WADAU WATOA OMBI KWA WIZARA,KAMPUNI ZA SIMU KUANGALIA NAMNA YA KUPUNGUZA BEI KUBWA KATIKA VIFURUSHI VYA DATA

Wasema imekuwa mwiba wa maendeleo ya kidigitali Tanzania, waeleza  sekta ya habari ilivyoathirika

WADAU wa sekta ya habari na hasa waliojikita katika kutoa  huduma za maudhui katika Tovuti, programu tumishi, mtandao wa YouTube na blogs wamelalamika kupungua kwa kasi kwa watumiaji wa huduma zao huku wakiiomba wizara na wadau husika kujadili na kulipatia mwarobaini suala hili.

Kupungua kwa watumiaji hao kunatokana na kupanda maradufu kwa bei za vifurushi vya interneti nchini, huku GB 1 ya Data ikipatikana kwa zaidi ya dola 1.3 ambapo kumesababisha kupungua kwa kasi idadi ya watumiaji wa internet nchini, hivyo kuathiri taasisi, mashirika na watumiaji binafsi wa interneti ambao hutumia huduma hiyo katika majukumu mbalimbali pamoja na burudani.

Taarifa iliyoandaliwa na baadhi ya watoa maudhui, waandishi wa habari za mtandaoni na watumiaji wa mitandao Tanzania wamesema  kutokana na bei hizo kutokuwa rafiki kwa watumiaji wa huduma hiyo hasa mwananchi wa kawaida Taasisi na tasnia mbalimbali zimetajwa kuathirika kwa namna moja au nyingine.

Wamesema  kuwa ili  kuendesha mitandao ya kijamii inatakiwa kutumia bando kila wakati ili kuendelea kuuhabarisha umma kuhusu habari na matukio mbalimbali hivyo gharama kubwa za vifurushi zimekuwa kikwazo kwa bloggers & youtubers.

Kwa upande wa Wasanii na watoaji maudhui  ya burudani hasa kwa mtandao wa video wa YouTube nao wamedai idadi ya wanaofuatilia kazi zao kushuka kwa kasi kwa siku za karibuni, jambo ambalo wamedai kuathiri sana kipato chao. Vilevile mitandao mbalimbali ya takwimu inaonesha kushuka kwa watumiaji wa mtandao wa YouTube Tanzania kwa siku za karibuni.

Wakati kwa watumiaji binafsi wa internet nchini Tanzania nao wameonesha kukerwa na kupanda mara kwa mara kwa bei za vifurushi tena vinapandishwa kimya kimya licha ya mamlaka kusema gharama zimeshuka huku wakidai uishaji wa haraka kuliko kawaida wa vifurushi hivyo, vile vile  wanakumbusha ahadi za wadau na wizara kuahidi mara kadhaa kulishughulikia tatizo hilo na kubakia ahadi hewa.

Pamoja na hayo, bei hizi ambazo zimetajwa kutokuwa rafiki kwa watumiaji  huenda zikazidi kuathiri  mfumo mzima wa maendeleo ya kidigitali hasa kwa mashirika, taasisi, na makampuni kama vile huduma za kibenki za kidigitali, huduma za afya, elimu, na dini zinazopatikana kwa njia za kidigitali pamoja na tasnia ya michezo ya bahati nasibu ya mtandaoni.

Pamoja na hayo wamedai hali hiyo imeathiri haki ya  kupata taarifa huku wakifafanua kila mtu ana haki ya kupata taarifa, kwa miaka ya karibuni kutokana na ukuaji wa maendeleo ya teknolojia ya habari na mawasiliano hata Serikali imekuwa ikitoa taarifa zake kwa idara mbalimbali kwenda kwa wananchi kwa njia ya mitandao.

Hiyo inahusisha hata Matangazo ya moja kwa moja ya Uapisho wa viongozi, uzinduzi wa miradi na hotuba za viongozi kwa wananchi ambao wapo maeneo tofauti tofauti. Kwa mujibu wa wadau hao wamesema hapo awali ilikuwa rahisi mtu kufatilia mubashara matangazo ya matukio ya kitaifa kupitia mtandaoni.

Lakini  hivi sasa wananchi wengi wanapata shida kuangalia hadi mwisho matangazo hayo kwani maranyingi kabla tukio halijaisha kifurushi cha data kinakuwa kimeshaisha, hivyo athari hizi si tu kwetu wananchi ila hata kwa watoa taarifa wakiwemo viongozi wa Serikali.

Na hivyo ujumbe uliokusudiwa kuwasilishwa kwetu wananchi unakuwa umekwamishwa na gharama za vifurushi vya data.

Kutokana na hali hiyo wadau mbalimbali wanaishauri  wizara husika, pamoja na kampuni za simu nchini yanayotoa huduma hiyo muhimu kwa maendeleo kuangalia upya na kwa umakini jambo hili kwa maendeleo na tija ya nchi.

Wamesema wanafahamu Vifurushi vya Data ni Ofa za kampuni ya simu katika kufanya ushindani wa kibiashara, lakini licha ya ofa basi wanashauri ziwe zenye kuleta unafuu kwa mwananchi kwani kukiwa na huduma hizo nzuri, hata matumizi ya mawasiliano kwa njia ya simu yataongezeka na kutaongeza mapato kwa Serikali kwa njia ya kodi na tozo zilizopo hivi sasa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments