Recent-Post

KAZI YA SIASA SIO UONGO, SIO MAJUNGU SIO VITINA WALA SIO UMBEA

Katibu Mkuu wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Ndg. Daniel Chongolo amekemea tabia ya baadhi ya viongozi wa kisiasa kuendekeza uongo, fitina, majungu, umbea na kusingiziana ambapo amewakumbusha kuwa, kazi ya siasa ni kusemeana mema, kupendana, kushikamana na kuneneana mema.

Katibu Mkuu ameyasema hayo katika muendelezo wa ziara yake na Sekretarieti ya Halmashauri Kuu ya CCM Taifa mkoa wa Kagera akiwa wilayani Muleba tarehe 14 Novemba, 2021 katika kikao cha shina namba 05 tawi la Lulanda.


Katibu Mkuu amekemea kwa kueleza kuwa, "Kazi ya siasa sio uongo, kazi ya siasa sio majungu, sio fitina, sio umbea wala sio kusingiziana, Kazi ya siasa ni kuombeana mema, kazi ya siasa ni kupendana, kushikamana, kazi ya siasa ni kuneneana mema wenzio."

Kauli hiyo ya Katibu Mkuu imekuja baada ya kupokea taarifa ya viongozi mbalimbali wa wilaya hiyo walionza kusemana vibaya na kujengeana fitina ikiwa ni maandalizi kuelekea Uchaguzi Mkuu wa ndani ya Chama mapema mwakani.

Katika hatua nyingine, Katibu Mkuu amezitaka serikali za mikoa na wilaya zinazopakana na ziwa victoria kuendeleza jitihada za kupambana na uvuvi haramu katika ziwa hilo.

Katibu Mkuu amesema, madhara ya uvuvi haramu katika ziwa hilo ni makubwa na kwamba serikali ikiacha kudhibiti matendo hayo, uvuvi haramu utaendelea kutengeneza mazingira magumu kwa mikoa hiyo na wananchi kunufaika na uchumi unaotokana na ziwa hilo.

“Ziwa Victoria ni uchumi mzuri ambao ukilelewa vizuri kwa kufuata uvuvi unaofuta sheria na taratibu, utasaidia kudumu kwa uchumi ambao unatokana na ziwa hilo miaka na miaka,” amesema.

Aidha, wananchi, Madiwani na Wabunge wa Muleba, kwa nyakati tofauti katika ziara hiyo, wameendelea kutoa shukrani kwa Mhe. Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuwajali kwa kuwapelekea fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo ikiwa ni pamoja na ujenzi wa madarasa yote ya sekondari wilaya ya Muleba na ujenzi wa vituo vya Afya unaoendelea.
                     www.bandolamedia.co.tz

Post a Comment

0 Comments