MASOMO WAKATI WA LIKIZO CHANZO KUDUMAA KWA UBONGO WA WATOTO


Na JUMA ISSIHAKA 

HATUA ya wanafunzi wa Shule za Msingi na Sekondari kulimbikiziwa masomo muda wa ziada na wakati wa likizo, imetajwa kuathiri ukuaji wa ubongo wa mtoto na hivyo kusababisha wengi kuwa na uwezo wa kukariri badala ya kuelewa. 

Kwa mujibu wa Chama cha Madaktari (MAT), changamoto hiyo ndiyo sababu ya kuwa na wasomi wanaopata alama ‘A’ darasani lakini utendaji kazi wao katika maisha ya kitaaluma ni duni. 

Akizungumza na SAYARI NEWS, Rais wa Chama cha Madaktari (MAT), Dk. Shadrack Mwaibambe, anasema ratiba zinazomnyima mtoto likizo na muda wa kupumzika zina athari kiafya na maendeleo ya mwanafunzi. 

Anasema hatua ya wanafunzi kulimbikiziwa masomo bila mapumziko humfanya kuwa na uwezo wa kukariri badala ya kuelewa kwa kuwa wanakuwa na mzigo mzito wanaolazimika kuuhifadhi badala ya kuelewa. 

“Hii ndiyo sababu leo hii watoto wetu hawawezi kufanya wanachokisoma bali wanaweza kupata alama ‘A’ katika mitihani yao, unakuta mtoto amefaulu vizuri lakini ukimleta katika utendaji wa alichosomea anashindwa,” anasema. 

Anasema utaratibu huo huwaingiza watoto katika msongo wa mawazo kwa kuwa hawana uwezo wa kulalamika, lakini ni ukweli kwamba wanachoka. 

Rais huyo wa MAT, anasema madhara mengine yanayomkumba mtoto iwapo atakosa muda wa likizo ama mapumziko ni kudumaa kwa maendeleo ya ubongo. 

Anafafanua kwamba maendeleo ya ubongo wa mtoto hutokana na kuona, kusikiliza na kugusa hasa kwa watoto wadogo zaidi. 

Dk. Mwaibambe anaeleza watoto wa shule walishavuka ile hali ya kugusa na iliyobaki kwao ni kuona na kusikia ambapo hatua ya kukaa masaa 14 na nusu shuleni akisikiliza na kuona vitu vya aina moja hufanya ukuaji wa ubongo wake ulemae. 

“Mtoto hawezi kupata maendeleo ya ubongo kwa kusikia na kuona jambo moja wakati wote, tunajua nyuma ya hili kuna biashara lakini muhimu wapate mazingira tofauti, hasa wakati wa likizo ambao huutumia kutembelea ndugu na jamaa zao,” anasema. 

Anasema ratiba hizo huwafanya watoto kukosa muda na familia zao na hivyo kushindwa kujifunza mambo mengine muhimu nje ya taaluma za shuleni. 

Anashauri hata utaratibu wa wanafunzi kukaa bweni uwe hiari, wasilazimishwe kama inavyofanywa na baadhi ya shule hasa binafsi kwa madarasa ya mitihani. 

Alisema zipo faida nyingi za mtoto kukaa nyumbani na familia yake, kwani nje ya taaluma za shuleni anafunzwa stadi za maisha. 

Anaongeza kwamba hatua ya MAT kutaka kuanza utafiti wa madhara yanayowakumba wanafunzi kwa kukosa likizo na muda wa kupumzika imetokana na malalamiko ya baadhi ya wazazi. 

Anasema changamoto iliyopo ni kwamba baadhi ya watu wameitafsiri vibaya dhamira ya madaktari ambayo inalenga kusaidia watoto bali wao hudhani imelenga kuharibu biashara. 

Anasisitiza kwamba wanaendelea kukusanya maoni na baadaye wataomba kukutana na Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Profesa Joyce Ndalichako, ili kuzungumza naye. 

Hata hivyo, SAYARI NEWS imebaini kwamba utaratibu huo haufanywi na shule binafsi pekee, bali zipo baadhi ya shule za serikali huwanyima wanafunzi likizo zikiwataka kuendelea kubaki masomoni.


