Kocha mpya Simba kuanza na wanne

 

ALHAMISI wakati Taifa Stars ikikiwasha na DR Congo ya Djuma Shabaan kuwania kufuzu Kombe la Dunia, Kocha mpya wa Simba, Pablo Franco Martín aliyetangazwan jana atakuwa jukwaa kuu akiangalia viwango vya wachezaji wake wanne watakaoanza.

Hao ni Aishi Manula, Shomari Kapombe, Tshabalala na Muzamiru. Israel Mwenda, Boko, Kennedy Juma hawa wana nafasi kubwa ya kuanzia benchi lakini vilevile atamshuhudia kwa mara ya kwanza beki kiraka wa Yanga, Djuma Shabaan.

Simba jana ilimtangaza Franco raia wa Hispania ambaye ampitia katika klabu kubwa mbalimbali kama Real Madrid, Getafe kuwa kocha mkuu akichukua nafasi ya Didier Gomes.

Kocha Msaidizi wa Simba, Hitimana Thiery alibainisha kwamba jana  Jumamosi wangeanza programu rasmi ya mazoezi na wachezaji waliopo baada ya wengine wa timu hiyo kuwa kwenye timu zao za taifa, mazoezi ambayo anaamini yatatoa mwanga kwao.

Aidha amebainisha mikakati yake kipindi hiki ambacho Simba inapambana kuwa kwenye kiwango bora zaidi msimu huu ambapo imecheza mechi tano na kushinda tatu, kupata sare mbili ikikamata nafasi ya pili kwenye msimamo.

Alisema kikosi cha Simba leo kitaendelea na mazoezi baada ya mapumziko mafupi waliyokuwa wamepewa wachezaji ili kujiandaa na mechi za kuanzia raundi ya sita ya Ligi itakayoendelea baadae mwezi huu. baada ya kusimama kwa siku kadhaa kupisha mechi za kimataifa za Fifa.

Kocha Hitimana ameliambia Mwanaspoti kuwa mazoezi ya leo yatakuwa ni ya kawaida na ndiyo yatampa taswira ya programu yake kipindi hiki.

“Baada ya mazoezi ya kwanza hapo ndipo tutapata mwanga kama tuweke kambi nje ya Dar es Salaam au vinginevyo kulingana na idadi ya wachezaji nitakaokuwa nao mazoezini,” alisema Kocha huyo aliyekaa kikao wiki hii na Ibrahim Ajibu na Jonas Mkude na kuwarejesha kwenye ubora wao mpya ndani na nje ya Uwanja.

Alisema baada ya programu ya kesho watashauriana na uongozi ili nao waone cha kufanya kutokana na idadi ya wachezaji wao wengi kuwa kwenye timu zao za taifa.

Ingawa Mwenyekiti wa klabu hiyo, Murtaza Mangungu amedokeza kwamba benchi la ufundi ndilo litaamua kuhusu kambi yao iweje na ifanyike wapi kipindi hiki ambacho ligi imesimama.

Kwa mujibu wa Mangungu, Simba imekuwa ikijifua kwenye viwanja tofauti kwa wiki kadhaa sasa kufuatia uwanja wao wa Bunju kuwa kwenye matengenezo madogo.

“Benchi la ufundi ndilo litaamua kama kipindi hiki waendelee kubaki Dar es Salaam au vinginevyo,” alisema Mangungu jana.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments