Vifo vya watu mashuhuri vilivyotikisa mwaka 2021

Vifo vya viongozi wa kitaifa, watendaji wa Serikali na wafanyabiashara wakubwa ni miongoni mwa matukio yaliyoitikisa nchi mwaka huu na kuacha simanzi kwa familia, ndugu, jamaa na marafiki hata Taifa kwa ujumla.

Baadhi ya vifo hivyo vimeandika historia mpya nchini na kuwa kumbukumbu kwa vizazi vijavyo kutokana na nafasi za watu hao kwenye jamii wanamoishi na mambo waliyoyafanya.

Kwa mara ya kwanza, Machi 17, Tanzania ilipata pigo kwa kuondokewa na Rais wa nchi akiwa madarakani. Siku hiyo, Makamu wa Rais wa wakati huo, Samia Suluhu Hassan alitangaza kifo cha Rais wa awamu ya tano, John Magufuli kilichotokea katika Hospitali ya Mzena jijini Dar es Salaam alikokuwa anatibiwa.

Hadi sasa Tanzania imewapoteza marais watatu, akiwamo Mwalimu Julius Nyerere aliyefariki Oktoba 14 mwaka 1999 na Benjamin Mkapa aliyefariki dunia Julai 24 mwaka jana. Viongozi hao walifariki wakiwa wamestaafu utumishi, isipokuwa Dk Magufuli aliyekuwa bado yungali madarakani.

Machi 26, Hayati Magufuli alizikwa nyumbani kwao huko Chato mkoani Geita baada ya mwili wake kuzungushwa katika mikoa kadhaa kuwapa wananchi fursa ya kumuaga na kutoa heshima zao za mwisho kabla ya kupumzishwa katika nyumba yake ya milele.

“Kwa kweli kifo cha Rais Magufuli kiliniumiza sana, nitamkumbuka kwa ujasiri wake wa kufanya uamuzi na kutupigania wafanyabiashara wadogo. Tutamkumbuka sana,” anasema Martin Sigala, mfanyabiashara katika eneo la Tabata Relini.

Kwa mujibu wa Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Makamu wa Rais alitakiwa kuapishwa kuwa Rais na ndicho kilichofanyika Machi 19, siku mbili baada ya kufariki Rais Magufuli.

Jaji Mkuu, Profesa Ibrahim Juma alimwapisha Samia kuwa Rais wa Tanzania kisha hatua za mazishi ya Dk Magufuli zikaendelea wakati uongozi wa Serikali umetimia.

Kiongozi mwingine aliyefariki mwaka huu ni aliyekuwa Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Maalim Seif Sharif Hamad. Kinara huyo wa siasa za Zanzibar alifariki Februari 17 katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili alikolazwa akitibiwa maradhi yaliyokuwa yanamsumbua.

Kabla ya kifo chake, Maalim Seif aliwahi kukiri kwamba alikuwa anaugua ugonjwa wa Uviko-19. Jambo hilo pia liliwahi kuelezwa na chama chake, ACT Wazalendo.

Mwanamapinduzi huyo alizikwa Februari 18 katika Kijiji cha Mtambwe huko Pemba, kisha Rais Hussein Mwinyi akamteua Othman Masoud Othman kutoka ACT Wazalendo kujaza nafasi iliyoachwa wazi na Maalim Seif.

“Kila mtu anatambua jinsi Maalim Seif alivyokuwa na nguvu visiwani Zanzibar, ni mmoja wa waasisi wa Serikali ya Umoja wa Kitaifa, Wazanzibari watamkumbuka kwa hilo na wanasiasa wana mengi ya kujifunza kutoka kwake,” anasema mchambuzi wa masuala ya siasa, Andrew Bomani.

Mawaziri na wabunge

Ndani ya mwaka huu, Tanzania imeshuhudia pia vifo vya mawaziri na wabunge ambao walikuwa wanawakilisha majimbo yao katika Bunge la 12.

Mawaziri waliofariki ni pamoja na aliyekuwa Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa akitokea Jimbo la Ushetu, Elias Kwandikwa aliyefariki Agosti 2 wakati akitibiwa maradhi yaliyokuwa yakimsumbua. Mwingine ni aliyekuwa Naibu Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Uwekezaji), William Ole Nasha ambaye alikuwa Mbunge wa Ngorongoro. Ole Nasha alifariki Septemba 27 jijini Dodoma na kuzikwa katika Kata ya Kakiseo wilayani Ngorongoro Mkoa wa Arusha.

Kwa upande wa wabunge waliofariki ni pamoja na aliyekuwa mbunge wa Muhambwe, Atashasta Nditiye, aliyekuwa Mbunge wa Konde, Khatib Said Haji na Mbunge wa Viti Maalumu kutoka Mkoa wa Manyara, Martha Umbula.

Vifo vya wabunge hawa, vililazimu uchaguzi kuitishwa upya kwenye majimbo yao ili kuziba nafasi zilizoachwa wazi.

Watendaji na wastaafu

Juni 29, Watanzania walikumbana na simanzi kufuatia kifo cha Mtendaji Mkuu wa Wakala wa Barabara Tanzania (Tanroads), Patrick Mfugale kilichotokea jijini Dodoma akiwa kwenye kikao kazi kabla ya kuanguka na kukimbizwa hospitali, ambako jitihada za kuokoa maisha yake zilishindikana.

Mfugale ni mmoja wa watendaji katika taasisi za umma ambao waliaminiwa na Serikali, hasa kutokana na utaalamu na ujuzi wake usio na shaka katika usanifu wa madaraja na kwa heshima hiyo, Hayati Magufuli aliliita daraja la juu la Tazara kwa jina lake, Daraja la Mfugale.

Kifo kingine ni cha mwanasiasa mkongwe, Chrisant Mzindakaya ambacho kilitokea Juni 7. Mzindakaya alifariki alipokuwa akitibiwa maradhi ya moyo katika Hospitali ya Taifa Muhimbili jijini Dar es Salaam.

Mzindakaya ndiye mbunge ambaye ametumikia nafasi hiyo kwa muda mrefu kuliko wote, akiwawakilisha wananchi wa jimboni kwake kwa miaka 45 mfululizo na katika muda huo alikuwa akiwakilisha majimbo ya Sumbawanga na Kyela kwa nyakati tofauti, huku akitumikia nafasi nyingine kama vile mkuu wa mkoa.

“Mzindakaya ni mmoja wa watu ambao walinivutia katika siasa, kwa bahati nzuri wakati naingia bungeni kwa mara ya kwanza nilimkuta. Alikuwa mahiri katika kujenga hoja na wakati wote alikuwa akisema ukweli,” anasema Magdalena Sakaya, mbunge wa zamani wa Kaliua.

Vifo vya wafanyabiashara

Sekta binafsi nayo ilitikiswa, hasa kutokana na vifo vya wafanyabiashara maarufu nchini ambao walikuwa wanamiliki kampuni kubwa wakiwa na ukwasi unaogusa maisha ya watu wengi ambao wameajiriwa kwenye kampuni zao.

Kifo cha Mwenyekiti wa Kampuni za Asas Group, Alhaj Faraj Ahmed Abri kilichotokea Agosti 13 jijini Dar es Salaam kiliibua simanzi kwa familia, wakazi wa Iringa na Taifa kwa ujumla kutokana na mchango wa mfanyabiashara huyo katika maendeleo ya mkoa huo na Taifa kwa ujumla.

Wengine waliofariki mwaka huu ni mfanyabiashara maarufu wa madini ya Tanzanite, Mathias Manga aliyewahi kuwa mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM (NEC), akiwa nchini Afrika Kusini.

Pamoja na umiliki wa mgodi wa Tanzanite wa Manga Gems uliopo kitalu D, marehemu Manga, aliyefariki Agosti 12 alikuwa mmiliki na mwendeshaji wa hoteli za Gold Crest zilizopo jijini Arusha na Mwanza na alikuwa anamiliki majumba kadhaa ya kifahari jijini Arusha.

Mfanyabiashara maarufu, Tanil Kumar Chandulal Somaiya alifariki dunia Agosti 11 jijini Dar es Salaam. Baadhi ya maeneo ya biashara zake alizokuwa amefanikiwa ni mawasiliano kupitia kampuni ya Shivacom na ile ya ulinzi ambayo ni Ultimate Security.

“Nahodha wa timu ya mpira akipata shida, timu yote inaweza kutetereka. Licha ya kuwa biashara zao bado zipo, tumepoteza rasilimali watu muhimu katika ukuaji wa biashara yoyote ile,” anasema Francis Nanai, Mkurugenzi Mtendaji wa Taasisi ya Sekta Binafsi Tanzania (TPSF).

Wafanyabiashara wengine waliofariki mwaka huu ni aliyekuwa mmiliki wa Hoteli ya Peacock, Joseph Mfugale aliyefariki Julai 31 jijini Dar es Salaam. Mfugale ni miongoni mwa wamiliki wa hoteli kubwa wazawa aliyepata mafanikio katika biashara hiyo, akimiliki hoteli jijini Dar es Salaam na nyingine mkoani Iringa.

Vilevile, mfanyabiashara maarufu wa mabasi ya Sumry, Hamoud Sumry alifariki Agosti 9 jijini Dar es Salaam, siku chache kabla ya kifo cha John Lamba, ambaye ni mfanyabiashara na mmiliki wa Hoteli ya Travertine jijini Dar es Salaam.

Viongozi, watendaji wa Serikali na wafanyabiashara hawa waligusa maisha ya watu, lakini Mwenyezi Mungu hakuwapa nafasi ya kuuvuka mwaka 2021, hivyo akaamua kuwatwaa.

TUANDIKIE MAONI YAKO HAPA CHINI

Je, wewe ni Mfanyabiashara na Unatamani Kutangaza Bidhaa Zako Kupitia Tovuti/Blog Yetu? Tafadhali, wasiliana nasi kupitia bandolaonline@gmail.com au WhatsaApp: + 255 766 365 560 au 0652 388 516

Post a Comment

0 Comments