Mshitakiwa kesi ya kina Mbowe aeleza alivyoteswa

Dar es Salaam. Mshtakiwa wa tatu katika kesi ndogo ndani ya kesi ya ugaidi inayomkabili Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe na wenzake watatu ameieleza mahakama jinsi alivyokamatwa akiwa mkoani Kilimanjaro kuteswa kisha kusafirishwa hadi Dar es Salaam.

Mohamed Abdillahi Ling’wenya ameiambia mahakama leo Alhamisi Novemba 25, 2021 kuwa baada ya kukamatwa alipelekwa Kituo Kikuu cha Polisi Moshi ambapo alifungwa pingu na kupitishiwa bomba katikati ya miguu hali iliyomfanya awe kichwa chini miguu juu.

Soma hapa ushahidi wake

Wakili Matata anaanza kumuongoza kutoa ushahidi wa utetezi wake anasema: “Naitwa Mohamed Abdillahi Ling'wenya, naishi Kimara King'ong'o. Nilikuwa Askari wa Jeshi la Wananchi. Niliacha mwaka 2017”

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya kuacha kazi nikawa naishi Shinyanga. Baada ya Shinyanga nikapata kazi Mtwara

Mshtakiwa Ling'wenya: Nilikuwa kwenye kampuni ya Mhindi. Niliacha huko nakumbuka nilipigiwa simu na Denis Urio kwamba Mbowe anahitaji ulinzi wa VIP Protection

Jaji: Naomba uwe unatoa sauti ili watu wote wasikie.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tarehe 5 mwezi wa 8, 2020, nakumbuka nilikuwa Moshi. Nilivamia na askari Polisi nikawekwa kwenye gari na kupelekwa Central Police Moshi.

Askari walikuwa zaidi ya wanane. Walivyotuvamia hatukujua kama ni Polisi maana hawakujitambulisha, baada ya kuingia kwenye gari na kufungwa pingu mmoja akatoa amri kwenda police Central.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nilikuwa na Adamu Hassan Kasekwa (mshtakiwa wa pili)

Mshtakiwa Ling'wenya: Nawakumbuka baadhi, nakumbuka Goodluck Minja, Mahita, Jumanne, Ramadhani Kingai, ndio hao nawakumbuka kwa majina.

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya kufikishwa Moshi niliwekwa selo baada ya muda nikatolewa nikapelekwa kwenye chumba ambacho nilikuta kuna watu wengi... Ni eneo la palepale Central.

Mshtakiwa Ling'wenya: Waliokuwemo humo chumbani ni wale niliowataja mwanzo na wengine sikuwafahamu. Nilikuta wana simu zao wakawa wanarekodi na nikaanza kuhojiwa  nini kilichokuleta Moshi

Mshtakiwa Ling'wenya: Aliyekuwa ananihoji ni Jumanne anadakia Mahita, sababu nilipokuwa najibu kuwa ni VIP protection kwa Mheshimiwa Mbowe wao wakawaa wanasema sisi tunajua kilichokuleta huku usitudanganye.

Mshtakiwa Ling'wenya: Aliyeniambia hayo maneno ni Jumanne.

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya kuniambia hivyo Mahita akasema huyu si hataki kusema. Nilikuwa nimefungwa pingu, akanifunga akachukua bomba akapitisha bomba katikati ya miguu akanyanyua  nikabinuka nyayo zikawa juu kichwa chini.

Mshtakiwa Ling'wenya: Mahita akaanza kunipiga kwenye nyayo. Zoezi hili lilichukua makadirio kama nusu saa.

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya kupigwa pale sana na kilichokuwa kinaulizwa sasa ni kilio tu sina la kuongea. Nikasikia sauti humo nadhani ya askari kuwa msipige.

