Kikwete akemea uzembe vifo vya mama na mtoto

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete akizungumza wakati akizindua mdahalo uliozungumzia huduma bora za afya ya mama na mtoto na nini kifanyike katika mkutano wa mwaka wa kisayansi wa huduma za afya ya uzazi. Picha na Sunday George

Rais wa Awamu ya Nne, Jakaya Kikwete amesema kumekuwa na uzembe wa makusudi ambao unaendelea katika vituo vya afya vya umma na binafsi wakati wa utoaji huduma kwa wajawazito jukumu alilotaja la wote kukemea.

Amesema changamoto ya vifo vya mama na mtoto ni kubwa nchini, ijapokuwa mengi yamefanywa bado hatujafanikiwa kuvipunguza hivyo nguvu inahitajika.

Kikwete ameyasema hayo leo Alhamisi, Novemba 18, 2021 wakati akifungua mdahalo kwenye mkutano wa mwaka wa kisayansi wa huduma za afya ya uzazi, mtoto, vijana na lishe wenye lengo la kuongeza kasi ya kupunguza vifo vitokanavyo na uzazi, watoto wachanga, watoto chini ya miaka mitano na vijana.

“Kumekuwa na uzembe wa makusudi ambao unaendelea katika vituo vya afya, kuna hospitali moja binafsi mama ambaye ni mkunga alienda kumwangalia mwanaye akakuta amejifungua lakini anavuja damu wanabadilisha tu shuka. Kwa kuwa anafahamu ikabidi asaidie pale kudhibiti damu isiendelee,” amesema.

Ametoa wito kwa ngazi za familia, watoa huduma ngazi ya jamii (CHWs), mashirika na asasi za kiraia, balozi, nchi wahisani na Serikali kuungana pamoja kuhakikisha vifo hivyo vinatokomezwa.

“Tunahitaji wote tuungane pamoja kuhakikisha tunatokomeza vifo hivyo, ninaamini Serikali kupitia Wizara ya Afya, Tamisemi zitashirikiana nanyi.

“Kasi mbele yetu bado ni kubwa hata kwa viwango vya kimataifa, tumebakiza miaka kama 9 pekee tunatakiwa kufikia vifo 70 katika vizazi hai 100,000 ifikapo mwaka 2030 ni kazi kila mmoja kichwani mwake aseme tunafanyaje? kuanzia wataalamu, wakunga, wadau na Serikali,” amesema Kikwete.

Kikwete ameipongeza Serikali kuzindua ajenda ya Uzazi wa Mpango (FP2030) ambao unaelekeza nini kinatakiwa kufanywa na namna ya kukifanya.

“Sekta mbalimbali tuungane pamoja kuhakikisha tunaokoa maisha ya mama na mtoto kwa kutumia utaalamu, teknolojia na kuwezesha miundombinu,” amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments