WIZARA YA NISHATI YAJIVUNIA MIAKA 60 YA UHURU KUONGEZEKA KWA KUZALISHA UMEME NCHINI

Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara  ya Nishati Mhandisi Felichesmi Mramba,akitoa taarifa ya wizara ya Nishati kwa kwa niaba ya Waziri wa Nishati,Januari Makamba kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru leo November 9,2021 jijini Dodoma

 

Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali wakifatilia hotuba ya Waziri wa Nishati Januari Makamba iliyowasilishwa na Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara  hiyo  Mhandisi Felichesmi Mramba kuhusu mafanikio yaliyopatika kwa kipindi cha miaka 60 ya Uhuru leo November 9,2021 jijini Dodoma

…………………………………………………………..

Na.Alex Sonna,Dodoma

KATIKA kuelekea maadhimisho ya miaka 60 ya uhuru Wizara ya Nishati imetaja  mafanikio yaliyopatikana katika sekta ya umeme na nishati jadidifu ni  kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme nchini ambapo hadi kufikia  septemba 2021 upatikanaji wa umeme umefikia Megawati 1,609.91 ikilinganishwa na Megawati 17.5 kabla ya uhuru.

Akizungumza leo Novemba 9,2021 jijini Dodoma Kaimu Katibu Mkuu wa Wizara  ya Nishati Mhandisi  Felichesmi Mramba kwa niaba ya Waziri wa Nishati,Januari Makamba  kuhusu mafanikio na maendeleo ya sekta hiyo katika kipindi cha miaka 60.

KUONGEZEKA KWA UZALISHAJI WA UMEME
Mramba amesema katika  kipindi cha miaka 60 ya uhuru wa Tanzania Bara mafanikio yaliyopatikana katika Sekta ya Umeme na Nishati Jadidifu ni pamoja na kuongezeka kwa uzalishaji wa umeme nchini ambapo hadi kufikia mwezi Septemba, 2021 upatikanaji wa umeme umefikia MW 1,609.91 ikilinganishwa na MW 17.5 kabla ya Uhuru. 

Amesema ,uwezo wa mitambo ya kufua umeme iliyoungwa katika mfumo wa Gridi ya Taifa umefikia MW 1,573.65 ambapo umeme wa nguvu ya maji (36.46%); gesi asilia 57.28(%); Mafuta (5.60%); na Tungamotaka (Biomass) (0.67%) na kwamba uwezo wa mitambo hiyo unajumuisha mitambo inayomilikiwa na TANESCO ambayo huchangia (86.57%) na mitambo ya wazalishaji binafsi (IPPs/SPPs) ambayo huchangia (13.43%). 

“Uwezo wa mitambo ya kuzalisha umeme iliyopo nje ya Gridi ya Taifa (off-grid) ni MW 36.26 ambapo TANESCO inamiliki mitambo yenye MW 31.26 na mzalishaji binafsi NextGen Solawazi (Kigoma) MW 5 kwa kutumia nguvu ya jua,ukamilika kwa mitambo wa kuzalisha umeme kwa nguvu ya maji ya: Hale MW 21 (mwaka 1964).

“Na kwa  njia ya kusafirisha umeme ya msongo wa kV 11 kutoka hale hadi Dar es salaam; Nyumba ya Mungu MW 8 (mwaka 1969) na njia ya umeme ya msongo wa kV 66 Kutoka nyumba ya Mungu hadi Arusha; Kidatu MW 240 (mwaka 1975- 1981); Mtera MW 80 (mwaka 1988); New Pangani Falls MW 68 (mwaka 1995); na kihansi wa MW 180 (mwaka 2000),”Alifafanua.

Amesema kukamilika kwa ujenzi wa mitambo ya kufua umeme kwa kutumia gesi asili ya  Songas MW 189 (mwaka 2004) Ubungo I MW 102 (mwaka 2008), Ubungo II MW 105 (mwaka 2012), Tegeta MW 45 (mwaka 2009), Somanga Fungu MW 7.5 (mwaka 2010), Kinyerezi I MW 150 (mwaka 2016) na ujenzi wa njia za umeme wa kV 220 (Kinyerezi – Kimara) na kV 132 (Kinyerezi – Gongolamboto); Nyakato MW 63 (mwaka 2013), Kinyerezi II MW 248 (mwaka 2018) na Mtwara gas power plant MW 22 (mwaka 2019). 

Amesema   kukamilika kwa ujenzi wa njia za kusafirisha umeme za kV 66 yenye urefu wa Kilomita 125 kutoka Mbala, Zambia hadi Sumbawanga (mwaka 2001) kV 220 kutoka Singida na Arusha (mwaka 1996) km 300, kV 132 kutoka Ubungo-Makumbusho (mwaka 2010) kilomita 7; kV 132 yenye urefu wa kilomita 80 kutoka Mtwara hadi Mahumbika (Lindi).

“Pamoja na vituo vya kupoza umeme vya Mtwara na Mahumbika, kV 400 kutoka Iringa hadi Shinyanga kupitia Dodoma na Singida km 670 (mwaka 2016), kV 220 kutoka Makambako hadi Songea km 250 pamoja na ujenzi wa vituo vitatu (3) vya kupoza umeme vya Makambako, Madaba na Songea (mwaka 2018); na kV 220 Bulyanhuku Geita km 55 (mwaka 2020).

VITUO VIPYA VYA KUBORESHA UPATIKANAJI WA UMEME 

Ameyataja  mafanikio mengine yaliyopatikana ndani ya miaka 60 ya uhuru ni  kukamilika kwa ujenzi wa vituo vipya vya kupoza umeme kwa ajili ya kuboresha upatikanaji na umeme vya Mbagala, Kipawa, Gongolamboto na Mburahati Mkoani Dar es Salaam, vituo vya kupoza umeme vya Njiro B, Mount Meru, Sakina, Unga Ltd, Kiltex na Themi Mkoani Arusha.

Mramba amevitaja vituo vingine ni   vya kupoza umeme vya Bomambuzi na Trade School Mkoani Kilimanjaro; ukarabati wa vituo vya kupoza umeme vya Mikocheni, Oysterbay, City Centre, Gongolamboto, Kariakoo, Mbagala, Chang’ombe, Kipawa na Ubungo Mkoani Dar es Salaam. 

“Kukamilika kwa ujenzi wa njia za msongo wa kV 33, kV 11 na kV 0.4 kwa ajili ya kusambaza umeme katika Mikoa ya Dodoma, Iringa, Manyara, Mbeya, Morogoro, Mwanza, Njombe na Tanga kwa ufadhili wa Millenium Challenge Corporation (MCC).

Kukamilika kwa mradi wa kusambaza umeme wa Electricity V (2015) katika Wilaya za Bukombe, Kwimba, Magu, Mbogwe, Misungwi na Sengerema. Mradi huo ulihusu ujenzi wa njia ya kusambaza umeme wa Msongo wa kV 33, kufunga transfoma na kuwaunganishia umeme wateja 8,600,”amesema.

SEKTA YA MAFUTA NA GESI 

Amesema kabla ya uhuru biashara ya mafuta ilianza maeneo ya mwambao wakati  Smith MacKenzie alipoanza kuingiza mafuta kwenye visiwa vya Zanzibar kama wakala wa Kampuni ya Shell.

Amesema Kampuni hiyo ilipanua shughuli zake hadi maeneo ya Tanzania Bara na pia ilijihusisha na utafutaji wa mafuta hadi mwaka 1964.

“Mwaka 1966, Serikali kwa kushirikiana na kampuni ya Agip iliunda kampuni ya Tanzania and Italian Petroleum Refinery (TIPER) ambayo ilihusika na kuagiza, kusafisha na kuuza mafuta kwa kampuni za usambazaji,”amesema.

Amesema  kiasi cha mafuta kilichokuwa kinasafishwa na kampuni hiyo hakikukidhi mahitaji kutokana na sababu hiyo, mwaka 1969 Serikali ilianzisha Shirika la Maendeleo ya Petroli nchini (TPDC).

Amesema TPDC pia ilikuwa na jukumu la kusimamia shughuli za utafiti wa awali na utafutaji mafuta kwa kushirikiana na kampuni nyingine chini ya mikataba ya Production Sharing Agreement (PSA). 

Amesema Serikali ilitoa leseni ya utafutaji wa mafuta ya petroli kwa Kampuni ya AGIP katika eneo la mwambao wa bahari ya Hindi kutoka Mtwara hadi Tanga.

“Shughuli za utafutaji wa mafuta zilianza rasmi mwaka 1973 na kampuni hiyo ikagundua gesi asilia katika eneo la Songo Songo mwaka 1974. Kwa kuwa lengo lilikuwa ni kupata mafuta, AGIP ilirudisha eneo hilo kwa Serikali mwaka 1975 na kuendelea na utafutaji wa mafuta. 

“Wakati AGIP ikiendelea na juhudi za utafutaji mafuta, TPDC ilianza rasmi shughuli za uagizaji mafuta ghafi mwaka 1977,Mwaka 1980, Sheria ya Utafutaji na Uendelezaji wa Mafuta (Petroleum Exploration and Production Act, 1980) ilitungwa ili kuwezesha mikakati ya Serikali ya kuhamasisha ushiriki wa kampuni za kimataifa,”amesema.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments