Recent-Post

CCM yarejea utaratibu wake, kina Polepole waitwa kamati kuu kujieleza

 Chama cha Mapinduzi (CCM)  kimerejea utaratibu wake wa kuadhimisha kitaifa sherehe za kuzaliwa kwake.

Mbali na hilo CCM imesema wabunge wake watatu, Askofu Josephat Gwajima (Kawe), Jerry Silaa (Ukonga) na Humphrey Polepole (kuteuliwa na rais)  wataitwa wakati wowote kwenye kamati kuu kujieleza.

Hayo yamesemwa leo Jumamosi Desemba 18, 2021 na katibu wa Itikadi na Uenezi, Shaka Hamdu Shaka muda mfupi baada ya kumalizika kwa kikao cha Halmashauri Kuu ya Taifa (Nec).

Shaka amesema mwakani CCM inatimiza miaka 45 tangu kuzaliwa kwake Februari 5, 1977  baada ya kuunganishwa vyama vya Afro Shirazi na Tanu.

Amesema CCM katika miaka ya karibuni  ilikuwa haifanyi maadhimisho ya kitaifa na badala yake zilifanyika shughuli za kijamii kwa kila mkoa kivyake katika kuadhimisha siku hiyo.

Amesema maadhimsho ya miaka 45 mwakani yatafanyika kitaifa mkoani Mara na mgeni rasmi atakuwa mwenyekiti wa chama hicho, Rais Samia Suluhu Hassan.

Shaka amesema uzinduzi wa sherehe hizo utafanyika Januari 29, 2022 katika Mkoa wa Kusini Unguja na zitazinduliwa na makamu mwenyekiti wa CCM Zanzibar, Dk Ali Mohamed Shein.

Pia, Shaka amesema suala la wabunge watatu ambao wanatuhumiwa kwa kukiuka taratibu za CCM limepokelewa na kwenye kikao cha kamati kuu kilichotanguliwa na kamati ya maadili ya Taifa iliyokaa chini ya Rais Samia.

Amesema wabunge waliohojiwa na kamati ya maadili ya wabunge wa CCM ripoti yake iliwasilishwa kwenye chama kwa ajili ya maamuzi na uamuzi na kwamba wataitwa wakati wowote.

"Chama kimepokea taarifa ya viongozi wake kukiuka maadili, wataitwa kwa mujibu wa taratibu za chama. Tarehe ya kuwaita itapangwa ikiwamo kuwajulisha wahusika,"  amesema Shaka.

Wabunge hao walituhumiwa kwa makosa ya kusema uongo, kulidhalilisha Bunge na kugonganisha na wananchi na Serikali.

Kosa hilo liliwasababishia adhabu ya kufungiwa kushiriki  mikutano miwili ya Bunge na kulipwa nusu mshahara.

Post a Comment

0 Comments