Recent-Post

Serikali yatenga Sh48.5 bilioni ujenzi vyuo vya Veta

Waziri wa Elimu, Sayansi na Teknolojia, Joyce Ndalichako amesema Serikali imetenga kiasi cha Sh48.5 bilioni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na ununuzi wa samani kwa vyuo vya mafunzo ya ufundi stadi VETA 29 ambavyo vinatakiwa kukamilika ifikapo Juni 2022.

Akizungumza leo Desemba22, 2021 mjini Kasulu mkoani Kigoma wakati wa makabidhiano ya majengo pamoja na uwekaji wa jiwe la msingi katika ujenzi wa chuo ufundi stadi (Veta) kilichopo kijiji cha Nyumbigwa, amesema Serikali imedhamiria kuendeleza ujenzi wa vyuo hivyo nchini.

Amesema fedha hizo ni kwa ajili ya kukamilisha ujenzi na kununua samani kwa vyuo 25 vya wilaya, vinne vya ngazi ya mkoa katika mikoa ya Njombe, Rukwa, Geita na Simiyu, mabweni mawili katika chuo cha ualimu wa ufundi stadi Morogoro na kwamba ukamilishaji wa vyuo hivyo utaongeza fursa za udahili wa wanafunzi 35,600 wa ufundi stadi.

"Ili kutimiza azma hiyo serikali imeendelea kutenga fedha kwaajili ya kukamilisha ujenzi wa vyuo vya mikoa na wilaya kwa awamu kupitia mpango wa maendeleo kwa ustawi Taifa na napambano dhidi ya UVIKO -19 ambapo serikali imetenga jumla ya sh 48.5bilioni," amesema Ndalichako.

Kwa upande wake Mkurugenzi Mkuu wa VETA Tanzania, Pancras alisema chuo hicho ni miongoni mwa mwa vyuo 29 vilivyojengwa nchini, lengo likiwa ni kujenga vyuo hivyo kila mkoa ifikapo mwaka 2025.

Amesema chuo hicho kitaanza kupokea wanafunzi kuanzia Januari 2022.

Awali akitoa taarifa ya ujenzi wa chuo hicho Mshauri elekezi, Faraji Maganila amesema chuo hicho cha Kasulu kinajengwa kwa awali mbili ambapo awamu ya kwanza walipokea Sh2.197 bilioni ikiwa na majengo 16 huku awamu ya pili itagharimu Sh1.2 bilioni kwa majengo saba.

By Happiness Tesha

Post a Comment

0 Comments