Mshtakiwa Ling'wenya: Wakanifungua kisha wakaninyanyua mpaka selo. Kipindi mimi napelekwa kuadhibiwa Adamoo yeye alikuwa selo maana yeye ndo alianza kuondoka ingawa sikujua anapelekwa wapi. Alikuwa selo nyingine.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hiyo ilikuwa tarehe 5 mwezi wa 8 nilikuja kutoka tena kesho yake tarehe 6, mwezi wa 8, 2020 ambapo nilifungwa kitambaa kizito nikajua safari imeanza.  Muda siwezi kukumbuka ila majira ilikuwa ni jioni sababu jua lilikuwa limeshaanza kupungua.

Mshtakiwa Ling'wenya: Madai kuwa tulipofikishwa Central Police (Moshi) tulitoka tena na kuanza kuzunguka sehemu mbalimbali na polisi ni uwongo, tulivyoingia hatukutoka mpaka tulipochukuliwa na kuanza safari.

Mshtakiwa Ling'wenya: Sikujua tunaenda wapi ila ilikuwa ni safari ya muda mrefu. Siwezi kusema masaa rasmi ila safari ilianza jioni na tulifika Alfajiri.

Mshtakiwa Ling'wenya: Wakati tuko kwenye gari kabla sijafungwa kitambaa walikuwemo kina Goodluck na wengine walioongezeka sikuweza kuwafahamu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hawa niliowataja niliwajua majina maana tangu walipotukamata mpaka tunapekekwa mahakamani tulikuwa nao na wakawa wanaitana majina.

Mshtakiwa Ling'wenya: Njiani (kuelekea Dar) hakuna kilichotokea ila ni mimi tu nilichoka shingo nainamishwa, lakini gari kusimama popote hakuna.

Mshtakiwa Ling'wenya: Mpaka hapo tayari nilikuwa nimeshajihisi ni matekwa maana nimepigwa pingu, sina uhuru wowote, nilishajihisi niko kwenye himaya yao.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tulipofika Dar bado nilikuwa nimefungwa kitambaa nikashushwa nikainamishwa hivyo na kitambaa change nikaingiza selo.

Wakili Matata: Baada ya Kufika selo

Mshtakiwa Ling'wenya: Waliponifikisha walinifungua kitamba cha usoni, wakanifungia. Niliposogea kwenye nondo nikaona kuna selo nyingina na kuna watu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hao watu wakanisogelea wakanza kuniuliza nini tatizo nikawaambia nimekamatwa Moshi sijui tatizo.

Mshtakiwa Ling'wenya: Yule mmoja akaniambia hapa ni Tazara na wanaoletwa hapa ni kwa tuhuma za kigaidi. Sisi unaotuona hapa ni tuhuma za ugaidi wakaniuliza ulikuwa unafanya kazi gani. Nikawaambia nilikuwa Askari

Mshtakiwa Ling'wenya: Naye akasema alikuwa Askari kikosi cha Twalipo kwa Aziz Ali, alikamatwa akiwa msikitini.

Mshtakiwa Ling'wenya: Pikipiki yake alikuwa ameiacha nje alipotoka msikitini akakuta imefungwa akakamatwa akapelekwa Tazara.

Mshtakiwa Ling'wenya: Alipokamatwa hilo suala alikuwa halijui lakini akasema alishaambiwa ni ugaidi.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nami nilijitambulisha ni Askari wa Kikosi cha 93KJ Kikosi cha Makomando

Mshtakiwa Ling'wenya: Kisha akasogea mwingine akasema yeye ni Sheikh wa Manyara. Walikwenda kumchukua wakamwachia wakamchukua tena

Mshtakiwa Ling'wenya: Pale kulikuwa na askari mmoja aliyekuwa anahusika anaitwa Sajenti Kidume, nipomuomba mswaki akasema kuwa yeye hahusiki nami kwa sababu niko pale kwa maelekezo.

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya muda nilikuja kutolea selo nikapanda juu kuna chumba na nikakuta soda juu ya meza ikiwa imepambwa na kitambaa, wakaingia watu ambao nawafahamu, Alex Ahadi na Chum Chungulu nilikuwa nao kule 92 KJ.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hiyo siku ilikuwa tarehe 7, mchana

Mshtakiwa Ling'wenya: Waliingia hao wawili nimapata kusalimiana nao, wakanisogelea wakaniuliza umetoke wapi nikawaambia sijui. Alex Ahadi akaniambia usiwe na wasiwasi hapa ni Polisi Tazara.

Mshtakiwa Ling'wenya: Mara akaingia Mahita, Jumanne, Goodluck, Kingai akaongezeka na mtu aliyeingia na video camera.

Mshtakiwa Ling'wenya: Walikuwa wananihoji jinsi nilivyompata mwenyekiti  Freeman Mbowe, kilichonipeleka Moshi na nani akiyeniunganisha na Freeman Mbowe.

Mshtakiwa Ling'wenya: Pale nilikuwa nikihojiwa na Omar Mahita.

Mshtakiwa Ling'wenya: Niliwajibu kwamba aliyeniunganisha na Freeman Mbowe ni Denis Urio ambaye ni Luten wa Jeshi 92 KJ na kazi aliyokuwa ameniambia ni VIP Protection

Mshtakiwa Ling'wenya: Kwa makadirio shughuli hiyo ya kunihoji dakika 30 hazifiki. Na aliniuliza sababu ya kwenda Moshi nikamwambia nilikuwa namfuata bosi ili tukaelewane naye.

Mshtakiwa Ling'wenya: Walikuwa wananichukua video na baada ya kumaliza hilo wakanirudisha selo.

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya kurudishwa selo nilipofungiwa ndo ulikuwa mwisho wa kunifungulia.

Mshtakiwa Ling'wenya: Ilipofika tarehe 8 wale wengine ambao walikuwa wanaona huko nje wakaniambia jamaa wanakuja (Askari Polisi) lakini hawakufika kwenye selo yangu. Walizunguka nyuma wakiongea na simu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nikishawafahamu, kwanza nilimuona Good luck akaongea na simu baadaye Chuma Chungulu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tarehe 9, nilikuwa nasikia mtu analia, nilipochungulia hivi huko nyuma nikamuona mtu nikamtambua alikuwa ni Denis Urio.

Mshtakiwa Ling'wenya: Denis Urio Namfahamu nilishanya naye kazi 92, Kikosi cha Makomandoo

Mshtakiwa Ling'wenya: Kule kwenye magari sikuona walichokuwa wanamfanya Urio, ila niliona anatolewa wkuwa nilishasikia sauti ya kilio kwa ufahamu wangu nilijua alikuwa anapigwa.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hiyo tarehe 9 usiku, nikafunguliwa selo, nikafugwa kitambaa, nikaingizwa kwenye gari tukaondoka. Selo alinitoa Goodluck na Mahita.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tulikokuwa tunaenda mimi sikufahamu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Safari zetu mimi na Adamoo zilikuwa za kufungwa kitambaa ila tukiwa selo tulikuwa tunaongea mfano tulipokuwa Tazara baada ya kutambua kuwa tuko selo zinazokaribiana.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tulikuwa tunasalimiana namuuliza vipi hali, mahabusu pale Tazara nilikowekwa kulikuwa kuna selo nyingine mbele yangu ndio wakaniambia mwenzako kawekwa huku, na nilipomuita kwa sauti akaitikia.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hiyo safari (ya Agosti 9, 2020) mwanzo sikuifahamu nilifungwa kitambaa lakini wakati tunaendelea huyo Goodluck akawa ananitikisa na bastola kuwa hapa usilete ujanja na nikileta  usumbufu watanipoteza nitulie hivyohivyo.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tulipofika gari ikasimama wao wakashuka na baada ya muda nikasikia sauti, mshushe huyu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nikafunguliwa mlango  nikashikwa kwenye suruali nyuma nikapelekwa kaunta nikafunguliwa kitambaa ndio nikamuona kuwa ndiye huyu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Niliingizwa selo akaja Jumanne akanipa kikaratasi akaniambia kuanzia leo shika hiki kikaratasi akija mtu mwambie wew ni Johnson John, kile kikaratasi kilikuwa kimeandikwa Johnson John.

