Spika Ndugai Kuzindua Ofisi Ya TCCIA Makao Makuu Dodoma Kesho

SPIKA wa Bunge la Tanzania Job Ndugai anatarajiwa kufungua Ofisi ya Chemba ya Wafanyabiashara, Wenye viwanda na kilimo hapa nchini (TCCIA), kama sehemu ya mikakati yake ya kufanikisha utekelezaji wa sera ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo mwaka 2025.


Akizungumza na waandishi wa habari Jijini hapa mara baada ya kikao cha ndani cha Bodi ya Wakurugenzi wa Chemba hiyo, Rais wa TCCIA Bw. Paul koyi amesema chemba chombo chenye mtandao mkubwa wa wafanyabiasha wenye viwanda na kilimo hapa nchini imejipanga kwenda sambamba na kufanikisha azma ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda.

“TCCIA tayari tumeshaanza kutekeleza azma hiyo ya serikali ya kujenga uchumi wa viwanda ifikapo 2025 kwa vitendo. Na sasa tunatarajia Mheshimiwa Spika Job Ndugai atatufungulia ofisi ndogo ya chemba hapa makao makuu ili kuongeza ufanisi wa hazi za chemba,” alisema Bw Koyi.

Bw Koyi alisema ufunguzi wa ofisi makao makuu ni mongoni mwa mipango ya TCCIA ya kufanya mageuzi ndani ya chemba ikiwemo ufanisi wa utoaji wa huduma zake kwa wanachama na watanzania kwa ujumla wake.

Alisema TCCIA tangu kuanzishwa kwake imekuwa ikiteleza majukumu yake kama yalivyoainishwa sambamba kushirikiana na wabia wake kutoka sekta za umma na binafsi katika kuchagiza maendeleo na ustawi wa jamii wakiwepo wanachama wake.

"Tunaendelea kutekeleza azma yetu kama TCCIA ya kuwasaidia wafanyabiashara hapa nchini kufikia malengo yao kwa kubeba changamoto zao, mawazo yao na mapendekezo ya nini kifanyike na kuyafikisha kwa wabia mbalimbali hasa wadau toka sekta za umma na kujadili namna bora ya kuboresha mazingira ya biashara ambayo yataleta tija.’’ Alisema bw, Koyi.

Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi mtendaji wa TCCIA Bw, Nebart Mwapwele amesema uzinduzi wa ofisi mpya iliyopo Mtaa wa Mazengo Dodoma utaongeza chachu na ari kubwa kwa wananchama waliopo Kanda ya Kati sambamba na kuziimarisha ofisi za mikoa zilizopo katika mikoa hiyo.

“ Napenda kuchukua nafasi hii kuwakaribisha wafanyabiashara wenye viwanda na kilimo kufika wa wingi kushuhudia uzinduzi wa ofisi yao mpya ambayo itajikita kusikiliza, kubeba mawazo na kuwasilisha changamoto zinazotukabili ili kuweka mzingira rafiki kwa wafanyabiashara,’’ Alisema Bw. Mwapwele.

Alisema wanachama pia watapata fursa ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Viwanda na Mazingira wakati wa hafla hiyo muhimu ya uzinduzi wa ofisi ya chemba.

‘Tunaamini fursa hii ya kukutana na Kamati ya Kudumu ya Bunge itafungua ukurasa mpya wa mashirikiano na kujadili namna bora wanayoweza kutuwakilisha katika Bunge letu la Jamuhuri ya Muungano wa Tanzania’’ alisema Bw. Mwapwele.

TCCIA ni taasisi yenye mtandao mkubwa nchi nzima ambapo mwaka 2007 ilishinda tuzo ya Afrika kwa kuwa na mtandao bora barani Afrika. Bodi mpya chini ya Raisi wake Bw Koyi imejipanga kutoa mchango stahiki katika ujenzi wa viwanda hapa nchini ikiwepo kuongeza uzalishaji wa mazao.
   
    Na Mwandishi Wetu, Dodoma

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments