Bilioni 7.3/- kufungua barabara wilayani Iramba

              
SERIKALI kupitia Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) imetenga shilingi bilioni 7.3 kwa ajili ya kufungua barabara za Halmashauri ya Wilaya ya Iramba mkoani Singida ikiwa ni utekelezaji wa kauli mbiu yake ijulikanayo kama ‘Tunakufungulia barabara kufika kusikofikika’.
            

Akiwa katika ziara ya kikazi wilayani humo,Waziri wa Nchi Ofisi ya Raia Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (OR-TAMISEMI), Mheshimiwa Ummy Mwalimu amesema azma ya Serikali ni kufungua barabara za vijijini ili wananchi waweza kufanya kazi zao bila kikwazo cha usafiri.

Akikagua barabara ya Shelui - Tintigulu inayojengwa kwa urefu wa kilomita saba, Waziri ameelekeza barabara hiyo ijengwe kwa ubora unaotakiwa ili iweze kudumu na kuwasaidia wananchi wa Shelui katika shughuli zao za kila siku.

"Lengo la Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Samia Suluhu Hassan ni kuwafungulia wananchi wa vijijini barabara ili isiwe kikwazo tena katika shughuli zao na hapa nimeona baada ya barabara hii kukamilika inakwenda kufungua na kurahisisha mawasiliano ya kata tatu na vijiji sita,"amesema.

Pia Waziri Ummy alimuelekeza Meneja wa TARURA Wilaya, Mhandisi Evance Kibona kuhakikisha kuwa wanafanya usanifu wa Daraja la Nshoka linalounganisha kata za Shelui - Tintigulu ili barabara hiyo inayojengwa iweze kuleta manufaa zaidi kwa wananchi wa maeneo hayo.

"Nimekagua ujenzi wa barabara, umeanza lakini nimeona kuna mto Nshoka ambao unatakiwa kujengewa daraja ili barabara hii inayojengwa iweze kuleta manufaa, vinginevyo bado watakuwa wanapata usumbufu wakati wa mvua nataka tumalize kabisa changamoto hii.

"Mto huu ni mkubwa na hakuna daraja sasa wakati wa mvua wananchi hawawezi kupita hapa hivyo ni vyema hapa pakajengwa daraja ili barabara hii iwe na tija stahiki, hivyo wahandisi anzeni kufanya usanifu na muingize kwenye bajeti ya mwaka wa fedha 2022/23 tuweke ujenzi wa daraja hili kwenye bajeti yetu.

Akizungumza wakati wa ukaguzi wa barabara hiyo ya Shelui-Tintigulu, Meneja wa TARURA Wilaya ya Iramba, Mhandisi Evance Kibona amesema, ujenzi wa barabara hiyo umeanza Desemba 11 na utakamilika Juni,2022.

Pia ameeleza kuwa,barabara hiyo itakayokuwa na urefu wa kilomita saba itagharimu shilingi milioni 524 na inajengwa kwa kiwango cha lami.

Barabara hii inajengwa kwa fedha kutoka katika tozo na ikikamilika itaunganisha kata tatu na vijiji sita vyenye wakazi zaidi ya 14,000.

Kwa mwaka wa fedha 2020/21 bajeti ya miundombinu ya barabara katika Wilaya ya Iramba ilikuwa milioni 860 na katika mwaka wa fedha 2021/22 bajeti hiyo imeongezwa mpaka kufikia shilingi bilioni 7.3.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments