Recent-Post

Kocha apigwa risasi na mashabiki 'waliopagawa' uwanjani

Kocha wa Klabu ya Ferro de Gerenal Pico ya nchini Argentina, Mauricio Romero amepigwa risasi wakati mchezo unaendelea katika Ligi ya Argentina kwenye mchezo wa Ligi Daraja la Tatu uliopigwa usiku wa Oktoba 31, 2021.


Mtanange huo wa Kundi A kati ya Ferro de Gerenal Pico na Huracan Las Heras ulipigwa katika dimba la Estadio General San Martín lililopo Jimbo la Mendoza nchini Argentina.
Kocha Romero alijeruhiwa katika bega lake kama inavyoonekana katika picha. (Picha na Mariano Javier Pepa-Twitter)

Ukanda wa video ulioonwa na DIRAMAKINI BLOG unaonyesha kuwa, wachezaji baada ya kusikia mlio wa risasi walienda kumzingira kocha huyo kufuatia mashabiki wa Huracan Las Heras kusababisha vurugu na kupigana wenyewe kwa wenyewe wakati kikosi chao kikicheza na Ferro de General Pico.

Gazeti la michezo la Ole limeripoti kuwa kocha wa Ferro, Mauricio Romero alipata jeraha la risasi begani huku makundi ya mashabiki waliopangawa waliohusishwa na Huracan wakipigana wenyewe kwa wenyewe.
Video ilionyesha Romero akitibiwa jeraha kwenye bega lake, na klabu hiyo baadaye ikasema amekwenda hospitali.

"Romero anaendelea vizuri na yuko salama," Ferro imetweet. "Baada ya kutoka uwanjani alifanyiwa vipimo katika hospitali ya karibu na alitoa taarifa kwa polisi.

Huracan ilisema mapigano hayo yanaiharibia klabu hiyo. "Kwa miaka mingi familia zimekuwa zikifukuzwa uwanjani," klabu hiyo ilisema kupitia taarifa yake Facebook.

"Tunaomba wale wote wanaohujumu klabu wakae pembeni ili mashabiki wa kweli warudi,"iliongeza ambapo mechi hiyo ilisitishwa mwishoni mwa kipindi cha pili huku Huracan wakiwa mbele kwa mabao 3-1.

Post a Comment

0 Comments