Recent-Post

WAMACHINGA KIGAMBONI WAIPONGEZA CCM, WATOA KILIO CHAO KWA RAIS SAMIA..WASEMA WAMETIWA UMASIKINI

WAFANYABIASHARA katika Wilaya ya Kigamboni na hasa wanaofanya biashara zao katika Stendi mpya ya Feri Kigamboni na maeneo ya Chuo  cha Kumbukumbuku ya Mwalimu Nyerere wamekipongeza Chama Cha Mapinduzi kwa kuona changamoto wanayopitia wafanyabiashara wadogowadogo  tangu kuansa bomoa bomoa ya maeneo ya biashara.

CCM kupitia Katibu wa Itikadi na Uenezi wa Shaka Hamdu Shaka kimesema kuna baadhi ya Wilaya na mikoa wameendesha mchakato huo bila kufuata maelekezo yaliyotolewa na matokeo yake kusababisha malalamiko kila kona,hivyo kikataka mchakato huo lazima uwe umeshirikisha wafanyabiashara na si vinginevyo.

Wakizungumza leo na waandishi wa vyombo vya habari wafanyabiashara waliokuwa maeneo ya Stendi Mpya Feri Kigamboni wamesema wanaipongeza CCM kwa tamko ambalo wamelitoa kwa ajili ya wamachinga na kwamba pamoja na tamko hilo wamesema kuna haja ha mchakato huo kuwa shirikishi ,kwani wamebomolewa vibanda vyao vya biashara bila kushirikishwa.

Wamefafanua Oktoba 28 mwaka huu saa nane usiku askari wa Jiji la Dar es Salaam walivamia maeneo yao na kuanza kubokoa vibanda vya wafanyabiashara wakati wahusika wakiwa majumbani.Mbali ya kubomoa bidhaa na mali zao zilizokuwa katika mabanda yamechukuliwa, hivyo wengi wao wametiwa umasikini mkubwa na Serikali wanayoimini na kuwa kimbilio lao la wakati wote,hivyo wanamuomba Rais Samia Suluhu Hassan kuwaangalia kwa jicho la huruma.

Akizungumza kwa niaba ya wafanyabiashara hao Jamilla Hussein ambaye naye ni mfanyabiashara amesema usiku wa Oktoba 28 mwaka huu umeacha majonzi na masikitiko makubwa kwa familia za wafanyabiashara ndogondogo wilayani Kigamboni, wamebolewa vibanda vyao na mali zao kuchukuliwa.

"Banda langu pamoja na mabanda mengine mali zetu zimechukuliwa, wamekuja usiku wamevunja, wameshindwa kutushirikisha na hakuna kiongozi kutoka ofis ya Wilaya alyekuja kuzungumza nasi ,hakuna wa kututetea.Katika maeneo ambayo mabanda yetu yamewekwa tulipangwa na hata aliyekuwa Rais wetu Hayati Magufuli enzi za uhai wake alipokuja huku Kigamboni alifurahishwa na jinsi tulivyojipanga na kufanya biashara zetu.

"Mabanda yetu yako mbali na barabara,yako mbali na waenda kwa miguu, na wala hakuna tunayemsumbua, eneo ambalo tulikuwa tunafanyabiashara ni hili la Bandari hapa Kigamboni, leo wameboa na wanatuambia twende kwa Urasa, Banda la Mkaa na Vilabu vya Pombe ambako kwanza hakuna biashara na kibaya zaidi hakuna miundombinu yoyote, tunamuomba Rais Samia atusaidie,"amesema.

Amefafanua kuwa wafanyabiashara wa Feri Kigamboni wateja wanaowategemea ni watu wanaovuka na vivuko na wanafunzo, hivyo maeneo ambayo wamepelekwa ni sawa na kuua mitaji yao na kuwatia umasikini."Kigamboni sio Kariakoo,ni Wilaya Changa na itaendelezwa na wananchi wenyewe, tumewachagua viongozi mtutetee na sio kutuone na kutuona kama wakimbizi."

Kwa upande wake Mwenyekiti wa  Machinga, wilayani Kigamboni, Mengi Kajato, amesema wanakishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kutoa tamko la kuwapanga bila kuwanyanyasa wamachinga na kwamba wamba wafanyabiashara wa Kigamboni na hasa wa eneo la Stendi mpya na Mwalimu Nyerere wamesikitishwa kwa jinsi walivyofanyiwa,mabanda yamebolewa usiku.

"Baada ya kauli ya jana iliyotolewa na Shaka imetufariji sana wafanyabiashara ndogondogo Kigamboni.Maeneo ambayo tumepangiwa hayana miundombinu yoyote, lakini wengi wamepoteza mali ,wengine wamerudisha mali nyumbani.Eneo ambalo tulikuwa tunafanyabiashara hatujagusa lami wala mtaro, tulikuwa tumejipanga vizuri lakini tunasema na tunaomba viongozi watusikie kilichofanyika Kigamboni ni tofauti na maelekezo,"amesema.

Ameongeza kwamba Rais Samia Suluhu Hasan nia yake ni nzuri na hakuna mfanyabiashara anayepinga kupangwa lakini utaratibu ambao umetumika ndio unaolalamikiwa, hawakushirikishwa zaidi ya kubomolewa vibanda vyao."Sisi ndio wafanyabiashara na tunaposhauri tunajua,leo tunaambiwa twende Kwa Urasa kule hakuna biashara.Nia ya Rais nzuri lakini utekelezaji wake umekuwa tofauti."

Amesisitiza ni vema viongozi na wafanyabiashara wakaa mezani kujadiliana na kwamba wao sio wanyama."Sisi sio wanyama ni binadamu, kuna maisha baada ya uongozi, kuna maisha baada ya Ukuu wa Wilaya,Ukuu wa Mkoa,pia kuna maisha baada ya Urais.

"Tutangulize ubinadamu na kumuogopa Mungu.Wafanyabiashara tuna imani kubwa na Rais Samia na CCM, tunaamini katika hili watakuwa upande wetu.Kuwa Mmachinga sio dhambi, tumeamua kujiajiri kupitia biashara ndogondogo."

Mwenyekiti wa Machinga, wilayani Kigamboni, Mengi Kajato(aliyevaa kofia), akizungumza na waandishi wa habari, Dar es Salaam, wakati akikishukuru Chama Cha Mapinduzi kwa kutoa tamko la kuwapanga bila kuwanyanyasa wamachinga. Na Said Mwishehe,Michuzi TV

Post a Comment

0 Comments