Simulizi mtoto aliyefanyia mtihani akiwa gerezani

Mtoto Kunde Gambija Kilulu aliyefanya mtihani wa darasa la saba gerezani, akitumia Simu akiwa nyumbani kwao wakati wa mahojiano na mwandishi wa Mwananchi. Picha na Samirah Yusuph

Baada ya kusota gerezani kwa siku 123, Kunde Kilulu (15) hatimaye yupo uraiani akitumikia kifungo cha nje cha miezi sita akiwa chini ya uangalizi wa Idara ya Ustawi wa Jamii.

Mtoto huyo alikuwa katika gereza la Bariadi Mkoa wa Simiyu kwa kesi ya mauaji na baadaye Mahakama Kuu kanda ya Shinyanga ilipokea hoja ya kubadili hati ya mashtaka kuwa kesi ya kuua bila kukusudia iliyomuweka kifungoni Novemba 15, 2021.

Ikiwa ni historia iliyobeba machungu ya maisha yake ya elimu ya msingi, Kunde anasimulia kuwa maisha ya gerezani yalikuwa ni magumu na yasiyozoeleka kwa kipindi chote alichokuwao mahabusu gerezani.

“Kula na kulala ni kwa shida, kilichokuwa kinanikatisha tamaa ni watu niliowakuta kule ndani walivyokuwa wananibeza na kuniongelesha kwa sauti ya ukali. Kwa siku za mwanzo nilipoteza matumaini kabisa,” alisema.

Huku akilengwa na machozi, anasema kilichompa moyo na kurejesha matumaini ni baada ya mfungwa mmoja kumshauri na kumpa moyo kwamba kuwa gerezani haukuwa mwisho wa maisha.

Sikuamini maneno ya yule mtu kwa sababu sikuwa na uhuru tena na nilikuwa katika mazingira magumu hadi siku Mkuu wa magereza Mkoa wa Simiyu alipokuja kututembelea gerezani, ndipo nilipata nafasi ya kumwambia kuwa mimi ni mwanafunzi wa darasa la saba nimesajiliwa kufanya mtihani ninahitaji nipate kibali cha kufanya mtihani,” anasema.

Hatua hiyo ndiyo ilimrejeshea matumaini, kwani watu wote mle ndani walitambua dhamira yake na walianza kumpa ushirikiano hadi ilifikia hatua ya Ofisa elimu msingi Kata ya Nkoma, Jumanne Mongai kwenda kumtembelea akiwa gerezani na kumpelekea notisi kwa ajili ya kujisomea.

“Zilikuwa zimebaki wiki mbili kufikia siku ya kufanya mtihani, nilipata notisi pia nilipata mwalimu ambaye naye alikuwa mfungwa akawa ananifundisha hasa masomo ya sayansi na hisabati. Tulitumia muda wa mapumnziko saa nne hadi saa sita mchana,” anasema.

Baada ya saa mbili za mchana alipata tena muda baada chakula cha jioni na muda wa kulala alikuwa na saa tatu, hivyo saa mbili hadi muda wa kulala aliutumia kujisomea mwenyewe.

Usiku wa kuamkia siku ya mtihani nilisoma hadi saa tano usiku, nilivyoingia chumba cha mtihani sikuwa na hofu, lakini matumaini ya kufalu yalikuwa kidogo nilikuwa nikijitazama nipo jela sijui nitatoka lini na nilijiona kuna vitu vingi sijasoma,” anaeleza.


Safari ya mahakamani

Alisema wakati anapelekwa gerezani Julai 16, 2021, shauri la kesi iliyokuwa inayowakabili yeye na baba yake mzazi, Sayi Gisabu lilikuwa limefungwa katika mahakama nyingine, hivyo wakisubiri lisomwe Mahakama Kuu.

Kwa mara ya kwanza Novemba 8, 2021 kesi hiyo ilitajwa Mahakama Kuu na mwanasheria wa upande wa utetezi aliomba mahakama kubadilisha hati ya mashtaka kutoka kesi ya mauaji na kuwa ya kuua bila kukusudiwa na kwa pamoja walikiri kosa hilo.

Hukumu ya kesi ilipangwa kutolewa Novemba 10, 2021, lakini ilishindikana kwa sababu ustawi wa jamii walikuwa hawajawasilisha taarifa yao, hivyo tulirudishwa gerezani kwa ajili ya kusubiri siku ya hukumu ambayo ilipangwa kuwa Novemba 15,2021” anasimulia Kunde.

Anaeleza siku ya hukumu alipata mawazo kwa sababu hakujua nini kitatokea na alihofia kukosa nafasi ya kusoma iwapo atahukumiwa kuwa gerezani.

“Siku hiyo baba alihukumiwa miaka mitano jela na mimi miezi sita, kifungo cha nje,” anasema.


Usiku usiosahaulika

Usiku wa Julai 7, 2021 ni siku ambao Kunde hatamani ujirudie kwenye maisha yake kwa sababu ni usiku uliomfanya aitwe mahabusu katika gereza la Bariadi.

Akiwa hataki kufafanua zaidi, anasema alitoka shule alipokuwa katika kambi za kitaaluma kwa ajili ya maandalizi ya mtihani wa darasa la saba jioni ya Julai 6, ikiwa ni mapumnziko ya Sikukuu ya Saba saba.

Sikukuu ilikuwa vizuri na walilala salama yeye na kaka yake hadi saa tano usiku walipogongewa mlango na baba yao akiwaamsha na kuwaambia kuwa dada yao alikuwa na mwanaume ndani ya chumba chake.

Baba aligonga mlango wa dada akatoka akiwa peke yake alivyo ingia ndani jamaa aliyekuwa ndani alimsukuma na kukimbia. Tulimkimbiza na kuanza kumpiga kwa kutumia fimbo, kumbe tulimjeruhi vibaya (aliongea akitokwa na machozi) ndipo majirani aliwaita ndugu zake wakamchukua na kumpeleka kwenye matibabu”.

Aliyeuawa ni Gegedi Kulabya (57) tofauti ya miaka miwili na Sayi Gisabu (55) baba wa familia hiyo aliyekuwa faragha na binti wa familia hiyo mwenye umri wa miaka 36 na mama wa watoto wawili.


Maisha ya uraiani

Baada ya kutoka gerezani, Kunde yupo kijiji cha jirani tofauti na ilipo familia yake akiwa anapumzisha akili pamoja na kufanya maandalizi ya kuanza kidato cha kwanza mwakani.

Licha ya kuwa uraiani, alichokusudia kufanya baada ya kuwa huru kinashindwa kutimia kwa sababu uchumi wa familia yake umeyumba baada ya tukio hilo, hali iliyowalazimu kuuza mifugo na mashamba waliyokuwa nayo ili kulipa kifuta machozi kwa familia ya wafiwa.

“Kwa sasa bado sijajua kama nitaendelea na masomo japo ninatamani nisome, mama yangu ni mzee amebaki na jukumu la kuhudumia familia tukiwa hatuna hata mashamba ya kulima wala ng’ombe, hivyo kupata mahitaji ya shule itakuwa ngumu,” anasema.

Anasema baba yake alikuwa ni kila kitu katika familia, hivyo baada ya kuwa jela familia haijiwezi tena na kaka yake mkubwa aliyekuwa ni nguvu kazi ya familia alikimbia baada ya tukio.


Mama awaangukia Watanzania

Wakati wa mahojiano na Mwananchi kijijini kwao Dasina Wilaya ya Itilima, Mama Mbuke Sayi anaasema amefurahi mwanae kuwa huru, lakini hana uhakika kama ataweza kumudu gharama za mahitaji ya shule na familia.

“Roho inaniuma ninatamani mwanangu asome, lakini sina cha kufanya hivyo ninawaomba Watanzania wanishike mkono ili kutimiza ndoto za mwanangu.” anasema Sayi.

Juhudi za kuupata uongozi wa Wilaya ya Itilima kuzungumzia suala hilo haukufanikiwa jana baada ya simu zao kuita bila kupokelewa.


TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments