RC MJEMA AELEZA KUTORIDHISHWA NA KASI YA UJENZI WA MADARASA SHULE YA MMANGU, KITUO CHA AFYA SALAWE

 

Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, (kulia) akishiriki shughuli za kufyatua Matofali katika ujenzi wa vyumba vya Madarasa katika Shule ya Sekondari Solwa. kushoto ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy.

Na Marco Maduhu, Shinyanga

MKUU wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, amefanya ziara ya kukagua miradi ya kimkakati katika Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga, na kueleza kutoridhishwa na kasi ya ujenzi wa vyumba vya madarasa katika Shule Mpya ya Sekondari ya Mmangu iliyopo Salawe wilayani humo.

Mjema amefanya ziara hiyo leo, akiwa ameambatana na Mkuu wa wilaya ya Shinyanga Jasinta Mboneko, Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy, Mwenyekiti wa Halmshauri Ngassa Mboje, wataalamu, pamoja na viongozi wa Serikali na Chama Cha Mapinduzi CCM.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa maendeleo ya ujenzi wa Madarasa Matatu katika Shule Mpya ya Sekondari Mmangu iliyopo Salawe wilayani humo, alisema hajafurahishwa na kasi ya ujenzi wake, ambapo kwa sasa ndiyo wanapima msingi, huku wakisaliwa na mwezi mmoja madarasa hayo yawe yameshakamilika.

“Nimefurahishwa na wananchi wa kijiji hiki cha Mmangu kujitoa kujenga Madarasa Sita kwa ajili ya kuanzisha shule mpya ya Sekondari, na sasa Rais Samia Suluhu Hassan ametoa Sh.milioni 60 kwa ajili ya ujenzi wa Madarasa matatu katika shule hii, ambayo yana takiwa Novemba 30 yawe yameshakamilika,”alisema Mjema.

“Kasi ya ujenzi wa Madarasa haya sijaridhika nayo, ambapo nilitaka nije kuona tena maendeleo yake baada ya wiki mbili, lakini nitakuja baada ya wiki moja kuona hatua ilipofikia, ili kama kuna tatizo mahali tuongeze nguvu”,aliongeza.

Aidha akiangalia maendeleo ya ujenzi wa kituo cha Afya Salawe, napo aliagiza kasi iongezeke, ili ujenzi huo ukamilike kwa wakati na kutoa huduma ya matibabu kwa wananchi, huku akimpongeza Rais Samia Suluhu Hassani kwa kutoa fedha za miradi mbalimbali ya maendeleo mkoani humo kiasi cha zaidi ya Sh.bilioni 26.

Katika hatua nyingine akizungumza na wananchi wa kijiji cha Mwasekagi Kata ya Solwa, aliwapongeza kwa kuwa mstari wa mbele kuchangia shughuli za maendeleo, na kutoa wito kwa wananchi wote mkoani humo, waendelee kushirikiana na Serikali katika maendeleo.

Kwa upande wake Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy, alimwahidi mkuu huyo wa Mkoa, kuwa maelekezo yote ambayo ameyatoa atayafanyia kazi ili kuhakikisha ujenzi wa Majengo katika kituo hicho cha Afya Salawe na vyumba vya Madarasa shule ya Sekondari Mmangu unakamilika kwa wakati.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, (kulia), akiwa katika ukaguzi ujenzi wa Madarasa katika shule mpya ya Sekondari ya Mmangu Kata ya Salawe wilayani Shinyanga, (kushoto) ni Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy.
Mkuu wa Mkoa wa Shinyanga Sophia Mjema, akizungumza mara baada ya kumaliza kutembelea maendeleo ya ujenzi wa Majengo kituo cha Afya Salawe na vyumba vya Madarasa shule ya Sekondari Solwa, na Mmangu.
Mkurugenzi wa Halmashauri ya wilaya ya Shinyanga Nice Munissy, akizungumza kwenye ziara hiyo ya Mkuu wa Mkoa na kuahidi kutekeleza maagizo yake yote.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments