Recent-Post

VYOMBO VYA HABARI VITUMIKE KUFIKISHA TAARIFA SAHIHI KWA WANANCHI JUU YA CHANJO YA UVIKO 19

Vyombo vya habari na wanahabari wametakiwa kuandika habari sahihi za chanjo ya UVIKO 19 ili jamii ifahamu ukweli wa umuhimu wa chanjo hiyo na ijitokeze kupata chanjo.

Hayo yamesemwa na Profesa Haroun Ngonyani toka Hospitali ya Jakaya Kikwete alipokuwa akiwasilisha mada kwenye kongamano la mtandaoni la vyombo vya habari na AZAKI lililoandaliwa na Klabu ya Waandishi wa Habari ya Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Taasisi ya Freedom House.

Profesa Nganyani alisema kuwa, kwenye mitandao ya kijamii kuna habari nyingi za uongo ambazo zinawatia hofu wananchi kwenye kujitokeza kupata chanjo ya UVIKO 19, hivyo vyombo vya habari visaidie kueleza wananchi ukweli juu ya umuhimu wa chanjo ya UVIKO 19.

Aliongeza kwa kusema kuwa, wananchi wanaviamini sana vyombo vya habari hivyo wao kama wataalamu wanaviomba vyombo vya habari kusaidia kufikisha taarifa sahihi kwa wananchi.

Nae Afisa Habari wa Taasisi ya Freedom House Lina Muro alisema kuwa, kuna uhitaji mkubwa wa elimu toka kwa wataalamu ili kundi la waandishi wa habari na AZAKI wapate elimu ya kutosha juu ya umuhimu wa chanjo.

Pia aliwashukuru wataalamu hao kwa kujitokeza kwenye mijadala kama hiyo kwa kuwa inaleta tija kwa jamii.

Makamu Mwenyekiti wa Klabu ya waandishi wa habari ya Mkoa wa Mwanza Alex Mchomvu aliwashukuru waandaaji na washiriki wote na kusema majadiliano hayo ni fursa kwao na hivyo wayatumie vizuri ili jamii iweze  kunufaika.

Mshiriki wa Mafunzo hayo Tony Alphonce alisema kuwa, elimu aliyoipata itamsaidia kuandika habari za UVIKO 19 kwa usahihi zaidi.

Majadiliano hayo ya kimtandao yaliandaliwa na klabu ya waandishi wa habari ya Mkoa wa Mwanza kwa kushirikiana na Taasisi ya Freedom House na kufanyika kwa njia ya kimtandao na mada mbalimbali ziliwasikishwa na kufuatiwa na majadiliano.
Na Judith Alex  - Mwanza

Post a Comment

0 Comments