Wadau wa elimu wataka miongozo waliojifungua kurejea shuleni

Mkurugenzi Mtendaji HakiElimu, Dk John Kalage akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uwamuzi wa Serikali kuruhusu watoto walioacha Shule kwa sababu ya ujauzito kurudi shuleni katika mfumo rasmi, kulia ni Meneja fedha na Utawala, Peter Letema.Picha na Michael Matemanga

Siku chache baada ya Serikali kutoa waraka wa kuruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni kwa mfumo rasmi baada ya kujifungua, wadau wa elimu wameeleza kuwa utekelezaji wa hilo unahitaji miongozo.

Wamesema miongozo maalumu itamuwezesha mtoto wa kike kurudi shuleni baada ya kujifungua itakayoeleza hatua kwa hatua ya namna ambavyo hilo linaweza kutekelezeka.

Jumatano Novemba 24, 2021 na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Ndalichako alitangaza na kutoa waraka wa Serikali kuwaruhusu wanafunzi waliokatisha masomo kutokana na sababu mbalimbali ikiwemo ujauzito kurejea shuleni kwa mfumo rasmi baada ya kujifungua.

Leo Ijumaa, Mkurugenzi wa Taasisi ya Hakielimu, John Kalage amesema kuwa pamoja na Serikali kutangaza na kutoa waraka unatoa maelekezo ya kumruhusu mtoto wa kike kurudi shuleni waraka huo haujitoshelezi.

“Waraka huu haujitoshelezi katika vipengele vya hatua gani zichukuliwe ili mtoto huyu arudi shuleni bila kubaguliwa, akijiamini pamoja na kulinda haki ya mtoto aliyezaliwa ya kupata malezi ya mama.

Lazima kuwepo mwongozo utakaoonyesha huyu mtoto anayerudi shule anarudi vipi, mtoto wake anamuachaje anapata vipi nafasi ya kumhudumia na kumnyonyesha,”amesema Kalage.

Mkurugenzi huyo ameweka wazi kuwa ni vyema miongozo hiyo ikaandaliwa na kuanza kutumika mapema ili kutoa fursa ya mtoto wa kike aliyeacha shule kati ya mwaka 2019 na 2020 aweze kurudi shuleni katika mwaka wa masomo 2022.

Sanjari na miongozo Kalage amesema uamuzi huo wa kuwarudisha shuleni watoto wa kike waliojifungua unapaswa pia kuwekwa kwenye sera, sheria na mwongo wa sheria ya elimu unaohusu ufukuzaji na usimamishaji masomo wa watoto walioko shuleni wa mwaka 2022.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments