RC Mahenge ashiriki utiaji saini mikataba 26 kati ya Wakandarasi na TARURA

MKUU wa Mkoa wa Singida,Dkt.Binilith Mahenge leo Desemba 1, 2021 ameshiriki utiaji wa saini katika mikataba 26 ya awamu ya pili baina ya Wakandarasi na Wakala wa Barabara za Vijijini na Mijini (TARURA) wa mkoani hapo zenye thamani ya shilingi Bilioni 12.6 ambazo zimetokana na makusanyo ya tozo za miamala ya simu.


Utiaji saini huo umefanyika katika ukumbi wa Mkuu wa Mkoa na kuhudhuriwa na viongozi mbalimbali wa mkoa pamoja na taasisi za kifedha zikiwemo Benki ya CRDB, NMB na makampuni ya bima kwa ajili ya kuandaa mazingira ya kuwakopesha wakandarasi hao.
Akiongea katika hafla hiyo, Mkuu wa Mkoa amewataka wakandarasi waliopata kazi hizo za utengenezaji wa barabara katika halmashauri saba za Mkoa wa Singida kuhakikisha zinajengwa kwa viwango na kulingana na thamani ya fedha zinazotolewa.

Aidha, RC Mahenge amewakumbusha wakandarasi hao kutumia ratiba ya kazi vizuri na kukamilisha kazi kwa wakati huku akiwataka kutumia muda huu ambapo mvua sio nyingi kuanza utekelezaji wa miradi kwa sababu hakutakuwa na muda wa nyongeza.
“Kwa kuwa fedha zinazotumika ni kodi za wananchi zinazotokana na makato kweye simu ni vizuri kila mmoja wenu afanye kazi kwa uzalendo kwa kuwa miradi yote inatekelezwa na wakandarasi wazawa, tuhakikishe fedha zinatumika kulingana na kazi zinazofanyika,”amefafanua Dkt.Mahenge.

“Kupata mradi ni jambo moja na kutekeleza mradi ni jambo la pili, nafahamu wapo watu watatumia zaidi ya siku 14 walizopewa za kukusanya vitendea kazi kwa mambo mengine hivyo kusababisha ucheleweshaji wa kazi, hatutakuwa na msamaha kwa mkandarasi yeyote atakayefanya kazi mbaya na atakayechelewesha kazi,”alisisitiza Dkt.Mahenge.
Hata hivyo, Dkt.Mahenge ametumia muda huo kuishukuru Serikali kwa kutoa Bilioni 12.6 kwa ajili ya ujenzi wa barabara za mijini na vijijini katika wilaya zote mkoani Singida na kukiri kwamba kwa kipindi kifupi kilichopita walipata sh. Bilioni 27 za UVIKO-19 ambazo zililenga kwenye miradi ya maendeleo hivyo kwa kipindi kifupi Serikali imeleta fedha nyingi kwa ajili ya kuendeleza miradi mbalimbali mkoani hapa.

Akimaliza hotuba yake RC Mahenge amewashukuru TARURA kwa jitihada zao za kufanikisha mchakato wa kuwapata Wakandarasi wenye sifa zinazukubalika hivyo kuwataka wakala hao wa barabara za vijijini na mijini kuwasimamia ili waweze kukamilisha kazi kwa wakati na kwa kiwango kinacho stahili.

Kwa upande wake Mwenyekiti wa CCM Mkoa, Jumanne Kilimba amesema kupitia kamati ya siasa watahakikisha wanakagua miradi hiyo kwa umakini mkubwa ili kuhakikisha wananchi wanapata kile kilichotarajiwa kufikishwa na Serikali kwa lengo la kuwanufaisha wakazi wa Mkoa wa Singida.

Hata hivyo, amebainisha kwamba wakandarasi hao wana uwezo mkubwa kwa kuwa wengi wao wameshafanya kazi mkoani hapo na kuwahakikishia kwamba wanaendelea kupata kazi mkoani hapo endapo watafanya vizuri na kuwakumbusha kwamba atakayeharibu Mkoa wa Singida asitegemee kupata kazi mkoa wowote.
Awali akieleza malengo ya hafla hiyo Meneja wa TARURA Mkoa wa Singida, Mhandisi Tembo D.R amesema, mikataba hiyo itatekelezwa katika Wilaya ya Iramba, Itigi, Singida DC, Manyoni, Mkalama, Ikungi na Manispaa ya Singida.

Amesema, makampuni yaliyopata kazi hizo ni M/S Kangwa General Supply Ltd, M/s J.P Trader Ltd, Chase Investment, Brand Mark, Kumba Quality, Sumaco Eng., Coyesa company, Gornad company na nyinginezo nyingi ambazo kwa mujibu wa mkataba wanatakiwa kumaliza kazi ndani ya miezi sita.
 NA MWANDISHI DIRAMAKINI

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments