Kaburi la marehemu Veronika Wambali (69) aliyezikwa Desemba 26, 2021 saa 9:00 alasiri katika makaburi ya Mwangaza Manispaa ya Mpanda limefukuliwa kisha jeneza kuvunjwa na kuachwa wazi na watu wasiojulikana.
Tukio hilo limedaiwa kutokea leo Desemba 27,2021 saa 1: 00 asubuhi limegunduliwa na wasamaria wema waliokuwa wakipita katika eneo hilo.
Akizungumza na Mwananchi Digitali msemaji wa familia hiyo, Mulela Mallac amesema marehemu alifariki Ijumaa katika hospitali ya Tumbi iliyopo Kibaha mkoani Pwani alipokuwa akipatiwa matibabu na baadaye alisafirishwa kwenda Mpanda kwa ajili ya maziko.
“Jana mchana tulifanya mazishi, leo tulikuwa tunatoa mavazi kimila tulipomaliza alikuja wifi wa marehemu akasema kaburi limefukuliwa,”amesema.
Amesema baada ya kupata taarifa walifika eneo la tukio na kushuhudia kaburi kufukuliwa huku jeneza likiwa limefukiwa na mchanga kidogo.
“Tulitoa taarifa polisi kwakushirikiana na mwenyekiti wa mtaa, polisi walifika wakaidhinisha tufukue jeneza tukafukua tukaona marehemu yumo ndani wakaamuru tuzike,”
Mwenyekiti wa mtaa wa Mpadeco, Ivo Chambala amekiri kupokea taarifa za tukio hilo kutoka kwa wasamaria wema na baadaye kuwajulisha polisi.
Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Katavi, Ally Makame ameithibitishia mwananchi kutokea kwa tukio hilo.
“Nimepokea taarifa hizo nimemtuma RCO kwenda eneo la tukio baadaye nitakuwa na maelezo zaidi,”amesema Makame.
0 Comments