Recent-Post

Waziri Mkuu:Rais Samia ana matumaini na Taifa Stars

 NA MWANDISHI MAALUM


WAZIRI MKUU Kassim Majaliwa amesema Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan ana matumaini makubwa na Timu ya Taifa ya Mpira wa Miguu ya Tanzania (Taifa Stars) na anaamini itafanya vizuri na kufuzu kushiriki kombe la Dunia litakalofanyika nchini Qatar 2022.
Waziri Mkuu, Kassim Majaliwa akimsikiliza Kapteni wa timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa Miguu (Taifa Stars) John Bocco kwenye ukumbi wa hoteli ya Golden Tulip jjjini Dar es salaam Novemba 5, 2021 alikokwenda kutoa hamasa kwa timu hiyo kuelekea mechi za kufuzu kombe la dunia dhidi ya timu ya Taifa ya Congo na Madagascar, Novemba 5, 2021 (Picha na Ofisi ya Waziri Mkuu).

Ametoa kauli hiyo Novemba 5, 2021 wakati alipozungumza na wachezaji wa Timu ya Taifa ya Soka ya Tanzania, (Taifa Stars) katika Hoteli ya Golden Tulip, Jijini Dar es Salaam ambapo timu hiyo imeweka kambi ili kujiandaa na michezo ya awali ya kufuzu kombe la Dunia dhidi ya Timu ya Taifa ya DR Congo na Madagascar.

Waziri Mkuu amesema Serikali kupitia Wizara ya Michezo na Shirikisho la Mpira wa Miguu Tanzania (TFF) wataendelea kuisimamia na kufuatilia maendeleo ya timu hiyo ya Taifa hadi hatua ya mwisho na kuhakikisha timu hiyo inafanya vizuri.

“Mheshimiwa Rais ana matumaini makubwa na nyinyi na anawatakia kila la kheri katika maandalizi yenu, Ni matumaini yake kuwa mtafanya vyema na kufuzu hatua ya kumi bora na hatimaye kupata nafasi kuwa miongoni mwa timu tano zitakazo shiriki kombe la Dunia kutoka Afrika.
 Waziri Mkuu amewasihi wachezaji wa timu ya Taifa kujitoa na kufanya mazoezi kwa bidii, pamoja na kuzingatia maelekezo wa Mwalimu na wataalam wa benchi la ufundi ili kuhakikisha Ushindi unapatikana.

“Viongozi wa kamati ya Hamasa ya Taifa Stars kwa kushirikiana na TFF hakikisheni mnaisimamia timu vyema, Wachezaji wale vizuri na wafanye mazoezi na wapewe kila kinachohitajika ili kujihakikishia tunapata ushindi.”

Akizungumza kwa niaba ya wachezaji wenzake, Nahodha wa Taifa Stars John Bocco ameahidi kuwa watajitoa kwa nguvu zote ili kuhakikisha wanapata ushindi katika mechi zote zilizobaki.

Kikao hicho kilihudhuriwa na viongozi kutoka TFF wakiongozwa na Katibu Mkuu wa Shirikisho hilo Wilfred Kidau, Viongozi wa Baraza la Michezo Tanzania BMT, Mwenyekiti wa kamati ya Hamasa ya Taifa Stars, Ghalib Mohamed na Makamu Mwenyekiti Salim Abdala “Try Again” na Katibu wa Kamati hiyo Hersi Said.
Waziri Mkuu Kassim Majaliwa akizungumza na wachezaji wa timu ya Taifa ya Tanzania ya mpira wa Miguu (Taifa Stars) ikiwa ni sehemu ya hamasa kuelekea mechi za kufuzu kombe la dunia dhidi ya timu ya Taifa ya Congo na Madagascar, Novemba 5, 2021 katika ukumbi wa Hotel ya Golden Tulip jijini Dar es Salaam.

Post a Comment

0 Comments