Mshtakiwa Ling'wenya: Kwenye hiyo safari ndani ya gari siwezi kusema idadi kamili maana nilifungwa kitambaa, lakini niliposhuka alinishika Goodluck, akaja Jumanne na Kingai

Mshtakiwa Ling'wenya: Baadaye nilikuja kufahamu pale ni Mbweni baada ya kuuliza. Kuna Askari mmoja alikuwa ni Koplo, nikamuuliza hapa ni wapi? Akasema hupajui, utapajua tu na utasema akaondoka

Mshtakiwa Ling'wenya: Baadaye muda huohuo akarudi akaanza kuniuliza particulars zangu nikamwambia nilikuwa Askari 92 ( Kikosi cha Jeshi). Tulivyoongea sana akaniambia hapa ni Mbweni Polisi na kama wewe ni komando basi mmeshafika watatu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nikamuuliza huyo wa tatu ni nani, akaniambia mmoja mmeingia naye mwingine nilipomuuliza akasema ni Luten wa Jeshi naye ni Komando.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nikamuuliza yuko yukoje  huyo?  Akaniambia ni mweupe anaitwa Urio jina nikamtajia Denis.

Mshtakiwa Ling'wenya: Alisema huyo mwingine akijaribu kumsemesha anajificha

Mshtakiwa Ling'wenya: Akaenda huko akarudi akaniambia ndiye Denis Urio, anasema yeye aliwatafutia kazi kwa nia njema tu hayo mengine hayafahamu, nikamwambia mwambie na huyo Adamu asiwe anajificha, tuwe tunasalimiana.

Mshtakiwa Ling'wenya: Hivyo Tulikuwa tunasalimiana kwa sauti.

Mshtakiwa Ling'wenya: Walivyoniacha pale kesho yake tarehe 10 mwezi wa 8, 2020, alikuwa anapita Mkuu wa Kituo, mwanamke.

Mshtakiwa Ling'wenya: Alipofika kwangu akaniuliza unaitwa nani, nikamwambia Naitwa Johnson John. Akaniambia nini kilichokuleta huku, nikampa maelezo na kazi yangu, na kazi niliyokuwa naifuatilia mpaka nikakamatwa.

Mshtakiwa Ling'wenya: Akaniambia wewe niambie jina lako la ukweli ndipo nikamwambia Mohamed Abdillahi Ling'wenya.

Mshtakiwa Ling'wenya: Baada ya kumtajia majina yangu aliniahidi kuwa tutakusaidia, akaondoka mpaka asubuhi

Mshtakiwa Ling'wenya: Alipoondoka yeye muda mfupi akaja Goodluck, Jumanne na Mahita waliponifungulia nikakutana na Alex Ahadi na Chuma Chungulu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nikaingizwa kwenye chumba fulani hivi. Hicho chumba kutoka selo nilikokuwa nilitembea kwenye korido nikapishana na Urio, nikakata kona kulia na kisha kulia tena nikakutana na chumba na ndani tena kuna chumba kinaitwa Ofisi ya Upelelezi, nikaishia chumba cha nje.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nilipokataa pale, Goodluck akawa amesimama mlango akaja Jumanne na bahasha akaifungua akasema bwana hatutaki usumbufu maana kila kitu tumeshakijua. Chukua hayo makaratasi usaini.

Mshtakiwa Ling'wenya: Niliangalia mlango nikamuona Goodluck amesimama na bastola akaniambia ukitaka kuleta ujanja wako tutakufanya kama tulichokuwa Moshi.

Mshtakiwa Ling'wenya: Niliogopa kwa mazingira yale ya bastola na wakati nafikiria pale kusaini akapitishwa Adamu mimi nikiwa nimekaa na Jumanne.

Mshtakiwa Ling'wenya: Zile karatasi alizotoa Jumanne sikupata kufahamu ni za nini hakunipa hata ruhusa ya kusoma alichotaka ni kusaini tu.

Mshtakiwa Ling'wenya: Aliziweka mezani nikasaini akazirudisha tena kwenye bahasha.

