MBUNGE KUNAMBI AKABIDHI MILIONI 918 MIKOPO YA ASILIMIA 10 KWA WANAWAKE, VIJANA NA WENYE ULEMAVU

MBUNGE wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi amekabidhi hundi yenye thamani ya Sh Milioni 918 kwa vikundi 100 vya Wanawake, Vijana na Watu wenye Ulemavu pamoja na kukabidhi Pikipiki 20 zenye thamani ya Sh Milioni 50 kwa vikundi viwili vya vijana ikiwa ni sehemu ya mkopo uliotolewa kwa vikundi.


Akizungumza wakati wa kukabidhi hundi hiyo na pikipiki hizo, Mbunge Kunambi amewataka Wanawake, Vijana na wenye Ulemavu kuchangamkia fursa ya mikopo hiyo isiyo na riba inayotokana na asilimia 10 ya makusanyo ya ndani ya Halmashauri.

Kunambi amesema kupitia mikopo hiyo wananchi wengi wataweza kuimarisha vipato vyao na kuchochea maendeleo jambo ambalo limepelekea Halmashauri hiyo ya Mlimba kuongoza kwa makusanyo ya mapato kwenye robo ya kwanza katika Mkoa wa Morogoro ikiwa ni mara ya kwanza tangu kuanzishwa kwa Halmashauri hiyo sambamba na kushika nafasi ya saba Kitaifa.

" Niipongeze sana Halmashauri yetu inayoongozwa na Mkurugenzi wetu Mhandisi Kaliwa ambapo kwa pamoja akishirikiana na sisi Madiwani tumeweza kutenga Sh Milioni 275 na kukusanya Sh Milioni 643 ikiwa ni fedha za marejesho ya mkopo wa miaka ya nyuma na jumla yake ndio unapata Sh Milioni 918 ambazo leo tunazikabidhi kwa wananchi wa Mlimba.

Niwapongeze wananchi wangu wa Mlimba kwa kuwa waaminifu na kurudisha kwa wakati mnapochukua mikopo hii kwani inasaidia kuwezesha vikundi vingine navyo kupata, kupitia mikopo tunaenda kufungua uchumi wa Mlimba na kuimarisha maisha ya wananchi wetu, kwetu ni Historia kubwa kukabidhi hundi yenye thamani hii katika Halmashauri yetu, haijawahi kutokea," Amesema Mbunge Kunambi.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Mhandisi Stephano Kaliwa amesema kuwa Halmashauri hiyo imekua ikitenga kila mwaka asilimia hiyo na kuipeleka kwa walengwa kama mkopo ili kuinua hali zao za kiuchumi na kijamii.

" Pamoja na upelekaji wa mikopo hii Halmashauri itahakikisha kuwa fedha hizo zinarejeshwa kwa wakati kulingana na makubaliano ya mkataba," Amesema Mhandisi Kaliwa.

Mkopo huo wa Sh Milioni 918 umetolewa kwa vikundi 69 vya Wanawake vyenye mkopo wa Sh Milioni 570.5, vikundi 29 vya vijana vyenye mkopo wa Sh Milioni 339.5na vikundi viwili vya walemavu vyenye mkopo wa Sh Milioni Nane.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi (wa Tatu kutoka kushoto) akiwa katika Picha ya Pamoja na Mkurugenzi wa Halmashauri ya Mlimba, Stephano Kaliwa ( wa nne kutoka kushoto) na kikundi Cha vijana kilichopatiwa mkopo wa Pikipiki zenye thamani ya Sh Milioni 50.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi akizungumza na wananchi wa Tarafa ya Mngeta wakati alipofika kukabidhi hundi ya Sh Milioni 918 kwa vikundi 100.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi akiwasha Pikipiki ikiwa ni ishara ya kuwapatia vijana wanaounda vikundi viwili ambao wamepatiwa mkopo wa Pikipiki 20 zenye thamani ya Sh Milioni 50.
Mbunge wa Jimbo la Mlimba Mkoani Morogoro, Godwin Kunambi ( mwenye Suti nyeusi) akikabidhi hundi ya Sh Milioni 918 kwa vikundi 100 vilivyopatiwa mikopo na Halmashauri ya Mlimba.
Wananchi wa Tarafa ya Mngeta, Mlimba wakifuatilia mkutano wa Mbunge wa Jimbo la Mlimba, Godwin Kunambi.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments