Recent-Post

Gavana akoleza sakata la mikopo

Siku moja baada ya Rais Samia Suluhu Hassan kusisitiza Serikali itaendelea kukopa, Gavana wa Benki Kuu ya Tanzania (BoT), Profesa Florens Luoga amesema hadi sasa deni la Taifa bado ni himilivu kwa kiwango kikubwa.

Wakati akisema hayo, wachumi na wanasiasa wamesema mikopo kwa nchi haiepukiki, huku wakitahadharisha kuhusu matumizi ya mikopo hiyo.

Juzi Rais Samia alisema Serikali yake itaendelea kukopa fedha kwa ajili ya kukamilisha miradi ya maendeleo, kauli ambayo ilionekana kutofautiana na ile iliyokuwa imetolewa na Spika wa Bunge, Job Ndugai Jumatatu.

Ndugai alinukuliwa akitahadharisha kuhusu ukopaji, huku akitetea uamuzi wa Bunge kupitisha tozo za miamala ya simu kwa ajili ya kugharamia miradi ya maendeleo.

Akizungumza jana kwenye mahojiano na Kituo cha redio cha Clouds FM, Profesa Luoga alisema katika makadirio ya BoT, kiwango cha deni kwa pato la Taifa hakipaswi kuzidi asilimia 70, lakini akabainisha kuwa kwa mujibu wa utafiti uliofanyika Novemba 2020, uhimilivu ulikuwa asilimia 27.9.

Alieleza kuwa tayari kuna utafiti mwingine uliofanyika mwaka huu wa kupima kiwango cha deni na anatarajia hautaonyesha matokeo tofauti na yale yaliyoonekana Novemba 2020.

“Hii ina maana kwamba hatujafikia hata nusu ya kiwango cha asilimia 70,” alisema Profesa Luoga.

Aliendelea: “Mpaka sasa Tanzania haijagusa kizuizi cha deni, bado tupo kwenye kijani, hatujafikia alama nyekundu ya deni.”

Alisema kwa kuangalia kiwango cha deni na kiwango cha mapato ambacho ni asilimia 18, Tanzania kwa mwaka 2020/21 kilikuwa asilimia 14.6 ambapo kinatarajiwa kwa mwaka 2021/22 kuwa asilimia 14.2 na baadaye kuendelea kushuka hadi asilimia 12.

Ukiangalia uwiano wa deni kwa pato la Taifa kwa mujibu wa IMF, mwaka 2020/21 tulikuwa asilimia 18.8, 2020/22 ni asilimia 18.8 tena, 2022/23 inatarajiwa kuwa asilimia 18.7 na tunatarajia kufikia asilimia 20.2 2031/32, kwa hiyo hatuko katika hali mbaya kama nchi,” alielezea.

Alisema kwa mujibu wa IMF, iwapo nchi inakuwa na deni lisilozidi asilimia 40 ya pato la taifa, inakuwa salama na inaweza kuendelea kukopa.

“Nchi inapojikuta katika deni linalozidi asilimia hiyo ya pato la Taifa, mfano asilimia 100 hadi 200 tayari itakuwa hatarini,” alisema.

Kati ya nchi 170 duniani zenye mzigo mkubwa wa deni ikilinganishwa na pato la Taifa, alisema Japan inaongoza, huku Tanzania ikishika nafasi ya 109. Barani Afrika, Angola inaongoza kwa asilimia 111.

“Tunapokopa, hatukopeshwi kwa ajili ya chakula bali tunafanya kwa ajili ya miradi ambayo itaendelea kuzalisha, na kwa sababu tunaendelea kuzalisha, ina maana uwezo wetu wa kuhimili madeni utaendelea kuwa bora kadri mapato yanavyoongezeka,” alisema.

Alisema: “Serikali inapokopa nje ya nchi inategemea rasilimali ilizonazo. Ikitokea imeshindwa kulipa, mkopeshaji anaweza akarudisha pesa kwa kufanya nini?”

Alitoa mfano wa kukamatwa kwa ndege ya Tanzania nchini Canada, akisema iliachiliwa kwa sababu Serikali ilikuwa na uwezo na ililipa deni.


Wachumi watahadharisha

Akizungumzia mikopo inayochukuliwa na Serikali, mtaalamu wa uchumi na kodi, Dk Balozi Morwa alisema mikopo inatakiwa kuchukuliwa kwa ajili ya kuchechemua uchumi ili kuongeza ajira, huku pia akionya Serikali kuielekeza kwenye miradi isiyo na faida.

