Recent-Post

38 waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka.


  • 38 waaga dunia baada ya mgodi wa dhahabu kuporomoka Sudan

Makumi ya watu wamefariki dunia baada ya kuporomokewa na udongo kwenye mgodi wa dhahabu nchini Sudan.

Vyombo vya habari nchini humo vimeripoti kuwa, kwa akali watu 38 wamepoteza maisha baada ya kuporomokewa na mgodi huo wa dhahabu wa Darsay katika kijiji cha Fuja, mkoani Kordofan Magharibi, katikati mwa nchi.

Habari zaidi zinasema kuwa, mbali na watu 38 kuaga dunia kwenye ajali hiyo ya jana Jumanne, wengine zaidi ya wanane wamejeruhiwa na wanatibiwa katika hospitali iliyoko karibu na eneo la tukio.

Inaarifiwa kuwa, mgodi huo ulikuwa umesitisha shughuli zake kwa muda sasa, na kwamba uchimbaji wa madini ya dhahabu uliokuwa ukiendelea katika timbo hilo ulikuwa unafanyika kinyume cha sheria.

Nchi za Afrika zinasumbuliwa na umaskini licha ya utajiri mkubwa wa madini

Sudan ni moja ya nchi za bara Afrika zenye utajiri mkubwa wa madini hususan dhahabu, ingawaje shughuli za uchimbaji madini katika aghalabu ya matimbo ya nchi hiyo ya kaskazini mwa Afrika zinafanyika kinyume cha sheria na bila ya uangalizi wa vyombo vya dola.

Mwaka jana 2020, Sudan ilizalisha tani 36.6 za dhahabu, ikiwa ni nchi ya pili barani Afrika kuzalisha kiwango kikubwa zaidi cha madini hayo yenye thamani ndani ya mwaka mmoja.

Post a Comment

0 Comments