Recent-Post

Rais Samia awasilisha hati ya mali na madeni kwa Sekretarieti ya Maadili

Rais wa Tanzania Samia Suluhu Hassam amewasilisha hati ya tamko la viongozi wa umma kuhusiana na mali na madeni waliyo nayo kwa mwaka 2021 kwenye Sekretarieti ya Maadili ya Viongozi wa Umma.

Taarifa hiyo imetolewa leo Desemba 3, 2021 na Kamishna wa Maadili ya Viongozi wa umma, Jaji Sivangilwa Mwangesi wakati akizungumza na waandishi wa habari, ikiwa ni njia ya kuwakumbusha viongozi wa umma ambao hawajawasilisha hati hizo kufanya utaratibu huo mara moja.

Amesema takwa hilo ni kwa mujibu wa sheria No.13 ya mwaka 1995 sura ya 398 ibara ya 132 ya Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ikiwataka kuwasilisha hati hizo kwa Kamishna wa maadili.

Amesema kwa mwaka 2021, uwasilishaji data ulianza Oktoba mosi, 2021 mpaka 31, Desemba ambapo viongozi wanatakiwa kuwasilisha tamko hilo.

Kati ya wale waliowasilisha mpaka sasa hivi ni Rais wa Tanzania ambalo tamko lake limewasilishwa Novemba 29 Kanda ya Dar es Salaam, ambapo hapa makao makuu limewasilishwa jana,” amesema Jaji Mwangesi.

Akizungumzia hali ya utekelezaji wa takwa hilo amesema viongozi hao wameonekana kusuasua, kwani hadi mwishoni mwa Oktoba waliokuwa wamewasililisha tamko lao ni Kanda ya kati 28, Dodoma 6, Kanda ya Kusini 7, Kanda ya Kaskazini 11, Nyanda za juu Kusini 20, Kanda maalumu 53, Magharibi 18, Mashariki 8 na Kanda ya Ziwa 16.

Amesema idadi hiyo inasuasua kwa kuonekana bado kuna pengo kubwa la uwasilishaji huo kwani viongozi wanaotakiwa kupeleka ni zaidi ya viongozi 15,300.

Kama Kiongozi wa nchi anajua majukumu yake mapema basi ni vema viongozi waliobaki nao wafate nyayo zake, kwani muda uliobaki ni mchache,” amesema.

Jaji Sivangilwa amesema kutokurejesha wasilisho hilo ni kosa chini ya kifungu cha 15 cha sheria ya maadili ya viongozi wa umma ambapo sheria inaruhusu kuwapeleka viongozi wasiowasilisha tamko lao katika Baraza la maadili kuweza kuwatolea maamuzi.

Post a Comment

0 Comments