“Kama unachukua mikopo halafu (kwa mfano) unanunua ndege wakati biashara haitabiriki, itakuwa ngumu kulipa. Halafu Serikali isijiingize kwenye kufanya biashara, bali ichukue mikopo kwa ajili ya kuweka mazingira mazuri ya sekta binafasi ili yenyewe ikusanye kodi,” alisema Dk Morwa.

Pia Dk Morwa alionya uchukuaji wa mkopo wakati nchi inapoteza makusanyo ya mapato ya ndani kuwa nalo si jambo jema kiuchumi.

“Ni sawa na kujinunulia umasikini kwa hela zako mwenyewe. Ni vema basi kwanza tujiridhishe kuwa tumejitosheleza na vyanzo vyote vya mapato na kuziba mianya yote ya upotevu wa mapato kabla ya kukimbilia kukopa,” alisema.

Pia alionya mazingira ya rushwa, akisema yasipodhibitiwa yatasababisha mikopo isilipike.

Mkopo mzuri ni ule wenye uwezo wa kutengeneza ajira zitakazozalisha kodi na kuchechemua uzalishaji utakaolipa kodi na biashara katika sekta binafsi,” alisema.

Maoni hayo yameungwa mkono na Profesa Humphrey Moshi wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, akiongeza kuwa kinachozingatiwa kwenye mikopo ni masharti.

“Inategemea unakopa kwa masharti gani, mkopo mzuri ni ule wenye masharti matatu, kwanza unapewa muda wa msamaha mrefu kabla ya kuanza kulipa (grace period), pili riba inakuwa ndogo chini ya asilimia moja na tatu unalipa kwa muda mrefu. Siyo kizazi hicho hicho kinalipa,” alisema.

Pia alisema mikopo inatakiwa kuelekezwa pale ilipokusudiwa. “Kama itaelekezwa pale inapotakiwa itakuwa na faida, lakini kama itaelekezwa kwenye mifuko ya watu au kama zamani ambapo watu walikuwa wanaacha nusu yake kwenye benki za Ulaya, haitalipika.”

Kwa upande wake, Kiongozi wa ACT Wazalendo, Zitto Kabwe alisema tatizo linalosumbua kwenye deni la Taifa ni kuwepo kwa mikopo ya kibiashara yenye masharti magumu.

“Mpaka Machi 2021 Deni la Taifa lilikuwa Sh72 trilioni, kati ya hizo asilimia 40 ni mikopo ya kibiashara ambayo ni ghali sana na tunailipa kwa muda mfupi,” alisema.

Hata hivyo, amepongeza mwelekeo mpya wa kukopa, akitoa mfano wa mkopo uliotolewa na Shirika la Fedha la Kimataifa (IMF) wa Sh1.3 trilioni ambao hauna riba na utalipwa kwa muda mrefu.

“Mikopo nafuu ya aina hii kama vile IMF na Benki ya Dunia husaidia kuimarisha akiba ya fedha za kigeni, kwani ni mikopo ambayo huletwa nchini kwa dola za Marekani lakini matumizi yake ni kwa shilingi ya Tanzania,” alisema.

Akizungumza juzi na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Mbunge wa zamani wa Kigoma, Peter Serukamba alitetea uamuzi wa Serikali kuendelea kukopa mikopo yenye masharti nafuu, huku akihoji baadhi ya wanasiasa walioshindwa kukosoa mikopo yenye masharti mabaya.

“Rais wa nchi, Samia amekopa, lakini fedha zile ameweka wazi, amezileta kwenye Kamati ya Bunge ya Bajeti ikakaa ikazigawa, zikaenda kwenye huduma za jamii kwa maana ya maji, elimu, afya na barabara vijijini,” alisema Serukamba.

Alidai kuwa Serikali ya awamu ya tano ilikopa mikopo yenye masharti magumu ya kibiashara, yakiwemo ya kurudisha ndani ya miaka sita kwa ajili ya kugharamia ujenzi wa bwawa la umeme la Mwalimu Nyerere, Reli ya kisasa na ununuzi wa ndege.

“Lakini wakati yote haya yanakopwa hakuna aliyesema, hakuna aliyelaumu, hata wachache tuliosema, hakuna aliyeelewa,” alisema.

Post a Comment

0 Comments