Recent-Post

Uhusiano wa kimapenzi walimu, wanafunzi yalivyotikisa 2020/21


 Uhusiano wa kimapenzi kati ya baadhi ya walimu na wanafunzi umetajwa kuwa miongoni mwa mambo matano yaliyowatesa walimu kipindi cha 2020/21.

Kauli hiyo imetolewa na Mwenyekiti wa Tume ya Utumishi wa Walimu (TSC), Dk Willy Komba jijini Dodoma leo Jumatano Desemba 29, 2021 wakati akizungumza na waandishi wa habari kuhusu maadili ya walimu na changangoto wanazokutana nazo.

Dk Komba amesema katika kipindi cha 2020/21, kesi za mapenzi zilikuwa 211 ambazo ni asilimia 11.8 ya kesi za walimu katika kipindi wakati katika kipindi cha Julai hadi Septemba mwaka huu jumla ya kesi 31 zilifunguliwa pia.

Amesema bado walimu wengi wamekuwa na tabia ya kujihusisha na mapenzi na wanafunzi wanaowafundisha kazi aliyosema hailipi kwa wahusika wala kwa Serikali iliyowekeza kwa walimu na wanafunzi.

Mwenyekiti huyo amesema Tume yao imekuwa ikisikiliza maelezo kutoka kwa wahusika wote kuanzia mwanzo na pale wanapobaini kuwepo na tatizo mahali, hatua kali zinachukuliwa ili kuonyesha mfano kwa jamii.

“Jambo la tatu katika mambo ambayo yanatupa shida ni hili suala la mapenzi kwa walimu na wanafunzi, katika kipindi hiki lilichukua asilimia 11.8 ya kesi zote kwani tulikuwa na walimu 211 walioshitakiwa kwa makosa ya kujihusisha na mapenzi kwa wanafunzi,”amesema Dk Komba.

Makosa mengine yaliyotajwa kuwasumbua walimu ni utoro kazini, kugushi vyeti, ukaidi na ulevi ambavyo ametaja kuwa vinawasumbua walimu katika maeneo mengi nchini hali aliyosema isipodhibitiwa inaweza kuharibu malengo ya Serikali.

Dk Komba amewaagiza walimu kuwa makini kwenye utumishi wao na kuiishi kauli mbiu yao kuwa ualimu ni kioo cha jamii hivyo wanatakiwa kuwa mfano kwa jamii na taasisi wanazozifanyia kazi ikiwemo kuwa kwenye mavazi yenye staha yasiyowatilia shaka watu.

Post a Comment

0 Comments