Recent-Post

Ronaldo aokoa jahazi la Man United, Hakim Ziyech naye aiokoa Chelsea

 Cristiano Ronaldo ameendelea kuwa shujaa wa soka baada ya kuinasua Manchester United katika kipigo hatari kutoka kwa Atalanta katika mtanange wa Ligi ya Mabingwa ya UEFA maarufu kama Champions League.


Mtanange huo wa Novemba 2, 2021 umepigwa katika dimba la Stadio Atleti Azzurri d'Italia lililopo Jiji la Bergamo nchini Italia.
Kwa mbinu na juhudi shirikishi alizopata Ronaldo alifanikiwa kufunga goli katika kila kipindi kwenye mtanange huo mkali ambapo hadi mwisho wa mtanange ubao ulisoma mabao 2-2.

Josip Ilicic ndiye aliyeanza kuwanyanyua mashabiki wa Atalanta kwa kuachia bao safi ndani ya dakika 12 ya kipindi cha kwanza, bao ambalo lilidumu hadi dakika ya 45 na ushee ambapo Cristiano Ronaldo aliamua kuokoa jahazi kwa kuachia bao, hivyo hadi mapumziko ubao ulisoma Atalanta bao moja na Man United bao moja.

Kipindi cha pili kilianza kwa kasi, ambao Duvan Zapata ndani ya dakika 56 alianza vizuri kwa kuipachikia Atalanta bao la pili ambalo lilidumu hadi dakika ya tisini.

Wakati, Atalanta wakijiandaa kusherehekea alama tatu dhidi ya Man United, Cristiano Ronaldo aliamua bora yaishe kwa kugawana alama ambapo aliachia bao la pili ambalo liliwezesha miamba hao wa soka hadi mwisho wa mchezo ubao kusoma 2-2.

Kutokana na magoli hayo ya Ronaldo yanamfanya kuwa mchezaji wa kwanza kufunga mara nne mfululizo katika Ligi ya Mabingwa ya UEFA maarufu kama Champions League baada ya Ruud van Nistelroy mnamo April 2003.

Kwa matokeo hayo, Man United inaongoza Kundi F kwa alama saba sawa na Villarreal, huku Atalanta wakiwa na alama 5 na Young Boys ambao wanaburuza mkia katika kundi hilo wakiwa na alama 3.
Wakati huo huo, mabingwa watetezi wa Ligi ya Mabingwa Ulaya Chelsea wamefanikiwa kuondoka na alama tatu baada ya kuichapa Malmo bao 1-0.

Hakim Ziyech ndani ya dakika 56 ndiye aliwapa raha mashabiki wa Chelsea baada ya kufunga bao hilo ambalo lilidumu hadi dakika ya tisini, ni baada ya kuifanyia kazi nzuri pasi ya Callum Hudson-Odoi.

Mtanange huo umepigwa katika dimba la Eleda Stadion (Stadion Himmaborgen) lililopo mjini Malmo nchini Sweden.

Kwa ushindi huo, Chelsea inashika nafasi ya pili kwa alama 9 katika Kundi H ambalo linaongozwa na vinara Juventus kwa alama 12, Zenit alama 3 na Malmo alama sufuri. Tazama matokeo mengine hapa chini.
NA GODFREY NNKO

Post a Comment

0 Comments