Recent-Post

Mwenyekiti CCM Mara atinga Rorya akagua miradi, asisitiza uaminifu fedha zilizotolewa na Rais Samia

 MWENYEKITI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Samuel Kiboye (No.3) ameendelea kutoa wito kwa Watanzania kuendelea kufanya kazi kwa bidii huku wakimuombea Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan ili azidi kuchapa kazi kwa kasi ambayo itaendelea kuinua viwango vya uchumi wa Taifa letu na jamii kwa ujumla.

Wito huo ameutoa wilayani Rorya Mkoa wa Mara wakati akiendelea ziara yake ya kutembelea na kukagua miradi mbalimbali inayotekelezwa na Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan.

Amesema, kasi ya utekelezaji wa miradi hiyo inaendelea kuridhisha huku akitoa wito kwa wazabuni watakaopata tenda za kununua vifaa kwa ajili ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,fedha iliyotolewa na Rais Samia Suluhu kutochelewesha vifaa kufika eneo husika akikagua.

Mheshimiwa Kiboye ameyasema hayo wakati akikagua ujenzi madarasa ya Shule ya Sekondari ya Prof.Philemon Sarungi iliyopo mjini Rorya.
"Niwatake madiwani,walimu wakuu na watendaji wa Serikali kuhakikisha mnasimamia vizuri fedha hii ya ujenzi wa vyumba vya madarasa iliyotolewa na Mheshimiwa Rais Samia Suluhu ili kutimiza kiu yake ya kuhakikisha anatatua tatizo la upungufu wa vyumba vya madarasa shuleni.

"Niwaombe wananchi Rorya na Watanzania wote tuendelee kumuombea Mheshimiwa Rais Samia Suluhu azidi kuchapa kazi na mnaona jinsi ambavyo amejizatiti kusaidia Watanzania na ameonyesha umma kuwa, wanawake wanaweza,nimpongeze kwa kazi nzuri anayofanya,"amesema Mheshimiwa Samwel Kiboye.

Katika hatua nyingine, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Samwel Kiboye amekagua shamba lake la maembe katika Kijiji cha Ryagati kilichopo Kata ya Nyahongo wilayani Rorya mkoani Mara.

Wakati akikagua shamba hilo, Mheshimiwa Kiboye amewaasa wananchi kulima kilimo hicho huku akiwataka wataalamu wa kilimo kuangalia namna bora ya kuboresha zao hilo wilayani Rorya.
"Zipo aina mbalimbali za maembe yanayostawi katika Wilaya ya Rorya, hivi ndivyo hali ilivyo katika shamba langu,hivyo upo umuhimu wa wataalamu wa kilimo kuwashauri wananchi namna gani wanavyoweza kutumia zao hili kuwa fursa ya kiuchumi,"amesisitiza Mhe.Samwel Kiboye.

Wakati huo huo, Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Samwel Kiboye ametembelea kiwanda cha kufyatua matofali kwa lengo la kujua bei ya matofali ili kupata taarifa kamili.
Ni baada ya kubaini kuwa umekuwepo mchezo mchafu kwa baadhi ya wazabuni kuweka bei kubwa wanapoomba tenda.

"Afadhali hapa Empire mnauza shilingi 1500, kuna wengine wanauza shilingi 2650,"alibainisha Mwenyekiti huyo huku akiongeza kuwa, kwa yeyote ambaye atabainika kufanya ndivyo sivyo, Serikali itachukua hatua kali.

Pia Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Samwel Kiboye aliambatana na Mwwnyekiti wa Halmashauri ya Tarime Mji ambaye pia ni Diwani wa Kata ya Nkende, Mheshimiwa Daniel Komote kukagua maendeleo ya ujenzi wa vyumba vya madarasa,fedha iliyotolewa na Rais Samia katika Shule ya Sekondari Nkende.
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Mara, Mheshimiwa Samwel Kiboye akiteta jambo na Mkuu wa Wilaya ya Rorya, Mheshimiwa Juma Chikoka (Mchopanga) alipotembelea katika ofisi za wilaya ya Rorya ambapo amesisitiza usimamizi bora wa fedha zinazotolewa na Serikali huku akimpongeza DC huyo kwa kusimamia miradi ya maendeleo.

Post a Comment

0 Comments