzo ya usalama wa raia, mafunzo ya uhamiaji, mafunzo ya huduma ya kwanza, mafunzo ya usomaji wa ramani, mafunzo ya ujanja wa porini na mafunzo
kutoka TFS.

“Niwaombe askari mnaohitimu mafunzo kuzingatia kiapo chenu cha utii katika utendaji wenu wa kazi hasa utii, uaminifu na uhodari ili kuwa mabalozi wazuri wa jeshi la akiba na usalama,”amesema Mtesigwa.

Awali akisoma risala ya wahitimu hao, MGM Betha Japhect amemshukuru Mkuu huyo wa wilaya kwa kuwahakikishia kupata ajira hivyo wamemuahidi kuwa watiifu, waaminifu na waadilifu kwa Taifa lao.

“Tutakuwa waadilifu, wazalendo na kufanya kazi kwa kushirikiana na kujiepusha na maadili yasiokuwa ya Mtanzania,"aliahidi.
Kwa upande wake Diwani wa kata hiyo ambaye ni mhitimu wa mafunzo hayo, Mheshimiwa John Peter amesema kuwa mafunzo hayo yameleta hamasa kubwa kwa vijana hasa baada ya zawadi mbalimbali alizozitoa Mkuu huyo wa Wilaya pamoja na ajira ya askari waliohitimu.

Mmoja wa wazazi wa wahitimu hao, Matha Peter amesema kuwa wako tayari kuwahimiza watoto wao kushiriki mafunzo ya Jeshi la Akiba kwa sababu wanapata ajira na kuwa raia wema.

“Kwa kweli tumefurahiswa sana kwa watoto wetu kupata ajira kwani tumepunguza wazururaji mitaani, pongezi ziende kwa Mkuu wa Wilaya kwa kuungana na SUMAJKT kuwapatia vijana wetu ajira,"amesema.

NA MWANDISHI DIRAMAKINI

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments