SERIKALI YAJA NA MAREKEBISHO YA SHERIA YA MTOTO.

 


Katibu Mkuu Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu akizungumza katika Kikao Kazi kati ya Wizara na wadau kwa ajili ya kukusanya maoni ya marekebisho ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 Kilichofanyika jijini Dodoma.

Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Mwanaisha Moyo akifafanua jambo kuhusu masuala ya Ustawi wa mtoto wakati wa kikao kazi kati ya Wizara na wadau kwa ajili ya kutoa maoni ya rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 kilichofanyika jijini Dodoma.


Mkurugenzi wa huduma za Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Lucy Saleko akiwasilisha rasimu ya marekebisho ya ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 katika kikao kazi kilichowakutanisha wadau kutoa maoni kuhusu rasimu hiyo jijini Dodoma. 

Baadhi ya Wadau wakifuatilia hoja mbalimbali katika kikao kazi kilichowakutanisha na Wizara ya Afya (Maendeleo ya Jamii) na wadau kwa ajili ya kupokea maoni ya rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 jijini Dodoma.

Picha zote na Kitengo cha Mawasiliano Serikalini WAMJW

******************************

Na WAMJW Dodoma

Serikali kupitia Wizara ya Afya, Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wazee na Watoto, Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii imekutana na wadau wa masuala ya Watoto kupokea maoni yao kuhusu rasimu ya maboresho ya marekebisho ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 ili iendane na wakati na kusaidia kutatua changamoto mbalimbali zilizopo.

Akifungua kikao hicho jijini Dodoma,Katibu Mkuu Wizara ya Afya-Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii Dkt. John Jingu amewataka wadau hao kutoa maoni ili kuondoka na changamoto zilizopo katika Sheria hiyo.

Dkt. Jingu amesema utekelezaji wa Sheria hiyo inayolenga kumsaidia mtoto imekuwa ikikabiliwa na changamoto kadhaa na wadau wamekuwa wakiishauri Serikali kufanya marekebisho ya sheria hiyo ili iendane na wakati na kukabiliana na changamoto zilizojitokeza.

"Tulisikia maoni yenu kuhusu Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 na sasa tumewaita hapa kwa ajili ya kupokea maoni yenu kutokana na rasimu iliyoandaliwa ya marekebisho tupeni maoni yenu tupate Sheria iliyo bora" alisema Dkt. Jingu

Ameongeza kuwa kumekuwa na changamoto kubwa ya kusikilizwa kwa mashauri ya Watoto kutokana na kukosekana na Maafisa Ustawi wa Jamii ambapo ni lazima wawepo katika mashauri hayo hivyo kukwamisha mashauri hayo na kukosekana kwa kutolewa haki kwa Mtoto.

"Pale ambapo Maafisa Ustawi wa Jamii hawatoshi katika Maeneo yetu kunakwamisha ufuatiliaji na utekelezaji wa masuala ya Ustawi wa na Haki za mtoto hivyo, kinahitajika marekebisho ili kuweza kupata mbadala wa kutekeleza majukumu hayo pale ambapo Afisa Ustawi wa Jamii anakosekana" alisisitiza Dkt. Jingu

Mbali na kusimama kwa mashauri ya Watoto Mahakamani kutoka na upungufu wa Maafisa Ustawi wa Jamii ameyataja mambo mengine yanayochelewa au kukwamisha utekelezaji wake kuwa ni huduma za kuasili watoto, usajili na usimamizi wa vituo vya kulelea Watoto mchana na Makao ya Watoto.

Amesisitiza kuwa ili kukuza Ustawi na haki ya Mtoto kunahitajika marekebisho ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 kwa lengo la kuondoka na changamoto zilizopo katika utekelezaji wa Sheria hiyo.

Kwa upande wake Kamishna Msaidizi wa Ustawi wa Jamii Mwanaisha Moyo amesema kuwa Kikao hicho kitasaidia kupata uelekeo mzuri katika kuhakikisha masuala ya haki na Ustawi wa Mtoto vinazingatiwa katika utekelezaji wa masuala mbalimbali kuhusu mtoto.

Akiwasilisha rasimu ya marekebisho ya Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 Mkurugenzi wa Huduma za Sheria kutoka Wizara ya Afya Idara Kuu ya Maendeleo ya Jamii,Lucy Saleko ameyataja baadhi ya maeneo yaliyozingatiwa katika Sheria hiyo kuwa kila sehemu atakayotajwa Afisa Ustawi wa Jamii anatajwa pia Afisa Maendeleo ya Jamii ili kuwezesha utekelezaji wa majukumu hayo na kutokwamisha mashauri ya Watoto na masuala mbalimbali ya Haki na Ustawi wa Mtoto.

Baadhi ya Wadau wamesema marekebisho hayo ni muhimu kwani yatasaidia kuondokana na changamoto zilizokuwepo katika kutekeleza Sheria ya Mtoto na. 21 ya mwaka 2009 kwani imekuwa ikikwamisha utekelezaji wa majukumu hasa katika ngazi za chini.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments