RAIS SAMIA AFUNGUKA KUHUSU KUMSAMEHE FREEMAN MBOWE

 

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Samia Suluhu Hassan amewakumbusha viongozi wa vyama vya siasa kuzingatia na kutii sheria ili kuepuka heshima zao kuondoka.

Rais Samia ameeleza hilo leo wakati akijibu ombi la Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe ambaye alimuomba awasaidie kumsamehe Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe.

''Nataka nizungumzie kidogo aliloniomba mwanangu Zitto, kwamba yule mwenzetu msamehe basi aje awe na sisi. Demokrasia ni kuheshimu sheria, heshima ya mtu inakuja kwa kuheshimu sheria za nchi. Naomba tufanye kazi kwa kufuata sheria waswahili wanasema mtaka nyingi na saba... ingawa kusameheana nako kupo,'' ameeleza Rais Samia Suluhu.

Aidha Rais Samia amesisitiza kuwa kuna taifa moja tu ambalo raia wote wanawajibika kulilinda.

''Nitumie fursa hii kuwakumbusha kwamba Duniani kuna nchi moja tu inayoitwa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ambayo ni taifa huru lililojengwa kwa misingi ya amani, upendo, mshikamano na linaloongozwa kwa misingi ya katiba na sheria zilizotungwa na bunge na sio utashi wa mtu au mataifa mengine. Na wenye hili taifa ni sisi,'' amesema Rais Samia Suluhu.


Kiongozi Mkuu wa Chama Cha ACT Wazalendo Ndugu Zitto Kabwe amemuomba Rais Samia kuwasaidia kumtoa Mwenyekiti wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) Freeman Mbowe ili waungane naye katika kujenga taifa.

Zitto ameyasema hayo alipopata nafasi ya kuongea kwenye Mkutano wa Wadau wa Kujadili Hali ya Demokrasia ya Vyama Vingi Nchini uliofanyika leo Desemba 15, 2021 katika Ukumbi wa Hazina jijini Dodoma.

”Sisi viongozi wa Vyama tupo hapa lakin na kuna mwenzetu hayupo kwasababu ya changamoto za kisheria na tuna utamaduni sisi wa kumaliza haya mambo na haitakuwa mara ya kwanza, tunakuomba sana kwa mujibu wa sheria na taratibu zote za kisheria tusaidie mwenzetu tuwe naye,” ameeleza Zitto Kabwe.

Katika hatua nyingine Zitto ameeleza wanavyouchukulia Mkutano huo. ”Hatua hii sisi tunachukulia kuwa ni muhimu sana kuelekea katika kuwa na majadiliano ya kisiasa katika nchi yetu na kila jambo lina mwanzo na huu ni mwanzo mwema na Mungu atatuongoza tuweze kuwa na utaratibu huu kama ambavyo tulivyo Tanzania”.

CHANZO - EATV & Global Tv

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments