MTATURU AMBATIZA JINA WAZIRI MKUU KUWA AFISA UGANI MKUU.

 

………………………………………………………….

MBUNGE wa Singida Mashariki, Miraji Mtaturu(CCM),amependekeza maeneo mawili ya kutiliwa mkazo katika mapendekezo ya mwongozo wa maandalizi ya mpango wa Bajeti ya Serikali na mapendekezo ya mpango wa maendeleo wa Taifa kwa mwaka 2022/2023 ambayo ni Kilimo na Miundombinu ya barabara.

Akichangia mapendekezo hayo Novemba 8 Bungeni Jijini Dodoma,Mtaturu amesema kama kweli serikali inataka kuwekeza kwenye sekta ya kilimo lazima iwe na angalau Trilioni moja.

“Tupo kwenye theory zaidi hatupo kwenye practical, niombe serikali kama kweli tunasema tunataka kuwekeza tuhakikishe tunapata angalau trilioni moja ili iwekezwe kwenye sekta ya kilimo, tuweze kupata maafisa ugani wa kutosha, mbolea ya uhakika lakini zaidi tuwe na uhakika wa maafisa ugani katika vijiji vyetu tusipofanya hivyo hatuwezi kuvuka na hatuwezi kubadilisha kilimo chetu,”alisema.

Mtaturu amesema kwa sasa wanaongelea habari ya kilimo cha kutegemea mvua na Mamlaka ya Hali ya hewa wameshatangaza kupata mvua chini ya wastani msimu unaokuja.

“Je mkakati umekuja vipi katika eneo hili ,tunayotaarifa nzuri tunaletewa na serikali, hali ya hewa wametuambia hatutakuwa na mvua ya kutosha sisi kama taifa tumejiaandaaje au tunasubiri baadae tuseme kulikuwa na changamoto ya mvua chache wakati tulijua kabla,”aliongeza.

Amesema kwenye eneo la uwekezaji wa mabwawa kwa ajili ya kilimo cha umwagiliaji Serikali kupitia mpango huo haijasema imejiandaa vipi kuwasaidia wakulima nchini.

“Lakini juzi tuliazimia hapa kama bunge tukaielekeza serikali itafute fedha ya kununua mazao kutoka kwa wakulima kwa hiyo kuna mambo mawili yanagongana hapa tunahamasisha wakulima walime lakini mwisho wa siku hakuna masoko yakutosha ambayo yalipaswa yafanywe na serikali,”ameongeza.

Kuhusu miundombinu ya barabara amesema ili uchumi uweze kuimarisha ni lazima iwekwe miundombinu mizuri ya kutoa mazao kwenye maeneo ya wakulima.

“Katika eneo hili nitakumbusha barabara ambayo imetajwa miaka yote, mfano barabara ya Mkiwa- Itigi kwenda Makongorosi ilitengewa fedha na kwenye mpango uliopita ilisemwa itapelekwa Fedha kwa ajili ya kujenga kilomita 50
lakini juzi wamesema kilomita 20 na mpaka sasa tunavyoongea haijatangazwa,hili ni tatizo,

Ameongeza kuwa,”tuna barabara ya Singida kwa Mtoro kwenda Tanga, barabara ile ilitengewa kilomita 20 mpaka leo haijaanza, serikali ijipange vizuri kuleta mpango utakaotusogeza mbele,”amebainisha Mtaturu.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments