Recent-Post

Simba katika njia ngumu ya kusaka taji Afrika

Wawakilishi wa Tanzania katika mashindano ya Kombe la Shirikisho Afrika Simba, wamefanikiwa kutinga hatua ya makundi baada ya ushindi wa jumla wa mabao 4-2 dhidi ya Red Arrows ya Zambia katika hatua ya mwisho ya mchujo ambapo mechi zake za mwanzo zilichezwa Novemba 28 na mechi za marudiano ilikuwa Desemba 5.

Bado tarehe ya droo ya hatua ya makundi haijapangwa lakini kwa mujibu wa utaratibu, Simba ina nafasi kubwa ya kuwekwa katika chungu cha pili hivyo haiwezi kukutana na timu ambazo itapangwa nazo pamoja katika chungu kimoja ingawa inaweza kujikuta ikiangukia kundi moja na miongoni mwa timu 12 anbazo zitakuwa katika vyungu vingine.

Katika chungu cha pili, Simba itakuwa na Coton Sport na Orlando Pirates.

Chungu cha kwanza kina TP Mazembe na RS Berkane, Pyramids wakati cha tatu kuna Zanaco, JS Saoura, Asec Mimosas na Al Ahli Tripoli na cha nne kina AS Otoho, US Gendarmarie.

Bado mechi kati ya Enyimba na Al Ittihad haijaamriwa kama ilivyo kwa mechi kati ya Royal Leopards na JS Kabylie.

Makala hii inakuletea dondoo fupi za mafanikio katika mashindano ya Afrika kwa timu 10 zilizojihakikishia kutinga hatua ya 16 ambazo miongoni mwazo Simba inaweza kupangwa na tatu kwenye hatua ya makundi. 

TP MAZEMBE

Imefuzu baada ya ushindi wa bao 1-0 dhidi ya Marumo Gallants ya Afrika Kusini ikishinda 1-0 nyumbani na kutoka suluhu ugenini.

Imechukua Ligi ya Mabingwa Afrika mara tano na Kombe la Shirikisho Afrika mara mbili. Pia imetwaa kombe la Washindi mara moja na Super Cup mara tatu.


RS BERKANE

RS Berkane ya Morocco imetwaa ubingwa Kombe la Shirikisho Afrika 2019/2020 na nafasi ya pili mashindano hayo 2018/2019 kama ambavyo imewahi kuwa wa pili katika Super Cup 2021. Msimu huu iliitupa nje APR ya Rwanda kwa mabao 2-1 wakitoka sare tasa ugenini kabla ya kushinda mabao 2-1 nyumbani.


PYRAMIDS FC

Imetinga makundi baada ya kuitoa Maniema ya DR Congo kwa mabao 2-0 ikishinda 1-0 nyumbani na ugenini. Ilitinga fainali ya Kombe la Shirikisho Afrika 2019/2020.


AL MASRY

Ni miongoni mwa timu kongwe duniani kwani ina miaka 101 ingawa haina mafanikio makubwa Afrika.

Timu hiyo ambayo imeingia makundi baada ya kuitoa Rivers United ya Nigeria kwa faida ya bao la ugenini baada ya kutoka sare ya mabao 3-3 katika mechi mbili ikifungwa 2-1 huko Nigeria na kushinda 1-0 waliporudiana Misri.

Mwaka 1999 walifika nusu fainali ya Kombe la Washindi Afrika, wakaingia hatua hiyo Kombe la Caf 2002 na 2018 walifika nusu fainali ya Shirikisho Afrika.

Zanaco PIC

Kikosi cha Zanaco FC.

ZANACO

Wametinga makundi kwa kuitoa Binga FC ya Mali mabao 3-2, wakishinda 3-0 nyumbani Zambia na ugenini wakifungwa mabao 2-0. Mafanikio makubwa ya Zanaco klabu Afrika ni robo finali ya Kombe la Shirikisho 2019/2020.


JS SAOURA

Ni wawakilishi wa Algeria waliowahi kukutana na Simba hatua ya makundi Ligi ya Mabingwa Afrika 2018/2019 na sasa wamefika makundi kwa kuitoa Hearts of Oak ya Ghana kwa mabao 4-2 wakifungwa 2-0 ugenini na kushinda 4-0 nyumbani. Ni timu ambayo haina rekodi kubwa Afrika na msimu waliojitutumua ni 2018/2019 walipoishia makundi ya Ligi ya Mabingwa Afrika.


ASEC MIMOSAS

Miongoni mwa timu zenye historia kubwa katika Afrika.Msimu huu wameitoa Interclube ya Angola kwa mabao 5-2, wakishinda 2-0 nyumbani na mabao 3-2 ugenini. Wamewahi kutwaa Ligi ya Mabingwa Afrika 1998 na 1995 waliishia hatua ya fainali, huku wakicheza nusu fainali ya mashindano hayo mara sita na wakifika nusu Kombe la Washindi mara moja.


AL AHLI TRIPOLI

Wamepenya kwa ushindi wa mikwaju ya penalti 4-2 dhidi ya Stade Malien ya Mali baada ya matokeo ya jumla kumalizika kwa sare ya bao 1-1 kila moja ikipata ushindi wa bao 1-0 nyumbani kwake. Kushika nafasi ya pili Kombe la Washindi Afrika 1984 ni mafanikio yao makubwa.


AS OTOHO

Kuingia makundi msimu huu ndio mafanikio yao makubwa Afrika. Wameitoa Gor Mahia kwa mabao 2-1, wakishinda 1-0 nyumbani na sare ya 1-1 ugenini.

Orlando PIC

Wachezaji wa Orlando Pirates wakifanya mazoezi.

US GENDARMERIE

Waliitoa DC Motema Pembe ya DR Congo kwa mabao 2-1 wakishinda 2-0 nyumbani na kufungwa 1-0 ugenini.


Simba na matumaini

Licha ya kuwepo na timu nyingi zenye uzoefu, Simba wametamba kufanya vizuri.

“Kipaumbele namba moja ni kufika nusu fainali Kombe la Shirikisho na kutetea ubingwa Ligi Kuu. Mashindano yote tunayoshiriki tunataka kushinda,” anasema mtendaji mkuu wa Simba, Barbara Gonzalez.

Kocha wa timu hiyo, Pablo Fraco anasema kuwa lengo la kutinga hatua ya makundi wameshalitimiza na sasa wanajipanga kwa ajili ya hatua hiyo.

Post a Comment

0 Comments