Katibu Mkuu TAMISEMI, Prof. Rizik Shemdoe


SERIKALI YAPIGILIA MSUMARI 

Katika mazungumzo yake na SAYARI NEWS, Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI), Profesa Rizik Shemdoe, anasema kupitia marekebisho ya Sheria ya Elimu ya mwaka 1978, zilitungwa Kanuni za Elimu za mwaka 2002. 

Anabainisha sheria na kanuni hizo zinaweka idadi ya siku za masomo kwa mwanafunzi katika mwaka wa masomo husika, kuwa ni siku 194 kwa Shule za Msingi na Sekondari ukiondoa Jumamosi, Jumapili, Sikukuu za Umma na Likizo. 

Profesa Mdoe anasema maagizo hayo yanapaswa kusimamiwa kikamilifu na Ofisi ya Rais TAMISEMI ambayo ndiyo yenye jukumu la kutekeleza maelekezo ya Kisera na Sheria. 

“Kanuni hizo hazikuacha ombwe katika usimamizi, bali zimeeleza kuwa, endapo siku za masomo zitapotea kwa sababu zilizo nje ya uthibiti wa Shule au Mamlaka. 

“Shule au Mamlaka hiyo itapaswa kuomba kibali cha kufidia siku hizo kwa Kamishna wa Elimu na katika Kibali chake Kamishna ataeleza muda wa kusoma wakati wa likizo. Hiyo ni kwa shule zote za serikali na binafsi,” anasema. 

Anasema Wizara imefanya hivyo kwa kutambua kwamba, likizo ni muda wa mtoto kupumzika na hivyo kuwa na uwezo wa kufuatilia masomo vizuri zaidi katika muhula unaofuata. 

Aidha, anasema muda wa likizo humwezesha mtoto kuwatembelea na kuchangamana na ndugu, jamaa na marafiki na hivyo, kukuza stadi zisizo za kitaaluma. 

Anasisitiza kwamba ni muhimu kumuendeleza mtoto katika maeneo yote, kwa maana ya kitaaluma na mengine. 

“Watoto wetu ni zao la jamii na hivyo tusijaribu kuitenga elimu na jamii. Pia, tuwape watoto wetu fursa ya kujifunza shughuli ndogo ndogo za kijamii na kiuchumi kama vile usafi wa mazingira, kilimo, upishi, ujenzi na ujasiliamali,” anasema. 

Katibu Mkuu huyo, alizitaka shule zote za serikali na binafsi kuhakikisha zinazingatia sheria hiyo.


Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAPIE), Mahmoud Mringo


WAMILIKI SHULE BINAFSI WANENA 

Mwenyekiti wa Chama cha Wamiliki wa Shule Binafsi Tanzania (TAPIA), Mahmoud Mringo, anasema kwa kuwa serikali imetoa maelekezo wajibu wao ni kutekeleza. 

Alipoulizwa kuhusu nini watafanya kuhakikisha shule zote binafsi zinatekeleza hilo, alijibu kwa kifupi kwamba jukumu ya usimamizi ni la mamlaka za serikali, watakachokifanya wao ni kutekeleza maelekezo. 

Kwa upande wake, Mkuu wa Shule ya Sekondari St. Anne Marie Academy jijini Dar es Salaam, Mwalimu Gradius Ndyetabula, anakiri kuwepo kwa suala hilo, lakini mara kadhaa hufanywa kwa madarasa yanayokaribia mitihani. 

Anasema katika shule anayoiongoza wamekuwa wakiwapa mazoezi wanafunzi kwa mujibu wa maelekezo ya Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI). 

Mkuu huyo anasema mathalan kwa mwaka huu TAMISEMI imetoa muongozo unaotaka mwanafunzi akae shuleni kwa siku 192 tu. 

Anabainisha kwamba utaratibu waliokuwa wakiutumia ni kuandika barua za kuomba kuongeza siku chache kwa ajili ya kuwafanyia mazoezi wanafunzi wa madarasa yanayokaribia mitihani. 

“Waziri ametoa maelekezo na yeye ndiye msimamizi wa shughuli hizi, tunachosubiri ni maelekezo rasmi yatakayoshushwa kwa viongozi wa chini kuanza utekelezaji lakini tumepokea na tutatekeleza,” anasema. 

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments