Recent-Post

Wabunge wacharuka kuhusu machinga

Dodoma. Sakata la kuhamishwa wafanyabiashara ndogondogo maarufu machinga leo limeendelea kuwaibua wabunge wakihoji namna kundi hilo linavyozungushwa.

Baadhi ya wabunge wamehoji elimu za wataalamu wanaotoa mapendekezo ya wapi wapelekwe, kwamba vyuo vikuu walisoma kumwagia maua.

Sakata la machinga lilianza mapema kwenye maswali ya wabunge ambapo Mbunge wa Viti maalumu, Halima Mdee aliibua jambo hilo.

Mdee alihoji ni kwa nini mapendekezo ya mwongozo wa mpango wa Serikali hayakujumuisha namna ya kuwasaidia wamachinga.

Katika uchangiaji, kwa nyakati tofauti wabunge Joseph Kasheku 'Msukuma' na Ahmed Shabiby walizungumzia umuhimu wa kundi la machinga hata katika uchumi wa nchi.

Msukuma alisema kwa sasa maisha ya Watanzania yangekuwa magumu kutokana na mzunguko wa fedha ambao kwa sehemu kubwa ulitegemea wamachinga.

Kwa mujibu wa Msukuma, Serikali inatakiwa kuwa makini katika suala hilo vinginevyo wanakwenda kuharibu uchumi wa wengi.

Kwa upande wake mbunge wa Gairo, Ahmed Shabiby amesema kitendo cha kuwaondoa machinga katikati ya mji ni kutaka wafirisike na maisha yao kuwa magumu.

Shabiby amependekeza uwekwe Mpango maalumu wa kuwaacha machinga katikati ya mji na wawekewe mazingira rafiki.

Ametolea mfano kwa Jiji la Dar es Salaam kwamba wapangwe vizuri katika majengo ya Shirika la nyumba mitaa ya Msimbazi ambako wanaweza kulipa kodi zaidi ya wapangaji waliopo sasa.

Post a Comment

0 Comments