Mshtakiwa Ling'wenya: Nilipelekwa selo nikakaa pale. Mkuu wa kituo ananiambia tunaendelea kufuatilia

Mshtakiwa Ling'wenya: Hadi Tarehe 19,2020 nikatolewa selo, nikaingizwa kwenye gari baadaye Adamu naye akaletwa, tukaingizwa na tukaambiwa tusijali haki tutaipata Mahakamani.

Mshtakiwa Ling'wenya: Kuanzia Moshi hatukula chochote, safarini pia hatukupata chakula, Tazara tulifika tarehe 7 alfajili mchana tulipata ugali na mboga za majani.

Mshtakiwa Ling'wenya: Jioni hatukula tena Tazara mpaka tunaondoka. Mbweni nilikuwa napata lesheni lakini si ile mahabusu wote wanapewa bali nilikuwa napewa na yule askari, mpaka tulipopelekwa Mahakamani.

Mshtakiwa Ling'wenya: Mahakamani Kisutu tukiwa mahabusu, Goodluck alileta chakula wali na dagaa ndio tukala.

Mshtakiwa Ling'wenya: Tangu nikiwa Moshi, Tazara na Mbweni sikuwahi kuwasiliana na mtu mwingine yeyote.

Mshtakiwa Ling'wenya: Kila kituo tulichokuwa tunapelekwa nilichokuwa naomba naambiwa wewe hautuhusu na hao kina Goodluck, Jumanne ndio hawakuwa wanataka kusikia kitu chochote.

Mshtakiwa Ling'wenya: Central Police Dar. Sijawahi kufika, nilikamatwa Moshi nikaletwa moja kwa moja Tazara na kila kituo  nilikuwa nawekwa moja kwa moja selo sijawahi kurekodiwa kwenye kitabu chochote.

Mshtakiwa Ling'wenya: Siku ile Msemwa (shahidi wa pili wa kesi ndogo) aliposema alikuwa Central na alinipokea na baadaye akahamishiwa Oysterbay na siku ileile nilimuomba wakili wangu anisaidie kuandika barua ya kwenda kwa (Kamanda wa Polis Mkoa Ilala) ili aithibitishie mahakama kwa kunipa movement order ya kwenda Oysterbay, OB ( Kitabu cha Matukio) kuangalia matukio ya siku hiyo na Station Diary kuthibitisha kuwa siku hiyo aliingia kazini.

Mshtakiwa Ling'wenya: Barua hiyo aliiandika Wakili Kibatala na saini yake naifahamu kwa sababu ndiye kiongozi wa jopo la mawakili na tangu tukiwa Kisutu ndiye alikuwa anashughulika na kusaini makaratasi

Mshtakiwa Ling'wenya: Nikiiona barua hiyo nitaitambua kwa kuona jina langu, namba ya kesi namba 16 ya mwaka 2021, Mhuri wa Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Divisheni.

Jaji: Nina wasiwasi Kuna watu wanamsaidia shahidi, Naomba wengine muwe watazamaji mumuache shahidi ajibu.

Matata: Shahidi Ukijibu muangalie Jaji Kumtoa wasiwasi wa majibu yako.

Wakili Matata anaendelea kumuongoza shahidi namna ya kuitambua barua hiyo na anaiomba mahakama amuoneshe shahidi barua hiyo.

Mshtakiwa Ling'wenya baada ya kuangalia nakala hiyo anasema: Ndio yenyewe, nimeona Kuna kesi namba 16/2021, kingine nimeona jina langu Mohamed Abdillahi...

Wakili wa Serikali Mwandamizi Pius Hilla anapinga kuwa hayo mengine hakuyasema ya namba na jina.

Jaji Tiganga: Amesema kesi namba na jina ingawa hakutaja ni jina la nani?

Wakili Matata anaendelea kumuongoza naye akasema;

Mshtakiwa Ling'wenya: Kingine ni saini ya Kibatala, Divisheni ya Makosa

Pingamizi tena kutoka kwa Wakili Hilla akidai kuwa anakokwenda siko

Kisha Mshtakiwa Ling'wenya anaendelea na kueleza kuwa vingine ni vitu alivyoviomba kama diary....

Mara nyingine anasimama Wakili wa Serikali Mwandamizi Abdallah Chavula anapinga kuwa shahidi anasoma na hapaswi kwenda huko na Jaji Tiganga anamuongoza shahidi asisome bali ataje mambo aliyoyasema mwanzo kuwa akiyaona ndio yatamfanya aitambue.

Kisha shahidi akiongozwa na wakili Matata, anaiomba mahakama iipokee barua hiyo kuwa sehemu ya ushahidi wake.

Mawakili wa Serikali wanaikagua barua hiyo.

Wakili Kidando anasimama na kuieleza mahakama kuwa wanapingamizi kupokewa kielelezo hicho kwa sababu moja ni suala zima la competence.

Shahidi aliyeko mahakamani siyo competence na kielelezo anachotaka kukitoa pia siyo competent.

Pingamizi letu la pili ni suala zima la kutoku-establish chain of custody na la tatu ni barua hii inakosa uhusiano (lacks relevance) na la nne this witness has not laid foundation before seeking to tended this exhibit (shahidi huyu hajaweka msingi kabla ya  kuomba kuitoa Mahakamani). Kwa hiyo tunaomba ahirisho fupi kabla ya kuleta hoja zetu.

Wakili Kibatala: Kwanza tunapinga kabisa hilo ombi la atonement, lazima kwanza kuangalia muda, tumeanza saa ngapi na kwa nani kachelewesha.

Lakini pia huyu ni mshtakiwa wa tatu na ana wakili wake, hivyo nasi tunapaswa tuulizwe kama tunapinga.

Jaji Tiganga anakubaliana na hoja ya pili ya Kibatala ana anawataka mawakili wa utetezi kama wanapinga.

Wakili Mtobesya anasema anakubali barua hiyo kupokewa na anaanza kutoa sababu

Wakili wa Serikali Chavula anasimama na kupinga kuwa huo ni utaratibu mpya kwani haijawahi kutoa mtu anakubali kupokea kielelezo kisha anatoa sababu za kukubali. Kama anakubali basi mambo yanaisha.

Wakili Mtobesya:  Nami sijawahi kuona sheria inamzuia mtu kutoa sababu na kwamba huo utaratibu unaotaka kuletwa na upande wa mashtaka haupo.

Jaji Tiganga anakubaliana na upande wa mashitaka akisema kuwa hicho anachokifanya Mtobesya watakifanya wakati wa kutoa hoja na kwamba akiruhusu hicho maana yake atakuja kukirudia.

Mtobesya: Sawa Mheshimiwa, basi naomba iingie kwenye rekodi kwamba nakubali ipokewe lakini kwa sababu nitakazozitoa.

Wakili wa Serikali Hilla anasimama tena na kusisitiza hoja za Chavulla na anahoji kama nao ni parties kwenye suala hilo.

Wakili Kibatala anasimama na kuhoji kuna sheria gani inayomzuia kuunga mkono hoja na kutoa sababu na kwamba kuna upande unadhani kuwa una haki zaidi wakati mahakama ilishaamua kuwa pande zote kwenye kesi zina haki sawa ana akaomba utolewe uamuzi.

Jaji anatoa mwongozo kuwa hakuna mtu amesema sheria inamzuia bali alichokikataa kwa Mtobesya ni kufanya marudio wakati wa kutoa hoja.

Baada ya Jaji Tiganga kutoa mwongozo kwamba kila mtu awe anapinga au anaunga mkono atatoa sababu zake na mahakama itatoa uamuzi, mawakili wa utetezi wanaendele.

Wakili John Mallya: Nami nakubali ipokewe kwa sababu nitakazozitoa.


Wakili Kibalata: Nami naunga mkono kwa sababu nitakazozitoa.

Jaji Tiganga baada ya majadiliano mafupi ya pande zote anakubali ombi la kuahirisha kwa muda kama upande wa mashtaka ulivyoomba.

Jaji Tiganga: Naahirisha kesi hii hadi saa 9:10

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments