KAMPUNI YA DUBAI YAVUTIWA NA MAZINGIRA YA UWEKEZAJI SEKTA YA MADINI TANZANIA

    


************************ 

Asteria Muhozya na Abubakari Kafumba - UAE 

Kampuni ya Frontiers Gold and Gems ya Dubai imeridhishwa na Mazingira rafiki ya Uwekezaji yaliyopo kwenye Sekta ya Madini nchini baada ya kukutana na wawakilishiwa wa Tanzania wanaoshiriki Maonesho ya Dunia ya Expo 2020 Dubai, ambao wameihakikishia kampuni hiyo uhakika wa kufanya biashara kwa usalama. 

Wawakilishi wa Wizara ya Madini wakiongozwa na Kamishna Jenerali wa Banda la Tanzania katika Maonesho hayo Balozi Mohamed Abdallah Mtonga wameieleza kampuni hiyo kuhusu namna Serikali inavyoshiriki moja kwa moja kuhakikisha wawekezaji wanafanya shughuli zao kwa usalama na faida. 

Kikao baina ya Tanzania na Kampuni ya Frontiers Gold and Gems ya Dubai kilichofanyika Novemba 10 ni mwendelezo wa kikao kilichofanyika Novemba 9 ambapo Afisa Mawasiliano wa Kampuni hiyo aliomba nafasi ya Wizara ya Madini kukutana na Rais wa kampuni hiyo ili kupatiwa maelezo na ufafanuzi zaidi wa uwekezji kwenye sekta ya madini. 

Lengo kuu la kampuni hiyo kukutana na Serikali kupitia Wizara ya Madini ni kueleza nia yao ya kufanya biashara ya ununuzi wa madini ya dhahabu kutoka Tanzania au kupata wafanyabiashara watakaoshirikiana, pamoja na kupata madini ya Nano Copper yanayotumika kupunguza maambukizi yanayotokana na bakteria. 

Katika hatua nyingine, kampuni hiyo imevutiwa kushirikiana na Shirika la Madini la Taifa (STAMICO) katika miradi inayosimamiwa na taasisi hiyo ikiwemo ya uchimbaji wa copper, dhahabu na makaa ya mawe Iliyopo katika mikoa ya Kilimanjaro, Geita na Songwe. Baada ya kufahamishwa fursa kupitia STAMICO, mazungumzo zaidi yanatarajiwa kufanyika. 

Hatua hiyo inafuatia kupatiwa taarifa sahihi ambapo imeonesha nia ya wazi ya kufanya kazi na biashara nchini Tanzania baada ya kufahamishwa na kupata maelezo ya kina kuhusu namna na taratibu za kushirikiana na Tanzania katika uwekezaji kwenye Sekta ya Madini. 

Akizungumza katika kikao hicho, Mtendaji Mkuu wa Taasisi ya Jiolojia na Utafiti wa Madini Tanzania (GST) Dkt. Mussa Budeba amemweleza Rais wa kampuni hiyo Thaeer Safa kuhusu wingi wa madini ya aina mbalimbali yaliyopo nchini hususani madini ya vito, viwandani na madini mengine mengi pamoja fursa za kibisahara zilizopo katika Sekta ya Madini ikiwemo utafiti wa madini hayo. 

‘’Nitafurahi sana ikiwa utafikiria katika hili pia, kwa sababu eneo la utafiti ni moja ya maeneo muhimu ambayo yanahitaji kuendelezwa ili kuvumbua madini mbalimbali yanayohitajika. Ukiwa tayari kufanya kazi na GST taarifa za jiosayansi zipo GST na usiwe na hofu kuhusu udangayifu, na endapo uko tayari kufanya kazi na Sekta yetu unao uchaguzi wa biashara gani ufanye na sisi,’’amesisitiza Dkt. Budeba. 

Kwa upande wake, Mkurugenzi wa Ukaguzi na Biashara ya Madini kutoka Tume ya Madini Bw. Venance Kasiki amesisitiza kuhusu usalama wa kufanya biashara ya madini nchini na kueleza kuwa, serikali haitokubali wawekezaji kudanganywa kutoka kwa watu wasio waaminifu ambao wanashirikiana na wawekezaji na kwamba nafasi hiyo haipo. 

Amemweleza kuhusu uwepo wa Masoko ya Madini yaliyoanzishwa katika mikoa mbalimbali nchini na kusisitiza kwamba, biashara inayofanyika katika masoko hayo ni ya uwazi na Serikali imethibiti biashara ya madini isiyo rasmi. 

Aidha, ameieleza kampuni hiyo kuwa inao uchaguzi wa namna ya kufanya biashara ya madini ikiwemo kuchimba yenyewe, kununua ama kushirikiana na taasisi ya Serikali au wadau wengine.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments