Ngara yawawezesha vijana bodaboda, waanza kuneemeka kiuchumi

 Halmashauri ya Wilaya ya Ngara mkoani Kagera imewezesha vijana wake 33 mikopo nafuu ya usafiri wa bodaboda yenye thamani ya zaidi ya shilingi milioni 59.

Mfano wa pikipiki ambazo zimekuwa zikitumiwa na vijana wengi kujiajiri kwa ajili ya kubebea abiria, kazi ambayo imekuwa ikiwangizia vipato vikubwa kama ambavyo huko wilayani Ngara Mkoa wa Kagera zilivyoanza kuwaneemesha kiuchumi.(NA MTANDAO).

Solomon Kimilike ambaye ni Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri hiyo ameyasema hayo ofisini kwake huku akisisitiza kuwa, hiyo ni hatua moja wapo ya halmashauri kuhakikisha vikundi mbalimbali vya vijana vinajengewa uwezo ili kujiendeleza kiuchumi.

Kimilike amesema, mikopo hiyo ambayo inatokana na asilimia 10 ya mapato ya ndani ya halmashauri ni sehemu ya utekelezaji maelekezo ya Serikali iliyopo madarakani chini ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) kupitia ilani yake ya uchaguzi ambapo vijana wanapewa asilimia nne, wanawake nne na watu wenye walemavu asilimia mbili.

"Tumevikopesha vikundi viwili vya vijana vyenye jumla ya wanachama 33 jumla ya bodaboda 26 zenye thamani ya shilingi milioni 59.8, na katika mwaka ujao wa fedha pia tutatoa bodaboda zingine kwa vikundi vya vijana kwa ajili ya mradi wao wa usafirishaji abiria,"amebainisha Mkurugenzi huyo.

Pia amesema kuwa,kwa mwaka uliopita halmashauri yake ilitoa zaidi ya sh ilingi milioni 169 ili kuwezesha wananchi kiuchumi ambapo jumla ya vikundi 13 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu vilinufaika.

Mkurugenzi Mtendaji huyo ameongeza kuwa,kati ya vikundi 13 vilivyonufaika vya vijana vilikuwa vitano, vya wanawake vitano na watu wenye ulemavu vitatu ambapo aliyataka makundi yote kutumia mikopo hiyo vizuri na kwa kazi iliyokusudiwa na warejeshe kwa wakati.

Kwa upande wake Afisa Maendeleo ya Jamii wa halmashauri hiyo, Emanuel Kulwa amesema kuwa, halmashauri imeongeza kazi ya ukusanyaji mapato kutoka katika vyanzo vyake vyote ili kuhakikisha vikundi vingi zaidi vinawezesha mikopo hiyo.

Ametaja vikundi vya vijana vilivyopatiwa mikopo ya bodaboda kuwa ni Twitezimbele na Mkombozi vilivyopo katika Kata ya Ngara Mjini na kuongeza kuwa vikundi vingine vitatu vya vijana vilikopeshwa shilingi milioni 48 kwa ajili ya miradi yao.

Kwa upande wao, viongozi wa vikundi hivyo, Jafeti Makule wa Kikundi cha Twitezimbele amesema kuwa, mkopo huo umewainua vijana kwa kuwa sasa wana vipato vya uhakika na wengi wao wamejenga nyumba na kuoa wake.

Nnaye Eustachius Laurant ambaye ni Mwenyekiti wa Kikundi cha Mkombozi amesema kuwa, wamejiwekea utaratibu wa kurejesha kiasi cha sh.milioni 2.5 kila mwezi na ana uhakika ifikapo mwezi Juni, mwakani watakuwa wamerejesha mkopo wote ili uweze kunufaisha wengine.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments