Recent-Post

Wanawake Kata ya Arri, Babati Vijijini wamfagilia Rais Samia,wamshukuru kwa fursa ya umeme

 Rais Samia Suluhu Hassan ni mchapakazi, mpambanaji, mama ambaye ni mfano wa kuigwa, anayetujali akina mama na wananchi kwa ujumla;

Diwani mstaafu wa Viti Maalum, Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini mkoani Manyara, Elizabeth Seroneda akizungumza na wafanyakazi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA), Mhandisi Gilbert Furia (kulia) na Julian Kiiza (kushoto) hivi karibuni. Eizabeth anamiliki mashine ya kusaga nafaka inayohudumia wananchi wa kijiji na Kata ya Arri. Kijiji hicho kimenufaika na miradi ya umeme vijijini. (Picha na Veronica Simba-REA).

Hayo ni maneno ya Diwani mstaafu wa Viti Maalum, Halmashauri ya Wilaya ya Babati Vijijini mkoani Manyara, Elizabeth Seroneda wakati akizungumza na Mwandishi wa Habari hizi hivi karibuni, kwa niaba ya wananchi hususani wanawake wakazi wa Kata ya Arri, kuhusu manufaa ya umeme vijijini.

Diwani huyo mstaafu anaunganisha sifa hizo kwa Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Samia Suluhu Hassan na manufaa wanayoyapata wananchi wa Arri kutokana na umeme kufika katika kata hiyo.

Mama Seroneda anasema kuwa, awali wananchi katika kata hiyo walikuwa wakihangaika sana hususani katika kupata huduma ya kusaga nafaka ambapo walilazimika kusafiri kwa baiskeli au pikipiki, umbali wa kilomita takribani tano kufuata huduma hiyo katika eneo linalofahamika kama Kijiweni.

Anaeleza zaidi kuwa, hivi sasa hali imebadilika, kwani baada ya umeme kufika katika kata hiyo, wananchi wametumia fursa hiyo adhimu kufungua biashara mbalimbali ikiwemo mashine ya kusaga nafaka, saluni za kunyoa nywele na hata wapangaji wameongezeka katika nyumba na majengo yanayopangishwa.

“Kwa mfano hiyo nyumba ya tatu kutoka hapa ni ya kwangu, awali ilikuwa imepoa sana,lakini hivi sasa wapangaji wanapambania, kila mmoja anataka aweke biashara. Hii yote ni kutokana na uwepo wa umeme,” anasema Mama Seroneda.

Kutokana na kazi nzuri inayofanywa na Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA) ya kusambaza umeme vijijini, Diwani mstaafu Elizabeth amesema, wananchi wa Arri wanampongeza Rais Samia na kwamba wanajivunia utendaji kazi wake mahiri na wanamuombea afya njema.

“Mungu amtie nguvu, aendelee kututetea. Sisi wananchi tuko pamoja naye sana,” anasisitiza Mama Seroneda.

Ametumia nafasi hiyo kwa niaba ya wanawake wenzake kutoa rai kwa kila Mtanzania aweke nia ya kumsaidia Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan siyo kwa ajili yake bali kwa maslahi ya nchi na ya kila mmoja.

"Mama yetu. Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan anafanya kazi kubwa na nzuri, ili aweze kutekeleza majukumu yake kwa ufanisi, tunapaswa kwa umoja wetu wanawake wote nchini na Watanzania tumuunge mkono yeye (Rais) na wasaidizi wake. Mfano tunaona namna ambavyo wasaidizi wake kutoka REA wanafanya kazi kwa bidii kuhakikisha tunapata nishati ya uhakika huku vijijini, ni jukumu letu kuwaunga mkono na kuwaombea kwa Mungu pia ili kila wanalolifanya kwa maslahi ya Taifa liwe na tija kubwa zaidi,"ameongeza.
NA VERONICA SIMBA, BABATI

Post a Comment

0 Comments