2021: Mwaka wa ahueni vigogo waliosota mahabusu

Miongoni mwa mambo yaliyoacha kumbukumbu kubwa katika eneo la utoaji haki mwaka 2021 ni kufutwa kwa kesi nyingi za jinai, hasa zilizoteka hisia za watu wengi.

Kwa wachache waliokuwa na bahati, kesi zao zilisikilizwa wakiwa nje kwa dhamana. Walioshtakiwa kwa makosa yasiyodhaminika walijikuta wakisota mahabusu kwa miaka kadhaa hadi pale Mkurugenzi wa Mashtaka (DPP) au Mahakama walipoamua kuachana nazo kwa mamlaka waliyopewa na sheria.

Mwaka huu, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka inayohusika na ufunguaji na uendeshaji wa mashauri, hasa ya jinai, ilitoa taarifa ya kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka (nolle prosequi) dhidi ya watu wengi waliokaa mahabusu zaidi ya mwaka kupitia DPP.

Kifungu cha 91(1) cha Sheria ya Mwenendo wa Makosa ya Jinai (CPA) kimempa DPP mamlaka ya kufuta kesi yoyote ya jinai, wakati na katika hatua yoyote, kabla ya kutolewa uamuzi.

Anapotumia kifungu hicho, DPP halazimiki kubainisha sababu wala hawezi kuhojiwa na mtu au mamlaka yoyote.

Mamlaka nyingine iliyofuta kesi nyingi mwaka huu ni Mahakama chini ya kifungu cha 225 cha CPA. Kifungu hiki kimeipa mahakama mamlaka ya kufuta kesi pale inapokaa mahakamani kwa muda mrefu bila upande wa mashtaka kuwasilisha ushahidi.

Zifuatazo ni miongoni mwa kesi maarufu zilizomalizwa na DPP au Mahakama bila kusikilizwa hadi mwisho na kutolewa hukumu.


Masheikh wa Uamsho

Hii ni kesi ya ugaidi iliyokuwa ikiwakabili viongozi wa Jumuiya za Uamsho na Mihadhara ya Kiislamu Zanzibar (Jumiki) waliokaa gerezani kwa miaka saba kabla ya kuachiwa huru kuanzia Juni 15, 2021.

Sheikh Farid Hadi Ahmed na wenzake 35 waliachiwa huru baada ya DPP kuwafutia mashtaka ya ugaidi yaliyokuwa yakiwakabili.

Kesi hii ilivuta hisia za watu wengi huku wanaharakati wakipaza sauti kutaka waachiwe baada ya kukaa mahabusu muda mrefu bila kesi yao kusikilizwa.

Mara kadhaa Serikali ilikuwa ikieleza kesi hiyo ilichelewa kusikilizwa kwa kuwa upelelezi ulihusisha kutafuta taarifa nje ya nchi.

Walishtakiwa kwa kujihusisha na makosa ya ugaidi kinyume na kifungu cha 27(c) cha Sheria ya Kuzuia Ugaidi ya 2002, wakidaiwa kutenda makosa hayo kati ya Januari 2013 na Juni 2014, Tanzania Bara na Zanzibar.

Katika hatua ambayo haikutarajiwa na wengi, Aprili 23, 2021 Mahakama Kuu iliwafutia mashtaka 14 baada ya kukubaliana na hoja za mawakili wao, Daimu Halfani, Juma Nassoro, Jeremiah Mtobesya na Abubakar Salum kuwa mahakama hiyo haina mamlaka ya kusikiliza mashtaka hayo kwa kuwa makosa wanayotuhumiwa yanadaiwa kutendeka Zanzibar.

DPP alikimbilia Mahakama ya Rufani kuupinga uamuzi huo, lakini wakati wa usikilizwaji wa rufaa hiyo mawakili wa washtakiwa hao waiibua pingamizi dhidi ya rufaa hiyo ya Serikali wakidai DPP hakuwa na mamlaka tena ya kukata rufaa chini ya kifungu cha 6 cha Sheria ya Mamlaka ya Rufani, kwani Mahakama Kuu ilishakiondoa kuwa kilikuwa kinakinzana na Ibara ya 13 (1) na (2) na ya 6(a) za Katiba.

Mei 18, 2021 majaji Stella Mugasha, Shaban Lila na Winfrida Korosso waliitupilia mbali rufaa ya Serikali. Mwezi mmoja baadaye (Juni 15, 2021) DPP aliwafutia wote mashtaka.

Siku iliyofuata, Juni 16, DPP Sylvester Mwakitalu alilieza Mwananchi kuwa aliamua kuwafutia mashtaka baada ya Mahakama Kuu kuwafutia mashataka 14 na Mahakama ya Rufani kutupilia mbali rufaa yake. Alisema ushahidi waliobakia nao ulikuwa hautoshi kuwatia hatiani.


Kesi ya Rugemalira

Hii ni kesi ya uhujumu uchumi iliyokuwa inamkabili mfanyabiashara James Rugemalira na wenzake iliyotokana na kashfa ya uchotwaji wa mabilioni ya pesa katika akaunti maalumu Tegeta Escrow iliyokuwa ndani ya Benki Kuu (BoT).

Akaunti hiyo ilifunguliwa kutokana na mgogoro wa malipo ya gharama za uwekezaji baina ya kampuni ya kuzalisha umeme ya Independet Power Tanzania Limited (IPTL) iliyomilikiwa na Rugemalira na Shirika la Umeme (Tanesco), lililopinga malipo hayo kuwa yalikuwa makubwa.

Hivyo, akaunti hiyo ilifunguliwa kwa pamoja na pande hizo mbili zilizokuwa na mkataba wa uzalishaji na kuuziana umeme ili fedha hizo zihifadhiwe humo kusubiri utatuzi wa mgogoro kuhusiana na kiasi ambacho Tanesco ilipaswa kuilipa IPTL.

Baada ya kukaa mahabusu kwa miaka minne na miezi mitatu, Septemba 16, mwaka huu DPP alimfutia Rugemalira mashtaka yaliyokuwa yakimkabili na akaachiwa huru.

Wakati kesi yao ikiendelea waliongezewa mashtaka mengine sita na mwanasheria na Katibu wa Kampuni ya IPTL, Joseph Makandege naye aliunganishwa katika kesi hiyo.

Walishtakiwa kwa kula njama, kuunda mtandao wa uhalifu na kujipatia Sh309 bilioni na Dola za Marekani 22,198,544.60 kati ya Novemba 28, 29 mwaka 2011 na Januari 23, 2014 wakiwa makao makuu ya benki ya Stanbic, Kinondoni na Benki ya Mkombozi, tawi la St Joseph.

Pesa nyingi zilidaiwa kuchukuliwa na Sethi na Rugemalira akachukuia kiasi kilichobaki, yakiwa malipo ya hisa zake asilimia 30 alizoiuzia kampuni ya PAP inayomilikiwa na Sethi.

Takribani miaka minne baada ya kuibuka kwa sakata hilo ndipo Rugemalira na mwenzake wakapandishwa kizimbani.

Rugemalira akiwa mahabusu alipambana kujinasua na kesi hiyo, ikiwa ni pamoja na kupaza sauti mara kadhaa mahakamani kutaka mahakama imwachie huru.

Hata hivyo, harakati zake liliishia kugonga mwamba miaka yote hadi Septemba 16 mwaka huu DPP alipoamua kumwondolea mashtaka.

Sethi alifanya makubaliano na DPP ya kukikiri kosa ili aachiwe. Aliamuriwa kulipa zaidi ya Sh26 bilioni kama fidia na faini na kuachiwa kwa masharti ya kukamilisha malipo hayo ndani ya miezi 12.


Kesi za uchochezi za Lissu

Makamu Mwenyekiti wa Chadema na aliyekuwa mgombea urais kupitia chama hicho katika Uchaguzi Mkuu wa 2020, Tundu Lissu ni mmoja wa watu waliopata ahueni ya kufutiwa kesi na DPP na mahakama.

Lissu alikuwa akikabiliwa na kesi tano za uchochezi katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, zilizodumu kwa takribani miaka mitano.

Kesi hizo zilifutwa na DPP na nyingine na Mahakama kwa nyakati tofauti kati ya Julai na Septemba, 2021.

Kesi mbili zilifutwa na DPP baada ya kueleza kutokuwa na nia ya kuendelea na mashtaka, huku nyingine tatu zikifutwa na mahakama baada ya kutoendelea kwa muda mrefu.


Aliyedaiwa kumteka Mo

Hii ni kesi iliyohusu tukio la kutekwa kwa Mkurugenzi wa Kampuni za Mohamed Enterprises Limited (MeTL) Group, Mohammed Dewji, maarufu kwa jina la Mo.

Mo alitekwa na watu wasiofahamika Oktoba 11, 2018 katika Hoteli ya Colloseum iliyopo eneo la Oysterbay, Dar es Salaam saa 11:35 alfajiri alipokwenda kwa ajili ya mazoezi kabla ya kutelekezwa na watekaji wake siku tisa baadaye katika viwanja vya Gymkhana.

Novemba 11, 2018, Jeshi la Polisi Kanda ya Dar es Salaam, lilitangaza kumshikilia dereva teksi, Mousa Twaleb kwa tuhuma za kushirikiana na watekaji kwa kuwaunganisha na madalali wa nyumba waliyopanga huko Mbezi Beach, ambamo ilidaiwa kuwa ndimo Mo alikuwa amefichwa.

Takribani miezi mitatu baadaye baada ya Rais John Magufuli (hayati) kuhoji ukimya wa sakata hilo, huku akitilia mashaka taarifa za Polisi (Machi 4, 2018), hatimaye Mei 28, 2019, Twaleb alipandishwa kizimbani katika Mahakama ya Kisutu kwa makosa mbalimbali, likiwemo la utakatishaji fedha ambalo halina dhamana.

Baada ya kukaa mahabusu kwa zaidi ya miaka miwili, hatimaye Julai 26, mwaka huu, DPP aliamua kuachana na mashtaka dhidi ya Twaleb, huku upelelezi wa kesi hiyo ukiwa haujakamilika.

 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments