Kauli ya Samia yaibua maswali kibao

Hotuba ya Rais Samia Suluhu Hassan katika ufunguzi wa mkutano wa Baraza la vyama vya siasa jijini Dodoma juzi imeibua maswali sita kutoka kwa wanasiasa na wachambuzi wa masuala ya siasa, likiwemo la kutozungumzia suala la mabadiliko ya Katiba.

 Masuala mengine yaliyoibuliwa na wadau wa demokrasia, mbali na mabadiliko ya Katiba, ni zuio la vyama kufanya mikutano ya hadhara, maridhiano ya siasa, makada wa upinzani waliofunguliwa kesi, masuala ya kisiasa na kuachiwa huru kwa Mwenyekiti wa Chadema, Freeman Mbowe.

Soma zaidi:Rais Samia awataka viongozi wa vyama vya siasa kuzika tofauti

Hata hivyo, Mkurugenzi wa Mawasiliano ya Rais, Ikulu, Jaffar Haniu alipoulizwa kwa simu kuhusu maoni hayo, alihoji “hivi kwani mtu anapangiwa cha kuzungumza, hasa Rais?”

Alipoulizwa iwapo kuna fursa nyingine ya Rais kukutana na vyama vya siasa, alisema, “kama itakuwepo umma utataarifiwa.”

Pamoja na mambo mengine, juzi Rais Samia alisema yuko tayari kuvumilia kukosolewa, kusikiliza ushauri na kusamehe pale anapokosewa, ila akawataka wenyeviti wa vyama vya siasa kuongoza vyama vyao kutii sheria.

“Niwaombe wenyeviti wenzangu wa vyama vya siasa tusitazame yaliyopita, tutazame mbele kwa matumaini. Tuweke nguvu katika kujenga Tanzania mpya yenye kusameheana na kuheshimiana.

“Kama mlezi wa amani natakiwa kuwa mvumilivu, msikivu na mwenye kustahimili na niko tayari kufanya hivyo,” alisema Rais Samia ambaye pia ni mwenyekiti wa CCM.

Akijadili hotuba hiyo, Profesa wa Sayansi ya Siasa wa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Bakari Mohamed alisema hotuba hiyo haijatoa suluhisho la kisiasa kwa sababu hakugusia masuala ya msingi, hasa la mabadiliko ya Katiba.

“Sikumsikia Rais akizungumzia juu ya Katiba mpya, wala akizungumzia kufanya marekebisho kwenye Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC). Kwa hiyo mambo ya msingi hayajashughulikiwa ila wanataka kupozapoza mambo ili kupunguza kelele za ndani na nje ya nchi,” alisema Profesa Bakari.

Huku akisisitiza kutokuwepo kwa “matokeo makubwa” kutokana na mkutano huo, Profesa Bakari alisema hotuba ya Rais Samia imelenga kupoza majeraha ya kisiasa ya mtangulizi wake, , lakini hakujaonekana mpango wa kuleta mageuzi ya kweli.

“Ni mwendelezo wa mfumo uleule, mtangulizi aliyekuwepo alikwenda mbali zaidi, kwa hiyo wanataka warudi kwenye sehemu ambayo wanaweza wakapoza mambo.

“Kwa sababu wanaona aibu kuruhusu moja kwa moja mikutano na shughuli za siasa ziendelee, wanatafuta njia ili wapozepoze mambo. Wataruhusu mikutano ya siasa iendelee. Lakini mambo ya msingi hawakotayari kuyazungumzia,” alisema.

Mawazo ya Profesa Bakari yanalandana na ya Anthony Komu, naibu katibu mkuu wa NCCR-Mageuzi (Bara), kuwa hotuba hiyo haikugusa wala kutoa mwanga katika maeneo muhimu yanayolalamikiwa na vyama vya siasa.

“Tulitarajia azungumzie suala la marekebisho ya sheria ya uchaguzi, mkwamo wa mchakato wa Katiba mpya, kutoa suluhu ya shughuli za kisiasa na kumaliza suala la Mbowe. Lakini kwa kile tulichokisikia jana ni kama vile anaendeleza yale ya awamu ya tano,” alisema Komu.

Nje ya mjadala huo, Dk Hellen Kijo-Bisimba alipozungumza na Mwananchi kwa simu, alisema anadhani haikuwa sahihi kuzungumzia suala la Mbowe.

“Bado mahakama haijatoa uamuzi kuhusu suala hili, kwa tafsiri ya haraka unaweza kusema Mbowe amekosea, jambo ambalo si sahihi. Pia sioni sababu suala la mikutano ya hadhara lijadiliwe wakati sheria ipo wazi. Kinachotakiwa Rais Samia aseme waendelee kufanya shughuli zao za kisiasa kwa kufuata utaratibu,” alisema.

Naye Mkurugenzi Mtendaji wa Jukwaa la Katiba Tanzania (Jukata), Bob Wangwe aliungana na Dk Kijo Bisimba kueleza kuwa suala la Mbowe liliwasilishwa vibaya katika mkutano huo, jambo linaloleta tafsiri kama Mbowe amefanya makosa wakati mahakama haijatoa hukumu.

Wangwe alisema kujenga mustakabali mwema, kinachotakiwa wote (wadau wa siasa) wawe kitu kimoja na wazungumze ukweli kwenye kikao, wasioneane aibu ili kuleta maelewano na masikilizano.

“Rais Samia asione aibu kusema ukweli kama kuna mambo yalifanyika kinyume cha utaratibu katika awamu iliyopita,” alishauri Wangwe.

Hata hivyo, juzi Naibu Katibu Mkuu wa CCM Tanzania Bara, Christina Mdeme alisema hotuba ya Rais Samia imelenga katika kuleta umoja na mshikamano kwa Watanzania.

Pia alisema mlengo wa hotuba hiyo unakwenda kuhakikisha mustakabali wa Taifa unaenda kuwa wa umoja, amani na mshikamano.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments