Upinzani waunga mkono hotuba ya Rais Dkt.Mwinyi mwaka mmoja wa uongozi wake

CHAMA cha Demokrasia Makini kimesema kinaunga mkono kwa asilimia 100 hotuba ya Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Mheshimiwa Dkt.Hussein Ali Mwinyi aliyoitoa hivi karibuni kuhusiana na mwaka mmoja wa uongozi wake katika Ukumbi wa Hoteli ya Golden Tulip iliyopo Uwanja wa Ndege jijini Zanzibar.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Ameir Hassan Ameir Hassan ameyabainisha hayo ofisini kwake iliyopo Taveta jijini Zanzibar wakati akizungumza na vyombo vya habari.

Hassan amesema, hotuba ya Rais Dkt.Mwinyi imeleta matumaini makubwa kwa wananchi wote waliopo ndani na nje ya Zanzibar, hivyo wataendelea kumuunga mkono kwa asilimia zote ili aweze kutekeleza kwa ufanisi mipango yote aliyonayo kwa ajili ya kuinua viwango vya uchumi Zanzibar.

Amesema, miradi mbalimbali ya kimaendeleo ikiwemo katika sekta ya elimu, afya, maji, umeme na kuwawezeaha wajasiriamali wadogo wadogo inatarajiwa kutekelezwa jambo ambalo litawaondoshea usumbufu wananchi.

Pia amewaomba wasaidizi wake kumsaidia Rais Dkt.Mwinyi ikiwemo kuwa waamimifu na waadilifu ili kutimiza azma yake ya kuifanya Zanzibar iweze kupaa kiuchumi na kimaendeleo.

Wakati huo huo, Hassan amemuomba Mheshimiwa Rais Dkt.Mwinyi kusimama imara ilim kuhakikisha fedha zote kutoka IMF zinatumika kwa kusudi lililopangwa na pale ambapo atajitokeza mwenye nia ovu na fedha hizo, aweze kuchukuliwa hatua za haraka za kisheria.

"Naomba pia niwakumbushe viongozi wa vyama vya siasa, dini na asasi za kiraia na wananchi kushirikiana ili malengo ya Serikali yaweze kufikiwa kwa wakati,"amesema Katibu Mkuu huyo.

 NA  DIRAMAKINI

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments