Recent-Post

Rais Samia avipa thamani vituo shikizi, wizara yasisitiza kwa uwekezaji wa kisasa vinakwenda kuwa shule kamili

NAIBU Katibu Mkuu Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (anayeshughulikia Elimu), Gerald Mweli amesema, Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Samia Suluhu Hassan imewekeza katika Vituo Shikizi ambavyo kwa kipindi kirefu havikuboreshwa.

Akizungumza katika ziara yake wilayani Kongwa mkoani Dodoma yenye lengo la kukutana na walimu, kusikiliza changamoto zao na kukagua ujenzi wa miundombinu ya elimu, Mheshimiwa Mweli amesema, vituo hivyo sasa vinakwenda kuboreshwa ili kutoa elimu bora kwa watoto wa Kitanzania.

"Tathimini iliyofanyika inaonesha kuwa, kuna vituo shikizi 1,155 na kati ya hivyo 970 vina wanafunzi kuanzia 20 mpaka 400 na ndivyo vilivyopata fedha za ujenzi wa vyumba vya madarasa kwa kuwa vina wanafunzi wengi na vilikuwa na miundombinu duni ambayo haikuwa rafiki kwa wanafunzi kujifunzia.
"Hivyo tunakwenda kujenga vyumba vya madarasa 3,000 kwa gharama ya shilingi bilioni 60 na vitakapokamilika, vituo hivi shikizi 'vitagraduate' na kuwa shule kamili za msingi,hivyo tutaongeza shule 970,"amesisitiza Mweli.

Pia amesema, madarasa hayo yatakapokamilika watoto hao sasa hawatakuwa wanaenda tena kwenye shule Mama wanapofika madarasa ya juu, "hivyo tutakuwa tumewapunguzia umbali mrefu waliokuwa wanatembea hapo awali.

"Haya ni mafanikio makubwa katika Sekta ya Elimu na tunamshkuru sana, Mheshimiwa Rais Samia Suluhu Hassan kwa kutoa kipaumbele katika eneo hili la vituo shikizi,"amesema Mheshimiwa Mweli.
Amesema, vituo shikizi ni vituo vinavyoanzishwa kusaidia wanafunzi wenye changamoto za kijografia yakiwemo mobonde, makorongo, mbuga zenye wanyama wakali ukiwemo na umbali toka shule mama na ilipo jamii.

"Vituo hivi hutumika kufundishia wanafunzi wa elimu ya awali hadi darasa la pili wanaokaa mbali na shule mama,"amesema Mheshimiwa Mweli.

NA NTEGHENJWA HOSSEAH-OR-TAMISEMI

Post a Comment

0 Comments