Recent-Post

Rage afunguka mazito ujio wa kocha mpya Simba SC

 ALIYEWAHI Mwenyekiti wa Klabu ya Simba,Ismail Aden Rage amewataka mashabiki wa klabu hiyo ambayo ni mabingwa wa Ligi Kuu ya Tanzania Bara kuvuta subira na kumpa muda kocha mpya Pablo Franco Martin, mzaliwa wa Madrid, nchini Hispania.

Rage amesema anamtazama Pablo Franco Martin kwa jicho la mafanikio zaidi, hivyo hakuna haja ya kuwa na mihemko ya kizamani kwani, mafanikio ni polepole.

Mimi nliliposoma wasifu wa huyu kocha mpya wa Simba nimeamini kuwa Simba inazidi kupaa kiuongozi na uendeshaji wake.Kwani huyu kocha ni kocha ambaye ana kiwango kikubwa sana ila kakosa bahati tu angekuwa kocha wa Madrid ingependeza

Kwanza mwisho wa kuona kocha kama huyu hapa Tanzania ilikuwa mwaka 2008 tulipoleta kocha kutoka Brazil na wasaidizi wake na hadi leo nilikuwa sijaona kocha tena mwenye kiwango kama hicho ndio ninashudia tena leo amekuja Pablo.

Huyu kocha wanapaswa viongozi wasimuingilie mipango yake hata kidogo, wamsikilize kwanza ili waone makubwa yanayokuja pale Simba SC ninaamini biriani limerejea lililopotea miaka mingi.

Pia nawaomba mashabiki tusiwe na 'pressure' (mihemko) maana mkiwa na 'pressure' ninyi mtamfanya kocha awe hana imani na kila kitu anachokifanya, najua mashabiki kila siku mnahitaji mambo mazuri tu bila kujua kuwa hayo mazuri yanakuja taratibu.

Aidha, Rage alipoulizwa itakuwaje kuhusu Derby na ukizingatia imebakiza michezo michache tu ifike na Derby huwa na 'pressure' yake na mara nyingi huwa inafukuzisha makocha kwenye klabu nyingi.Rage amesema kuwa...

Viongozi wangekuwa na roho kama yangu na mafikirio kama yangu sisemi ni marefu sana au ni mazuri sana kuhusu Derby, Yanga hata watufunge miaka 10 mfululizo mimi hata sina kinyongo maana wanatufunga ila kikubwa ni kubeba kombe tu basi sina haja ya kuwafunga Yanga mimi.


Kocha Pablo ni nani?

Pablo Franco Martin, mzaliwa wa Madrid, nchini Hispania anatajwa kuwa miongoni mwa makocha wenye wasifu mkubwa kuwahi kutokea katika historia ya soka hapa Tanzania.

Akiwa amezaliwa Juni 11, 1980 mjini Madrid nchini Hispania na hadi anakuja kuwanoa Simba SC ana leseni ya UEFA Pro Licence ambayo inaelezwa kuwa ndiyo leseni inayotolewa kwa muhitimu wa mafunzo ya juu kabisa ya Ufundishaji na Usimamizi wa wa soka barani Ulaya.

Kocha huyo kijana ni miaka minne tu iliyopita alikuwa akifanya kazi na Kocha mwenye mafanikio makubwa Duniani kwenye mpira wa miguu akiwa kama mchezaji na kocha, Maestro Zinedine Zidane (Zizou) kwenye Klabu ya Real Madrid ya Uhispania kama kocha msaidizi. 

Pablo mbali na kuiongoza Real Madrid kama kocha msaidizi, aliwahi pia kufundisha timu za Getafe CF na Getafe B zote za Hispania, pia timu za Club Deportivo Santa Eugenia, Club Deportivo Illescas, Club Deportivo Puertollano zote za huko huko Hispania na FC Saburtalo ya Georgia.

Kocha huyo ana shahada ya juu ya kufundisha mbinu za mpira wa miguu, utimamu wa mwili wa mwanasoka na jinsi ya kuusoma na kuuchambua mpira wa soka timu zinapokuwa uwanjani.

Kocha Pablo anakuja Simba SC ikiwa nafasi ya pili na alama 11 kwenye msimamo wa Ligi Kuu Soka Tanzania Bara (NBC Premier League) msimu huu wa 2021-2022,ikiwa ndiyo timu pekee kwenye ligi ambayo haijafungwa bao hata moja.

Hata hivyo kumekuwepo na manung’uniko kutoka kwa baadhi ya washabiki wa timu hiyo kuwa kutokana na ukubwa wake na wachezaji walio nao haistahili kuwa hapo ilipo na hasa ukizingatia haikuwa na wakati mzuri kwenye Pre-season, na michuano ya Ligi ya Mabingwa ambapo licha ya kupata ushindi wa ugenini wa mabao 2-0 dhidi ya Jwaneng Galaxy ya Botswana, ilikuja kuchapwa mabao 3-1 kwenye uwanja wa nyumbani wa Benjamin Mkapa na kutolewa kwenye michuano hiyo ya mwaka huu ya Ligi ya Mabingwa barani Afrika.

Kazi kubwa ambayo kocha huyo Mhispania anatarajiwa kuifanya ni kuhakikisha Simba ambayo ni mabingwa mara nne wa Ligi Kuu ya Soka Tanzania Bara na kwa sasa anatetea taji hilo inarejea kwenye hadhi yake.

Post a Comment

0 Comments